MAWAZIRI 5 WATEMBELEA MPAKA WA TANZANIA, UGANDA

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
MAWAZIRI watano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wametembelea mpaka wa Tanzania na Uganda ili kutatua changamoto zinazoukabili mpaka huo na kuuboresha.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , William Lukuvi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Suzan Kolimba na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji , Mhandisi Isack Kamwelwe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya ardhi, miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa na mawaziri hao ni eneo la mpaka ya Tanzania na Uganda kwa upande unapopita mto Kagera na eneo la kivuko cha mpaka wa Tanzania na Uganda kilichopo Mtukula mkoani Kagera.
Katika ziara hiyo, mawaziri hao walijionea hali halisi ya maisha ya wakazi wa mipakani na jinsi wanavyohusiana na wenzao wa nchi ya jirani ya Uganda, ambapo wamekuwa wakishirikiana na kuishi kwa amani katika shughuli zao za kila siku.
CHANZO HABARI LEO

MAANDALIZI MKUTANO WA MAWAZIRI TANZANIA NA UGANDA: Ujumbe wa Tanzania wakagua maeneo itakapotekelezwa miradi ya umeme ya ushirikiano



 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa tatu kutoka kulia) akimweleza jambo Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Kagera, Mhandisi Francis Maze (wa kwanza kutoka kulia), wakati walipokuwa wakikagua eneo utakapotekelezwa Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 14 kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda, unaojulikana kama Murongo-Kikagati. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgavano. Wengine pichani ni Maofisa mbalimbali kutoka TANESCO, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Ardhi.
 Meneja wa Sheria anayeshughulikia Mikataba, kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mwesiga Mwesigwa (wa pili kutoka kushoto), akifafanua jambo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa kwanza kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgavano (katikati) wakati walipokuwa wakikagua eneo utakapotekelezwa Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 14 kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda, unaojulikana kama Murongo-Kikagati. Wa kwanza kushoto ni Meneja wa Uwekezaji kutoka TANESCO, Rwebangi Luteganya na wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Mikataba kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Evelyni Makala.
 Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Mkoa wa Kagera, Mhandisi Francis Maze (kulia), akifafanua jambo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) na Balozi wa Tanzania nchini Uganda (wa pili kutoka kulia), wakati walipokuwa wakikagua eneo utakapotekelezwa Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 35 wa Nsongezi kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda. Wengine kutoka kushoto ni Meneja wa Uwekezaji kutoka TANESCO, Rwebangi Luteganya, Mkurugenzi wa Mikataba kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Evelyni Makala na Meneja wa Sheria anayeshughulikia Mikataba, kutoka TANESCO, Mwesiga Mwesigwa.
 Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgavano na Meneja wa Sheria anayeshughulikia Mikataba, kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mwesiga Mwesigwa, wakitoka kukagua eneo la Nsongezi, utakapotekelezwa Mradi wa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda, wa kuzalisha umeme wa megawati 35.
 Meneja wa Uwekezaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Rwebangi Luteganya (kushoto), akiwaeleza jambo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgavano (kulia), wakati walipokuwa wakikagua eneo utakapotekelezwa Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 35 wa Nsongezi kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda.
 Sehemu ya Mto Kagera, unavyoonekana katika eneo la Nsongezi, mpakani mwa Tanzania na Uganda. Maji ya Mto huo yatatumika kuzalisha umeme wa megawati 35 kwa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya wananchi wake.
 Sehemu ya viongozi na wataalam mbalimbali kutoka Tanzania, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa pili kutoka kushoto), wakitoka kukagua eneo utakapotekelezwa Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 14 kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda, unaojulikana kama Murongo-Kikagati.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati), akisaini Kitabu cha Wageni katika Kituo cha Forodha Murongo, kilichopo mpakani mwa Tanzania na Uganda, alipokuwa katika ziara ya kazi kukagua maeneo itakapotekelezwa Miradi ya umeme kwa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Kushoto ni Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Francis Maze na kulia ni Ofisa Mfawidhi wa Kituo hicho cha Forodha, Ezekia Nonkwe.
 Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgavano, Ofisa Uhamiaji wa Kituo cha Murongo, Mnubi Mtaka na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, wakijadiliana jambo wakati Ujumbe wa Naibu Katibu Mkuu ulipopita mpakani hapo wakiwa katika ziara kukagua maeneo itakapotekelezwa Miradi ya umeme kwa ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Uganda.
Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgavano, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Francis Maze, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na Meneja Uwekezaji kutoka TANESCO, Rwabangi Luteganya, wakiangalia eneo utakapotekelezwa Mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 14 wa Murongo-Kikagati kwa ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Uganda.

Na Veronica Simba – Kagera

Baadhi ya viongozi na maofisa mbalimbali wa Serikali ya Tanzania, wamefanya ziara ya siku moja mpakani mwa Tanzania na Uganda, katika maeneo ya Nsongezi, Murongo na Kikagati, kwa ajili ya kukagua maeneo inapotarajiwa kutekelezwa miradi ya sekta ya nishati inayohusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, imefanyika leo Julai 27 ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, unaotarajiwa kufanyika Julai 29, wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera.
Kiongozi mwingine wa Serikali aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu Pallangyo katika ziara hiyo ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgavano.
Kwa mujibu wa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Francis Maze, miradi ya ushirikiano kwa sekta ya Nishati kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda inahusisha Mradi wa kuzalisha umeme wa Murongo-Kikagati wenye megawati 14, Mradi wa kuzalisha umeme wa Nsongezi wa megawati 35 pamoja na Mradi wa kupeleka umeme kwenye vijiji vya mpakani mwa nchi hizo mbili.
Mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda utatanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka nchi hizo mbili wanaoshughulika na masuala ya ushirikiano katika maeneo ya Mpaka, uliopangwa kufanyika kesho, Julai 28.
Maofisa wengine wa Serikali walioshiriki ziara ya kukagua maeneo itakapotekelezwa miradi ya nishati ni pamoja na Meneja wa Uwekezaji kutoka TANESCO, Rwebangi Luteganya, Mkurugenzi wa Mikataba kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Evelyni Makala, Meneja wa Sheria anayeshughulikia Mikataba, kutoka TANESCO, Mwesiga Mwesigwa na Mtaalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Raymond Bagenda.

JAFO AFURAHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI IHUNGO.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akifanya ukaguzi wa miundombinu inayojengwa katika Shule ya Sekondari Ihungo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa madarasa na mabweni katika Shule ya Sekondari Ihungo.
Jengo la bweni linalojengwa katika shule ya Sekondari Ihungo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akikagua majengo yanayojengwa katika Shule ya Sekondari Ihungo.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya Sekondari ya Omumwani wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo 

……………………………….. 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo amefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa shule ya wavulana ya kidato cha tano na sita ya Ihungo ambayo majengo yake yalibomoka kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mwaka Jana. 

Kutokana na kubomoka kwa majengo hayo, Serikali iliamua kuijenga upya kwa kutumia wakala wa majengo Tanzania (TBA). Akiwa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali mkoani Kagera, Jafo alitembelea shuleni hapo kukagua ujenzi wake. 

Naibu Waziri Jafo aliwapongeza wakandarasi kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ambapo kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti. Akizungumza na wananchi waliokuwepo katika eneo hilo, Jafo alisema serikali imeamua kuijenga sekondari hiyo kisasa zaidi. Alisema sekondari hiyo inatarajiwa kuwa sekondari ya mfano ndani ya Tanzania kwa kuwa na majengo ya kisasa zaidi kuliko sekondari zote hapa nchini. 

Hata hivyo, Jafo alitoa angalizo kwa sekondari hiyo kubaki kuwa sekondari ya wavulana kwani kutokana na uzuri wa miundombinu ya kisasa inayojengwa isije baadae wakaja watu na kubadilisha mawazo kuwa Chuo kikuu jambo ambalo sio sahihi. 

Alibainisha serikali imejipanga kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari kwasasa. Katika ziara hiyo, Jafo pia alitembelea shule ya Omumwani ambayo imeanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano ambao ni wasichana kwa mwaka huu. Alitoa maagizo kwa manispaa ya Bukoba kumalizia ukarabati wa maabara ndani ya wiki mbili zijazo ili kuwawezesha wanafunzi kufanya vyema zaidi katika masomo yao kivitendo.

CHADEMA 51 WAREJEA URAIANI


MAHAKAMA ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, imeamuru viongozi na wanachama 51 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuachiwa kwa dhamana.

Washtakiwa hao walikaa katika Gereza la Biharamulo mkoani Kagera kuanzia walipokamatwa Julai 7, mwaka huu.

Uamuzi huo umefanyika baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi lililowekwa na upande wa mashtaka la kuwanyima dhamana viongozi hao na wanachama wa chama hicho kwenye kesi ya kufanya mkusanyiko bila kuwa na kibali.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu wa Mahakama hiyo, Jovith Kato, baada ya kupitia hoja za pande zote za Jamhuri na utetezi.

Awali upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Semen Nzigo, baada ya kuwafikisha mahakamani viongozi na wafuasi 51 wa Chadema kwa madai ya kufanya mkusanyiko pasipo kuwa na kibali kwenye kata ya Muganza wilayani hapa, uliweka pingamizi washtakiwa wasipewe dhamana kwa madai ya kutovurugwa kwa upelelezi wa kesi hiyo.

Hoja hiyo ilikubaliwa na mahakama, hivyo washtakiwa wote walipelekwa mahabusu kwenye Gereza la Biharamulo kabla ya mawakili wa upande wa utetezi kuiomba mahakama kuwaondolea zuio hilo.

Baada ya majibizano ya kisheria Jumatatu wiki hii upande wa Jamhuri na utetezi uliokuwa ukiongozwa na mawakili kutoka kampuni ya Goldbelt Advocates, John Edward na Siwale Isambi kukamilika, mahakama ilisubiriwa kutoa uamuzi.
 
Aidha, mawakili wa upande wa utetezi walitumia kifungu cha 148(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kupinga zuio lililowekwa na Jamhuri.

Akisoma uamuzi huo, hakimu Kato alisema baada ya kuzipitia hoja zote na kwa kina, mahakama imekubali ombi la upande wa utetezi kuwa kifungu namba 148(5) kilichowekwa na upande wa Jamhuri ili kuzuia dhamana ya washtakiwa hakiendani na zuio hilo.

Hakimu aliongeza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Ibara ya 13(6)(b) inatamka wazi kuwa ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo.

Kadhalika Hakimu Kato alisema kwa mazoea ya uendeshaji wa mahakama katika mashauri ya jinai hayaliweki pingamizi hilo kuwa miongoni mwa makosa yanayonyima dhamana.

Kutokana na maelezo hayo, alisema washtakiwa wanayo haki ya kupewa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila moja na kwamba watatakiwa kuweka bondi ya Sh. 500,000 ndipo zitaandikwa hati za kuwafuata mahabusu kutoka katika Gereza la Biharamulo.

Wakati uamuzi huo unatolewa jana, washtakiwa hawakuletwa mahakamani. Aidha, Jumatatu hawakuletwa mahakamani.

Wakizungumzia hukumu hiyo nje ya mahakama, mawakili wa upande wa utetezi waliipongeza mahakama kwa kutenda haki, licha ya kwamba imetolewa kwa kuchelewa kutokana na wateja wao kusota mahabusu kwa siku 20.

Walisema baada ya uamuzi huo wa awali, wamejipanga vyema kuhakikisha wanapambana iwezekanavyo katika kesi ya msingi ambayo inadaiwa kuwa ya kukusanyika bila kibali ambayo itaanza baada ya polisi kukamilisha upelelezi.

Viongozi na wafuasi hao walikamatwa Julai 7 mwaka huu kwenye ukumbi wa Manzagata Kata ya Muganza wilayani Chato, wakiwa kwenye kikao cha ndani.

Baadhi ya viongozi walioko gerezani ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita, Phabian Mahenge, Katibu wa Chadema mkoa huo, Sudy Tuganyala, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoa, Vitus Makoye na Mwenyekiti wa Bavicha mkoa huo, Neema Chozaile.

Wengine ni Katibu wa Wilaya ya Chato, Mange Ludomya, Kaimu Mwenyekiti Wilaya ya Chato, Uhuru Selemani, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa wilaya hiyo, Meshark Tulasheshe na Katibu Mwenezi Kata ya Muganza, Marko Maduka.
 Chanzo:Nipashe

MAWAZIRI WATANO WAFANYA ZIARA MPAKA WA TANZANIA NA UGANDA



 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Luteni Kanali Denice Mwila kuhusu changamoto za mpaka huo wngine ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Suleman Jaffo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Suzan Kolimba.
 Jiwe la mpaka wa Tanzania na Uganda namba 30.
  Ujumbe wa Mawaziri kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania wakiwa juu ya Jiwe la mpaka wa Tanzania na Uganda namba 30.
 Moja ya jiwe la mpaka wa Tanzania na Uganda ambalo Mawaziri wamefanya ziara ya kuliona.
   Ujumbe wa Mawaziri kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania wakipita katika eneo la kivuko cha mpaka wa Tanzania na Uganda kilichopo Mtukula mkoani Kagera.
  Ujumbe wa Mawaziri kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania wakikagua huduma za vibali vya kuingia na kutoka nchini Tanzania na Uganda zilizopo Mtukula mkoani Kagera.

Eneo la mpaka ya Tanzania na Uganda kwa upande unapo pita mto Kagera.


Na. Hassan Mabuye
Mawaziri watano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watembelea mpaka wa Tanzania na Uganda ili kutatua changamoto zinazoukabili mpaka huo na kuuboresha.

Mawaziri hao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Suleman Jaffo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Suzan Kolimba na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe.

Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa na Mawaziri hao ni eneo la mpaka ya Tanzania na Uganda kwa upande unapo pita mto Kagera na eneo la kivuko cha mpaka wa Tanzania na Uganda kilichopo Mtukula mkoani Kagera.

Katika ziara hii Mawaziri hao wameweza kujionea hali halisi ya maisha ya wakazi wa mipakani na jinsi wanavyohusiana na wenzao wa nchi ya jirani ya Uganda ambapo wamekuwa wakishirikiana na kuishi kwa amani katika shughuli zao za kila siku.


Aidha, ziara hii ni maandalizi ya Mkutano wa ujirani mwema kati ya Mawaziri wa serikali ya Uganda na Mawaziri kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao unatarajiwa kufanyika mnamo tarehe 29 Julai 2017, Bukoba mkoani Kagera.

IGP SIRRO ASISITIZA WELEDI KWA POLISI




Imeandikwa na Demetrius Njimbwi, Jeshi la Polisi


IGP Simon Sirro.
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, amewataka askari wa jeshi hilo kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria na taratibu zitakazosaidia kujenga taswira chanya hasa wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Aliyasema hayo alipokutana na askari na maofisa wa mkoa wa Kagera, wakati akiwa kwenye mwendelezo wa ziara zake zenye lengo la kujitambulisha pamoja na kujua matatizo wanayokutana nayo wakati wakitekeleza majukumu yao.

Alisema kila askari analo jukumu mbele yake la kuhakikisha suala la uhalifu na wahalifu linadhibitiwa hususan kwa kuimarisha usalama wa raia na mali zao huku wakizingatia kuwa, mkoa huo unapakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.

Hata hivyo, katika ziara yake, IGP Sirro, amewahakikishia askari na maofisa kuwa, yupo tayari kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kuwataka askari kuongeza kasi ya kukabiliana na tishio la uhalifu na wahalifu ili kuifanya jamii kuishi kwa amani na utulivu.
CHANZO HABARI LEO

JPM AMUAGIZA NCHEMBA KUSITISHA KUWAPA URAIA WAKIMBIZI WA BURUNDI

Rais John Magufuli amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba kusimamisha kuwapa uraia raia wa Burundi kuanzia sasa.
Akizungumza Alhamisi Julai 20 wakati wa ziara yake mkoani Kagera, akiwa ameambatana na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza alimtaka asiwape uraia wanaotoka nchi nyingine.
“Rais amezungumza hapa kwa upole, Rais mwenyewe ana hofu ya Mungu, wazazi wake waliuawa, lakini anataka kushirikiana na Warundi wote kwa nini mnataka kuondoka kwenu,” amesema.
Awali, Rais Nkurunziza amezungumza na wananchi hao na kuwataka raia wa Burundi warudi nchini mwao kwani kwa sasa amani imerejea.
Kadhalika, Waziri Nchemba amesema katika kipindi cha 2016/17, Tanzania imewapa uraia wakimbizi wa Burundi 1060.
Pia, Waziri Nchemba amesema kati ya wakimbizi 247,000 waliopo nchini, 5,000 wameomba kurudi kwao.

Chanzo Mwananchi

JPM AAGIZA SH200 MILIONI ZA MRADI WA MAJI JESHINI ZITUMIKE KWA WANANCHI

 Rais John Magufuli ameagiza Sh200 milioni zilizopangwa kutumika katika mradi wa maji katika kambi ya jeshi zianze kuimarisha miradi ya maji kwa wananchi kwanza.

Akizungumza jana, Alhamisi Julai 20 katika ziara yake akiwa ameambatana na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza, Magufuli aliema amebaini kuwa pampu za maji wilayani Ngara zimeharibika kwa zaidi ya wiki tatu na kuwa wilaya hiyo ina uhaba mkubwa wa maji.
Alimuita, Mhandisi wa Maji ajieleze ni kwa nini pampu hizo hazifanyi kazi na baada ya kumsikiliza ndipo alipofanya uamuzi huo.
Akifafanua kuhusu hali ya maji, mhandisi huyo alisema awali visima vya maji wilayani hapo vilikuwa vikihudumia watu 400 lakini kwa sasa wilaya hiyo ina watu zaidi ya 240,000 na hivyo visima hivyo havitoshelezi.
“Tulikuwa tuna idadi ndogo ya watu sasa hivi imeongezeka, lakini tangu pampu iharibike, tumetengeneza mbili na kisima kimoja hakina pampu,” alisema.
Baada ya mhandisi huyo kufafanua hayo ndipo Rais alimuita Mkurugenzi wa Halmashauri kueleza mipango yake, ndipo Mkurugenzi huyo aliposema mradi wa maji wa Sh200 milioni utaanza kwanza katika kambi ya jeshi.
Kauli hiyo ndiyo iliyomfanya Rais Magufuli kushauri fedha hizo zitumike katika miradi ya maji katika makazi ya wananchi kwanza.
“Wanajeshi wapo 200 na wananchi wapo zaidi ya 20,000 sasa si bora waanze wananchi kwanza,” alisema.

Chanzo Mwananchi

IGP SIRRO AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI KAGERA


 Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro (kushoto) akizungumza na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Kamishna Msaidizi Muandamizi wa Polisi (SACP) Augusine Ollomi, muda mfupi alipowasili. IGP Sirro yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari pamoja na kujua chamgamoto wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao
 Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro, akizungumza na baadhi ya askari wa kikosi maalum kinachofanya doria za kupambana na wahalifu aliokutana nao katika eneo la Nyakanazi mkoani Kagera, IGP Sirro yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuzungumza na askari pamoja na kujua chamgamoto wanazokutananazo wakitekeleza majukumu yao.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (Mb), akitafakari jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro walipokutana katika viwanja vya Lemela wilayani Ngara mkoa wa Kagera, wakisubiri kuwasili kwa Rais Dkt. John Magufuli na Rais Pierre Nkurunziza wa Jamhuri ya Burundi. Picha na Demetrius Njimbwi – Jeshi la Polisi.

RAIS NKURUNZIZA AFANYA ZIARA RASMI YA KISERIKALI NCHINI TANZANIA.

Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza akiwasalimia wananchi wa Mji wa Ngara kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Posta Mjini Ngara 20 Julai 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza mara baada ya Rais wa Burundi kuwahutubia wananchi wa Mji wa Ngara kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Posta Mjini Ngara 20 Julai 2017.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia mamia ya wananchi wa Mji wa Ngara kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Posta Mjini Ngara Mkoani Kagera 20 Julai 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Lemela mjini Ngara Mkoani Kagera Julai 2017
Rais wa Jamuhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza akiwapungia wananchi alipowasili katika viwanja vya Lemela mjini Ngara Mkoani Kagera Julai 20,2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza wakiwa wamesimama wakipokea salamu za heshima kutoka kwa majeshi ya ulinzi na usalama.
Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza akikagua graride la lililoandaliwa na jeshi la ulinzi la Tanzania JWTZ katika viwanja vya Lemela mjini Ngara Mkoani Kagera Julai 20,2017
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mgeni wake Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza mara baada ya Kumpokea katika Uwanja vya Lemela mjini Ngara Mkoani Kagera 20 Julai 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza akiwasalimia wananchi wa Mji wa Ngara kwenye uwanja wa Lemela mjini Ngara Mkoani Kagera 20 Julai 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiteta Jambo na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza Mara baada ya kumpokea katika Mji wa Ngara kwenye uwanja vya Lemela mjini Ngara Mkoani Kagera 20 Julai 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Rais wa Jamuhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza kwa maongezi mjini Ngara Mkoani Kagera 20 Julai 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na ujumbe wake katika mazungumzo maalum ya kiserikali na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza na ujumbe wake Mjini Ngara Mkoani Kagera 20 Julai 2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza pamoja na mama Janeth Magufuli katika Maongezi.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgeni wake Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza wakiwapungia mikono wananchimwa mji wa ngara wakati wakiwasili katika uwanja wa posta mjini Ngara kwa ajili ya mkutano wa hadhara.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mgeni wake Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza wakiwapungia mikono wananchi wa mji wa Ngara waliohudhulia katika uwanja wa posta mjini Ngara kwa ajili ya Mkutano wa hadhara.
Umati wa ananchi wa mji wa Ngara waliohudhulia katika uwanja wa posta mjini Ngara kusikiliza Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa posta mjini Ngara 20 Julai 2017.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na mgeni wake Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza katika uwanja wa Lemela Mjini Ngara Mkoani Kagera 20 Julai 2017 baada ya kumaliza ziara yake Rasmi ya kiserikali Nchini. PICHA NA IKULU
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa