Home » » CAG AMBWAGA AMANI

CAG AMBWAGA AMANI

Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory AmaniMAHAKAMA Kuu kanda ya Bukoba, imetupilia mbali kesi namba moja ya mwaka 2014, iliyofunguliwa na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amani alifungua kesi hiyo, akipinga ripoti ya ukaguzi uliyofanywa na CAG katika halmashauri hiyo Desemba mwaka jana, kuhusu utekelezwaji wa miradi ya maendeleo akidai kwamba alionewa.
Ripoti hiyo, iliyosomwa na aliyekuwa CAG, Ludovick Uttouh mbele ya Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri ilimtia hatiani Amani na aliyekuwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Hamis Kaputa kwamba waliendesha miradi hiyo kwa kukiuka utaratibu wa kutoshirikisha Baraza la Madiwani na wizara husika.
Katika hukumu yake juzi, Jaji G. J. Mjemmas, alisema kumshtaki CAG ni jambo linalowezekana lakini kwa suala hilo la kuhusu ripoti ya ukaguzi haiwezekani CAG kushtakiwa kwasababu alitumwa na Serikali kufanya kazi yake na imekamilika.
Jaji Mjemmas, aliagiza vyombo vingine vinavyohusika katika suala hilo, kuchukua hatua za haraka kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya CAG na kusisitiza kwamba kesi hiyo haitaweza kuwepo kabisa huku Amani akitakiwa kulipa gharama zote za kesi.
Hii si mara ya kwanza kwa Amani kufungua kesi ya kujaribu kupigania umeya wake, ambao aliupoteza alipotangaza kujiuzulu muda mfupi baada ya CAG kuwasilisha ripoti yake, lakini baadaye akaibuka na kukana kujiuzulu.
Kwa sasa, Amani amefungua kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba dhidi ya Mkurugenzi wa manispaa hiyo, akimtaka amruhusu aingie katika vikao vya Baraza la Madiwani akiwa mamlaka yake ya umeya na kurejeshewa haki zake zote za usafiri na mahitaji mengine.
Suala hilo, lilikataliwa na mkurugenzi akisema kuwa hamtambui kwa sababu kwa mujibu wa maelezo ya barua aliyopewa na serikali ili ampatie ina maana kwamba yeye si meya tena na hasa kwa kuzingatia tamko lake la kujiuzulu baada ya CAG kusoma ripoti yake.
Msimamo wa mkurugenzi huyo, ndio ulimlazimu Amani kupitia kwa mwanasheria wake kufungua shauri katika mahakama hiyo, ambayo juzi iliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 2 mwaka huu.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa