WAZIRI MKUU AAGIZA KUFUTWA UMILIKI WA MASHAMBA MAKUBWA 11 WILAYANI NGARA

·         Yana ukubwa ekari 7,700 katika vijiji viwili tu
·         Aagiza Afisa Ardhi arudishwe kutoka Rorya kusaidia uchunguzi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kufutwa mara moja umiliki wa mashamba makubwa 11 yenye ukubwa wa ekari 7,700  kwenye  vijiji vya Kasharazi na Rwakalemera wilayani Ngara Kagera, ambayo hayana hati na yametelekezwa.

Ametoa agizo hilo leo asubuhi  (Jumatano, Machi 16, 2016) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Kasulo na Rwakalemera katika kata ya Kasulo wilayani Ngara akiwa njiani kuelekea mkoa wa Geita.

Waziri Mkuu alilazimika kufanya mkutano huo mapema asubuhi baada ya kuamua kuitisha uongozi wa wilaya ya Ngara ufike kwenye mkutano huo ili kujibu kero za wananchi waliosimamisha msafara wake jana wakati akielekea Ngara mjini.

Uamuzi huo unafuatia hatua ya Waziri Mkuu kumwita kwenye mkutano huo Afisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Bi. Betty Munuo ili aeleze chanzo cha mgogoro wa ardhi katika vijiji hivyo.

Bi. Munuo ambaye amehamishiwa wilaya hiyo Agosti, mwaka jana,  alisema aliyakuta malalamiko hayo na amefanya uchambuzi wa majina ya wamiliki wote wa mashamba na walikuwa wanapanga kuwapatia notisi ili wajieleze.

Katika orodha yake, Bi. Munuo alitaja wamiliki 18 wa mashamba makubwa lakini kati yao ni wamiliki saba tu ambao mashamba yao yana hati lakini matatu ndiyo yameendelezwa na manne hayajaendelezwa.

Mashamba yaliyoendelezwa yanatumika kwa kilimo,  ufugaji na shule. Nayo yanamilikiwa na Dayosisi ya Rulenge (shamba na. 606 lenye ekari 161 liko Mbuba); Dario Zakaria (shamba na. 639 lenye ekari 282 liko Nyakariba) na Masista wa Mt. Fransisco (shamba na. 234 lenye ekari 759 liko Kasulo).

Mashamba manne yenye hati lakini yametelekezwa ambayo yote yako kijiji cha Rwakalemera ni ya Abdallah Sadala na. 235 lenye ekari 521; Mahsen Saidi shamba na. 333 lenye ekari 458; Mshengezi Nyambele shamba na. 746 lenye ekari 388 na  Mushengezi Nyambele shamba na. 745 lenye ekari 497.


Akitangaza uamuzi wake, Waziri Mkuu aliwataja wamiliki wa mashamba yasiyo na hati kuwa ni Bw. Joseph Rugumyamheto mwenye shamba na. 527 (ekari 505 liko Rwakalemera); Bw. Nicolaus Kidenke shamba halina namba na ukubwa wake haujulikani; Bw. Gwasa Angas Sababili shamba na. 714 (ekari 236 liko Kasharazi);  na Bw. Makumi Adili Rufyega (ekari 500 liko Rwakalemera).

Wamiliki wengine ambao mashamba yao yapo kijiji cha Rwakalemera ni Paulo Shikiri ekari 250; Frank Mukama Derila ekari 750; Godfrey Kitanga ekari 800; Philemon Mpanju ekari 200; Issa Sama ekari 500; Hekizayo Mtalitinya ekari 225 na Joel Nkinga ekari 1,250.

Waziri Mkuu aliagiza ifanyike sensa ili kubaini kama wamiliki wa mashamba hayo yote ni Watanzania au la. "Haya yenye hati nataka yafanyike mapitio ya hati zao na kubainisha ni namna gani walipatiwa hati hizo. Nataka taarifa inifikie ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe 20 Machi, 2016," alisema.

Ili kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu ameagiza kurejeshwa mara moja kwa aliyekuwa Afisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Bw. Enock Mponzi ambaye amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ili aje asaidie uchunguzi wa ugawaji wa maeneo hayo.

Alimtaka Mwenyekiti wa kijiji cha Rwakalemera, Bw. Brighton Kemikimba aitishe mkutano wa kijiji kabla ya tarehe 31 Machi 2016 na abainishe mashamba yote makubwa ambayo yanazidi ekari 50. Pia afuatilie kama yana kibali cha Baraza la Madiwani.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameagiza kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Bw. Colnel Ngudungi na kutaka arejeshwe wilayani humo kujibu tuhuma za kuhusika na upotevu wa fedha za mauzo ya mbao kutoka kwenye msitu wa Rumasi, wilayani humo.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera,  Bw. Adam Swai ameagizwa kumwandikia  barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga ili atekeleze maagizo hayo na Bw. Ngudungi arejeshwe Ngara kujibu tuhuma hizo. Bw. Ngudungi alihamishwa  kwenda Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga,  Agosti 2015.

Akiwa njiani kuelekea Ngara jana mchana (Machi 15, 2016), waziri Mkuu alisimamishwa katika kijiji cha Rwakalemera na wananchi wenye mabango wakiomba kurejeshewa ardhi ya kijiji huku baadhi yao wakidai wanatishiwa na bunduki pindi wakisogelea mashamba hayo makubwa.

Pia walidai kuuzwa kwa msitu wa Rumasi na mapato kutojulikana yalipokwenda huku wakidai kuwa kijiji chao hakipati mapato yoyote kutokana na minada ya ng’ombe inayofayika kijijini hapo wakati sharia inataka asilimia 20 ya mapato ibakizwe kijijini.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, MACHI 16, 2016.

HATIMAYE MWIGULU NCHEMBA AANZA KUTRANSFORM UFUGAJI HOLELA KWENDA UFUGAJI WA KISASA "BLOCKS"

Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Mh:Mwigulu Nchemba akimuangalia mmoja wadume  la ng'ombe anayetumika kuzalisha Mitamba kwenye kitaru namba 9 shamba la kitengule-Karagwe.Baadhi ya ng'ombe waliopo kitaru namba 9 shamba la kitengule ambapo kwenye block hii moja kuna Ng'ombe zaidi ya 800 wanaolishwa na kuhudumiwa vizuri na mmiliki wa kitaru hiki.Ng'ombe wakitoka kuogeshwa kwaajili ya kuua baadhi ya wadudu kama kupe wanaopendelea kukaa kwenye mwili wa ng'ombe.Hili ni moja ya josho la kisasa ndani ya kitaru namba 9.
Kufuatia ziara ya waziri mkuu,Mh:Kassim Majaliwa ndani ya mkoa wa Kagera akiwa ameambatana na waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani,Ziara hiyo imekuja na maagizo kadhaa ikiwamo wamiliki wote wa vitaru kwenye ranchi za Taifa ambao hawajaziendeleza waziachie mara moja na maeneo hayo yagawiwe upya,Waziri Mkuu ameagiza pia kwa wamiliki wa vitaaru ambao sio watanzania wajisalimishe au waondoke kwenye vitaru hivyo kabla hatua kali hazijaanza kuchukuliwa.
Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Mh:Mwigulu Nchemba akiwa na timu yake ya wataalamu wameshaanza kupitia vitaru vyote "blocks" na wamiliki wake ikiwepo pia idadinya mifugo kwa kila block,Hii leo Mwigulu Ncheba amekutana na wamiliki wa vitaru kwenye shamba la Kitangile-Karagwe na kuagiza wamiliki wote ambao hawajaendeleza maeneo wanayoyamiliki yanachukuliwa na serikali kwaajili ya kuwapatia watanzania wenye uwezo wa kuziendesha.
Mwigulu Nchemba ameagiza pia wamiliki wa vitaru kuacha mchezo wa kukodisha na kuingiza mifugo kutoka kwa wafugaji haramu wa nchi jirani,kitendo hicho ni kosa na yeyote atakayebainika anakwenda jela na adhabu kali itafuta.
Mbali na vitaru hivyo,Waziri Mkuu akishirikiana na waziri wa kilimo wameagiza ofisi ya mkuu wa mkoa wa kagera kuondoa wavamizi wote kwenye pori tengefu ya serikali kabla hatua zingine zinazofuata kuanza kutekelezwa.
Kupitia uwekezaji mzuri kwenye kitaru namba 9 cha shamba la Kitengule,Mwigulu Nchemba ametoa rai kwa wafugaji wote nchini kuanza kujipanga kufuga kwa mfumo wa vitaru ili kuachana na ufugaji holela unaopelekea migogoro mbalimbali na wakulima.
Picha/Maelezo na Festo Sanga Jr.

WAZIRI MKUU AMPA RAS KAGERA SIKU 5 AMLETEE TAARIFA


*Ni za matumizi ya sh. milioni 120 za Hospitali ya Mkoa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera na kumpa siku tano Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Adam Swai amletee taarifa juu matumizi ya sh. Milioni 80 ambazo ni fedha za UKIMWI.

Pia amemtaka ifikapo Machi 20, nwaka huu awasilishe taarifa nyingine ya matumizi ya sh. Milioni 40 za ukarabati wa jengo la wagonjwa maalum  (Grade A)

Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Jumanne,  Machi 15, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo baada ya kutembelea maeneo kadhaa yakiwemo wodi ya watoto, wodi ya wazazi, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU ) na chumba cha kuhifadhia maiti.

"Kulikuwa na frsha za ukimwi sh. Milioni 80 ambapo kila mtumishi alipaswa kupata sh. 200,000/- lakini ninyi mmewapa sh. 80,000 /-. RAS fedha hizi zimeenda wapi?  Nataka uniletee taarifa ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe 20 mwezi huu," alisema huku akishangiliwa.

"Kwa mujibu wa taarifa ya CAG pale grade A kuna mgogoro wa sh. milioni 40. Wewe taarifa unayo lakini hujaifanyia kazi yoyote.  Nataka tarehe 20 nayo hii pia niipate na nione umetoa mapendekezo gani."

Kuhusu tatizo la madaktari katika hospitali hiyo, Waziri Mkuu alisema atawasiliana na Waziri wa Afya ili madaktari watano ambao wanasubiri ajira rasmi lakini wameanza kazi kwa mkataba hospitali hapo wapewe ajira rasmi. Pia alisema amebaini upungufu wa madaktari bingwa uliopo katika hospitali hiyo.

Pia aliahidi kufuatilia maombi yao ya gari la wagonjwa hasa ikizingatiwa kuwa anayo maombi kama hayo kutoka hospitali za Mawenzi (Kilimanjaro), na Ligula (Mtwara).

Katika hatua nyingine,  Waziri Mkuu aliwapongeza watumishi wa hospitali hiyo kwa huduma zao nzuri wanazotoa kwa wagonjwa.  "Nineridhishwa na kauli walizotoa wagonjwa juu yenu. Tofauti na hospitali nyingine nilizopita, wao wamesema hawajatozwa fedha ili wapatiwe dawa. Nimefarijika sana."

"Endeleeni kuwa na huruma kwa wagonjwa. Endeleeni kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa. Hawa wagonjwa hawakuogopa kuelezea hisia zao. Wamesema kwa uwazi kabisa kwamba mnawajali," alisema.

Mapema,  akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu,  Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk.  Thomas Rutachunzibwa alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa pamoja na madaktari wa kawaida.

"Tunao madaktari 10 lakini wanaohitajika ni 30. Tunao madaktari wasaidizi wanane lakini wanaohitajika ni 23 na madaktari bingwa waliopo ni watatu tu lakini wanaohitajika ni 24. Tunaomba tupatiwe watumishi hawa ili tuweze kutoa huduma kulingana na matarajio ya wananchi wetu," alisema.

Akifafanua kuhusu mahitaji ya hospitali hiyo, Dk. Rutachunzibwa alisema wanahitaji sh. bilioni 1.8 kwa mwaka bila ya kuweka mishahara ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini. "Tunahitaji sh. milioni 802 kwa ajili ya matumizi ya kawaida lakini tunachopokea hivi sasa ni sh. milioni 299 ambayo ni sawa na asilimia 30 ya mahitaji yetu."

"Bajeti ya dawa tuliyotenga ni sh. milioni 960 lakini tunapokea sh. milioni 143 ambazo kiuhalisia zinatosha kwa matumizi ya miezi miwili tu. Tumelazimika kufanya marekebisho ya bei za dawa kwa ridhaa ya Bodi ya hospitali ili tuweze kumudu kutoa huduma kwa wananchi," alisema.

Alisema ili kubana mianya ya upotevu wa mapato, wanahitaji kuwa na kompyuta 15 lakini hadi sasa wamefanikiwa kununua kompyuta mbili tu ambazo ziko Grade A na idara ya wagonjwa wa nje (OPD) ili kuimarisha utaratibu wa ukusanyaji mapato.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, MACHI 15, 2016.

WAZIRI MKUU ATOA POLE KWA PROFESA ANNA TIBAIJUKA(MB) KWA KUFIWA NA MAMA YAKE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Kassim Majaliwa,akiweka saini katika kitabu cha maombolezo ya msiba wa mama wa Mbunge wa Muleba Kusini,Profesa Anna Tibaijuka, alipofika kutoa pole kwa wafiwa.Katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dk. Medard Kalemani na anayefuatia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni ,ambao waliongozana na Waziri Mkuu kwenda kutoa pole kwa wafiwa.
 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa(kulia),akimpa pole Mbunge wa Muleba Kusini,Profesa Anna Tibaijuka,ambaye amefiwa na mama yake.Waziri Mkuu yuko mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni(kulia),akimpa pole Mbunge wa Muleba Kusini,Profesa Anna Tibaijuka, aliyefiwa na mama yake,marehemu Aurelia Kajumulo.(Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)


Majaliwa azungumza na watumishi wa serikali, viongozi wa dini na wadau wa maendeleo wa mkoani Kagera

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amekutana na watumishi wa serikali, viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Kagera akiwa yupo mkoani humo katika ziara zake za kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo.
IMGS8477Baadhi ya watumishi wa serikali, viongozi wa dini na wadau wa maendeleo wa mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba akiwa katika ziara ya mkoa wa Kagera Machi 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa