KUTOJIUNGA CHF KUNALETA PICHA MBAYA KAGERA-RC



Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe akifungua mkutano wa wadau mkoani humo jana

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba akitoa maelezo ya utangulizi kwa wadau.

 Mjumbe wa Bodi ya NHIF, Prof. Joseph Shija akitoa salaam za bodi kwa wadau wa Mfuko huo.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NHIF, Eugen Mikongoti na Mkurugenzi wa Takwimu na Utafiri, Michael Mhando wakisikiliza kwa makini hotuba ya Mkuu wa Mkoa.
Wadau wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa Uongozi wa NHIF.   
  =============  =============  ===========

Kutojiunga na CHF kunaleta picha mbaya Kagera-RC
Na Grace Michael, Kagera

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe amesema afya ni hazina kubwa kwa kila mwananchi ambayo inatakiwa kulindwa kwa gharama yoyote hivyo akazitaka Halmashauri mkoani humo kushindana katika uandikishaji wa kaya zinazojiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Amesema kuwa kitendo cha kushindwa kujiunga na Mfuko huo kinaleta picha mbaya mkoani humo kutokana na ukweli kwamba wananchi wanazo fursa nyingi za kujiiingizia kipato.

  Massawe aliyasema hayo jana mkoani hapa wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ulilenga kujadili mambo mbalimbali zikiwemo changamoto zinazoukabili Mfuko huo hatimaye huduma zake ziweze kuboreshwa.

"Afya ni hazina kubwa kwa kila mwananchi hivyo ni lazima suala hili tulione ni la muhimu na tulifanyie kazi, uchumi wa Mkoa huu ni mzuri tu...tusiwekeze afya zetu katika hali ya mashaka...wenzetu waheshimiwa madiwani, wabunge na viongozi wengine, hamasisheni wananchi kujiunga na Mfuko huu kwa kuwa unayo manufaa makubwa kwa afya zetu," alisema. 

Aliongeza kuwa ni lazima Halmashauri zishindane katika uandishaji wa kaya kujiunga na Mfuko huu ili lengo la kuwa na afya bora kwa wote lionekane kwa vitendo.

Alisema kuwa kutokuwepo kwa CHF ndani ya Halmashauri ni kuonesha kushindwa viongozi waliopo ndani ya Halmashauri husika, hivyo akaonya kuwa hali hiyo asingependa kuiona mkoani kwake.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wadau hao kutokuwa  wanaharakati katika kuchangia hoja mbalimbali kuhusiana na suala la Mfuko wa Afya ya Jamii hivyo akasisitiza kila mdau kuwa na mchango chanya ili kusaidia kuboresha huduma za Mfuko huo.

"Tusiwe kama wanaharakati ambao wanaangalia mambo kwa mtizamo hasi...lazima tuangalie kama kuna mahali pa kupongezwa Mfuko upongezwe na kama kuna eneo la kusahihiswa basi ifanyike hivyo ili kuutendea haki na uweze kudumu na kuhudumia wananchi wetu," alisema Massawe.

Aliongeza kuwa umuhimu wa suala la afya upo katika kila nchi na akasema kuwa katika nchi zingine kila mwananchi anatakiwa kuwa kwenye mfumo wa bima ili aweze kupata matibabu. Aidha aliupongeza Mfuko kwa hatua ya kusogeza huduma kwa wanachama wake hasa kwa kusogeza ofisi katika ngazi ya Mkoa kwani hiyo ndiyo hatua nzuri na yenye kuoneshwa mafanikio.  

"Natoa agizo kwa wakurugenzi wote kuhakikisha mnachangamkia fursa hii ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ili huduma katika vituo vyetu ziwe bora zaidi," alisema.

Massawe alitumia fursa hiyo kuuomba Mfuko kuendelea na uwekezaji katika miradi ya maendeleo katika sekta ya afya ikiwemo uwekezaji au ujenzi wa vituo vya matibabu vya mfano.  

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Prof. Joseph Shija, alitoa wito kwa watoa huduma kutumia fursa zinazotolewa na Mfuko huo kwa uzalendo na uadilifu mkubwa ili badae wananchi wote waweze kunufaika na mfuko.

Akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba, aliwataka wadau hao kutoa michango yao bila woga kwa kuwa ndio njia nzuri ya kusaidia kuboresha huduma zake.  

Baada ya mkutano huo wa wadau mkoani Kagera, timu nyingine ya Mfuko itaendesha mikutano katika Mikoa ya Tabora, Kilimanjaro na Tanga, lengo ni kuhakikisha wadau wanakutana na kujadili kwa pamoja ili kupata majibu ya uboreshaji wa huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

Welcome to Kagera Region Tanzania


Mkoa wa Kagera unapatikana kaskazini magharibi mwa nchi ya Tanzania. Makao makuu ya mkoa yapo katika mji wa Bukoba umbali wa kilometa 1500 kutoka Dar es Salaam, mkoa huu unapakana na nchi ya Uganda kwa kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa magharibi mkoa wa Kigoma, Mwanza kwa upande wa kusini na ziwa Victoria kwa upande wa mashariki. Vile vile mkoa wa Kagera uko kusini mwa ikweta kati ya 1 “00” na 2”45” latitudi. Kwa Iongitudo uko katika nyuzi 30”25” na 32”40” Mashariki mwa ‘greenwich'.
Mkoa wa Kagera ulijulikana kama “Ziwa Magharibi” jina hili lilidumu katika kipindi cha ukoloni na baada ya uhuru mpaka mwaka 1979 baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda.
Mkoa ulipata jina hili kutokana na mto Kagera ambao hutiririsha maji yake kutoka Rwanda kupitia kaskazini na kumwaga maji yake katika ziwa Victoria.
Mkoa wa Kagera una jumla ya eneo la kilomita za mraba 39,168 kati ya hizo kilometa za mraba 28,513 ni eneo la nchi kavu za kilomita 10,655 ni eneo la maji. Ukiacha mbali wilaya za Biharamulo na Chato ambazo ni tambarare sehemu kubwa ya mkoa ni yenye milima na vilima vilivyogawanywa na mabonde yenye matingatinga. Upande wa magharibi wa mkoa mito mingi inamwaga maji yale katika mto Kagera ambao nao humwaga maji yake katika ziwa Victoria.

Hali ya hewa
Hali ya hewa ya mkoa wa Kagera kwa ujumla ni ya joto la wastani wa 26.02 sentigredi. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,100 kwa mwaka kati ya mwezi Septemba na Januari na kati ya mwezi Machi na Mei. Mvua hizi ndizo zinazowezesha kuwepo kwauoto wa asili wa kuvutia katika maeneo mengi ya mkoa. Kwa miaka ya kawaida mkoa hupata mvua za uhakika za vuli na masika ambazo ni muhium kwa shughuli za kilimo na ufugaji.

UTAWALA
 
Wakati tunapata UHURU, mkoa wa Kagera ulikuwa na jumla ya wilaya nne (4), wilaya hizo ni Ngara ambayo ilianzishwa mwaka 1947, Biharamulo, Bukoba, na Karagwe mwaka 1958 ambayo ilizinduliwa rasmi na gavana wa kiingereza Sir Richard Turnbul. Aidha, mwaka 1975 wilaya mpya ya Muleba ilianzishwa kutoka kwenye wilaya ya Bukoba na mwaka 2007 wilaya ya Chato na Missenyi zilianzishwa na kuunda jumla ya wilaya 7 za mkoa wa Kagera.
Kwa sasa mkoa wa Kagera una jumla ya wilaya saba (7) na halmashauri 8. Wilaya hizo ni Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Chato, Karagwe, Missenyi na Ngara. Halmashauri ni Bukoba Manispaa, halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Chato, Karagwe na Missenyi.
Kisiasa mkoa una jumla ya majimbo 10 ya uchaguzi (Muleba 2, Karagwe 2, Ngara 1, Biharamulo 1, Missenyi 1, Bukoba Manispaa 1, Bukoba Vijijini 1 na Chato jimbo 1).

IDADI YA WATU
 
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 1967 mkoa ulikuwa na watu 658,712, mwaka 1978 watu 1,009,379, mwaka 1988 mkoa ulikuwa na watu 1,326,183 na mwaka 2002 watu 2,033,888. Ongezeko la idadi ya watu lilikuwa kwa wastani wa asilimia 2.7. Aidha, mwaka 2011 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 mkoa unakadiriwa kuwa na idadi ya watu 2,746,058.
Source: Tanzania Regions Site
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa