WAVUVI WAANDAMANA KUPINGA UVAMIZI

ZAIDI ya wavuvi 30 wa Kisiwa cha Mazinga, Kata ya Mazinga wilayani Muleba, wameandamana hadi kituo cha polisi cha wilaya, kulalamikia kutokuwepo ulinzi katika Ziwa Victoria, kiasi cha kutoa mwanya kwa majambazi kuwavamia na kuwapora zana za uvuvi.
Wakizungumza na Tanzania Daima mbele ya kituo cha polisi, wavuvi hao walisema wameamua kuandamana kutokana na kuongezeka kwa uvamizi huo, huku Jeshi la Polisi likionekana kutochukua hatua madhubuti za kuimarisha ulinzi.
Walisema mwishoni mwa wiki iliyopita kundi la majambazi liliwavamia wavuvi watano na kuwashambulia kwa mapanga, kisha kuwapora zana zao za uvuvi zenye thamani zaidi ya sh milioni 60.
Katika shambulizi hilo, majambazi hao waliwajeruhi Nicolaus Cleophas (33), Amidu Hussein (32 ), Mussa Antony (28) Medson Muhanika (30) na Juma Said (40 ) wote wakazi wa Mulumo Mazinga.
Walidai pia kuwa hivi karibuni kundi la majambazi wenye silaha za moto lilivamia kisiwa hicho na kupora zana za uvuvi mbalimbali, zikiwemo injini za mitumbwi sita zenye thamani ya sh milioni 18 pamoja na kuwajeruhi kwa mapanga wavuvi sita.
Imedaiwa kwa majambazi hao wamekuwa wakifanya uporaji kila wanapojisikia kwa kuwa wanajua Jeshi la Polisi wilayani humo haliwezi kufanya chochote.
Thomas Josia, mmoja wa wamiliki wa mitumbwi, alisema wakati wa kutoza kodi mbalimbali serikali inakuwa ya kwanza kufika visiwani humo huku wavuvi wakiwa mstari wa mbele kulipa, lakini serikali inakwama kuchukua hatua za haraka kuwalinda.
Diwani wa Kata hiyo, Alex  Bakenjela, alisema  wamezungumza na Jeshi la Polisi ambapo wamekubaliana kushirikiana ili kubaini chanzo cha ujambazi huo na njia za kukabiliana nao.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, George Mayunga, alisema hana taarifa za kuvamiwa kwa wavuvi hao, lakini akaahidi kulifuatilia suala hilo ili walipatie ufumbuzi kwa lengo la wananchi wafanye kazi zao bila hofu.
Chanzo:Tanzania Daima 

BOTI YAZAMA,YAUA WATANO

WAFANYABIASHARA watano wamekufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria ya Mv. Kitoko2 kuzama kwenye Ziwa Victoria kwa madai ya kuzidisha uzito.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alikiri kutokea kwa ajali hiyo Mei 23, 2014 saa nane usiku baada ya injini ya boti hiyo kuzima ghafla ikiwa safarini.
Alisema boti hiyo ilikuwa ikitoka Bugombe kupitia Kasenye kuelekea Mganza na abiria watano, kati yao mwili wa Jane Mlekatete (36) raia wa Rwanda uliopolewa.
Aliwataja wengine waliokuwepo kwenye boti hiyo kuwa ni Chikola Filbert (22) na Mapinduzi Daud (38), wengine walitambuliwa kwa jina moja ambao ni Asha na Suzy.
Chanzo:Tanzania Daima

Simanzi zatawala mazishi ya meneja wa Ewura

Waombolezaji wakijiandaa kushusha kaburini jeneza la aliyekuwa Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza aliyezikwa kijijini kwao Mulukulazo, Ngara mkoani Kagera jana. 

Simanzi, majonzi na kila aina ya huzuni vilitawala makaburini pamoja na minong’ono ya hapa na pale kuhusu mazingira ya kifo cha aliyekuwa meneja wa biashara ya petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza.
Gashaza aliyefariki Mei 18 mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha jijini Dar es Salaam muda mfupi akitokea Dodoma kikazi, alizikwa jana nyumbani kwao katika Kijiji cha Mulukulazo.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costa Kanyasu ni miongoni mwa mamia ya waombolezaji, wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki, viongozi wa dini na vyama vya siasa waliojitokeza kumzika Gashaza.
Akiongoza ibada ya mazishi hayo, Mchungaji Philipo Mvunyi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera, alisema wanafamilia, ndugu na jamaa wachukulie msiba huo kama mapenzi ya Mungu kwa kuwa kila mwanadamu kapangiwa mazingira ya kuondoka duniani.
Alisema kila mmoja katika familia, Serikalini alikokuwa akifanya kazi na hata watumishi wenzake na marafiki watakuwa na maswali mengi kuhusu kifo hicho, lakini wamtumaini Mungu.
Mkurugenzi wa mafuta wa Ewura, Godwin Samwel alisema kutokana na kifo cha mtumishi huyo, ofisi ya Ewura kwa kushirikiana na vyombo vya dola wanashirikiana kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alitangaza kuunda jopo hilo litakaloongozwa na mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo, Jaffary Mohamed atakayeshirikiana na wataalamu wa Maabara Kuu ya Polisi, daktari bingwa wa polisi na maofisa wa Serikali.
Alisema uchunguzi unafanyika ili kuondoa utata ulioanza kujitokeza kuhusu kifo hicho.
Chanzo;Mwananchi

Jamii yaaswa kuinua elimu

JAMII imetakiwa kufanya mabadiliko chanya katika elimu kwa kuwekeza na kupeleka watoto shule ili kuongeza uhamasishaji wa ufaulu mzuri kwa wahitimu ambao utasaidia kuchangia maendeleo ya haraka.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na mmiliki wa Shule ya Awali na Msingi ya New Vision iliyoko Kata ya Mugajwale, Tarafa ya Rubare, Wilaya ya Bukoba, Prosper Nduke, alipozungumza na Tanzania Daima.
Nduke alisema kumekuwa na mwamko hafifu katika jamii kuhusiana na suala la elimu, badala yake wazazi na jamii nyingi zimekuwa zikitumia muda na rasilimali kubwa kwa ajili ya mambo yasiyokuwa na tija.
Alisema wengine wamekuwa wakisifia na kuzitamani shule zinazotoa elimu bora, lakini wakiwa hawajali, wala kulipa ada na michango inayotakiwa.
“Ili taifa letu lipige hatua, hasa katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia, lazima tubadilike kwa kufuatilia maendeleo  yao na kuwajibika kwa kila jambo maana elimu ni gharama,” alisema Nduke.
Alieleza kuwa aliamua kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuanzisha shule hiyo mwaka 2003 ili kuinua elimu kwa watu waishio vijijini, hasa kwa wasichana waliokuwa wanafanya kazi za ndani.
Hata hivyo, Nduke ametoa rai kwa baadhi ya wamiliki wa shule kuacha tabia ya kuwakaririsha mitihani watoto ili kuwajengea uelewa zaidi na kuwezesha taifa kupata wasomi na wataalamu wenye uwezo wa kusaidia kuleta maendeleo.
Chanzo:Tanzania Daima 

HUDUMA ZA UJUMBE MFUPI WA MANENO (SMS) ZAZUIWA MKOANI KAGERA


Kwa takriban mwezi sasa watumiaji wa simu za mkononi ya Vodacom hawawezi kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwenda kwa watumiaji wa airtel kwa sababu amabzo hazijawekwa wazi.

Mtandao wa Harakatinews umefanya mahojiano na wasemaji wa Vodacom kwa bukoba mjini amabo wamekiri kuwepo tatatizo hilo lakini wanaongeza kwamba tatizo haliko kwako (vodacom) bali lipo Airtel ambapo juhudu za kuwapata wasemaji wa Airtel bado zinaendelea.



"Hili tatizo ni kweli lipo,na wateja wetu wanalalamika sana lakini  halipo kwetu bali lipo kwa wenzetu ingawa linashuguhulikiwa' alisema afisa wa vodacom Bukoba mjini.

Uchuguzi wa mtandao huu umebaini kwamba watu wengi kwa kagera wanaotumia mtandao wa Vodacom   hawajui kwamba hawezi kutuma SMS kwa jamaa zao wanaotumia mtandao wa airtel.

Tutaendelea kuwajuza kama tatatizo limetatuliwa.

Chanzo: Harakatinews

PINDA:SERIKALI HAIMTAMBUIMEYA BUKOBA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
 
Serikali haimtambui Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatoli Amani, kwa kuwa alijiuzulu mbele ya Baraza la Madiwani.
Hata hivyo kiongozi huyo alikana maamuzi yake na kuendelea kufanya shughuli za umeya ambazo serikali iliagiza zifanywe na Naibu Meya.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia  bajeti ya ofisi yake  na Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Khamis Kagasheki, kumtupia lawama Pinda  kushindwa kutatua mgogoro huo kwa miaka mwili.

"Nasisitiza Amani  si Meya tangu siku alipojiuzulu, alitoa tamko hili kutokana na ushauri uliokuwa umetolewa,”  alisema.

Alieleza kuwa  alichukua hatua mbalimbali ikiwa ni  kuunda kamati ya mkuu wa mkoa na  kuihusisha ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyefanya ukaguzi na kuandaa ripoti ambayo iliionyesha kasoro nyingi  na kuagiza kuwa kwa mazingira hayo Meya ajiuzulu pamoja na wataalamu waliohusika.

"Barua niliyoletewa na Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri, aliyehudhuria kikao kile, Meya alikubali kujiuzulu mbele ya Baraza la Madiwani, lilikuwa jambo la wazi katamka amekubali na kuandika barua ya  kuthibitisha, lakini muda kidogo pakatokea zogo ambalo sijui chanzo chake," alisema.

Pia alisema  madiwani walifungua kesi kuitaka mahakama iagize madiwani wa Manispaa ya Bukoba wasikutane  mpaka suala hilo litakapomalizika na kwamba kama kiongozi walipokea uamuzi huo na kuomba wanasheria kupinga uamuzi huo ili kazi za manispaa ziendelee.

Alisema shughuli za maendeleo zimesimama na kwamba madiwani hawawezi kuendelea kukutana kwa kuwa watakuwa wanakwenda kinyume na uamuzi wa mahakama.

Aidha, alimwagiza Mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu Fabian Massawe, kuzungumza na madiwani kuwa wananchi ndiyo wanaumia katika zoezi hilo na ni heri kuondoa kesi mahakamani.

"...kuliko kujifunga baraza lisikutane wana miradi ya mabilioni ya fedha, hakuna chochote kinachoweza kufanyika Bukoba, hili si jambo la busara kwa kiongozi unajua suala hili haliwasaidii wananchi wako lakini unasema potembelea mbalo, hili linanisumbua kidogo," alifafanua.

Hata hivyo,  hadi sasa Meya huyo hajaandika kwa maandishi kujiuzulu kwake na kubaki kwa maandishi kama alivyosema kwenye kikao huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa kwa madiwani hao.

Mgogoro huo kati ya viongozi hao unahusishwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa soko kuu la Bukoba na upimaji wa viwanja 5,000, miradi ambayo Kagasheki anadai ni ya kifisadi kwa madai kwamba mikataba yake haiko wazi na mmojawapo haujafanyiwa upembuzi yakinifu.

Baada ya mvutano mkali wa ndani CCM  mkoa wa Kagera chama hicho kiliwasimamisha madiwani tisa, lakini siku chache baadaye CCM Taifa iliwarejeshea nafasi zao.
CHANZO: NIPASHE

KAGASHEKI:PINDA NI DHAIFU

Asema kwa miaka miwili ameshindwa kuchukua hatua
  Shabibi naye apigilia msumari, akataa kuunga mkono bajeti
Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM),Balozi Khamis Kagasheki,
 
Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Khamis Kagasheki, amemtupia lawama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kushindwa kutumia nafasi yake kutatua mgogoro wa Manispaa ya Bukoba na kukaa kimya huku akiendelea kumtambua Meya Anatory Amani, ambaye alijiuzulu kisha kukana maamuzi yake.
Amani alijiuzulu wadhifa wake miezi mitano iliyopita baada ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi katika manispaa hiyo na kugundua matumizi mabaya ya fedha za halmashauri hiyo.

Balozi Kagasheki alitoa lawama hizo jana wakati akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2014/15 na kusema kuwa mgogoro huo unaitia aibu serikali kwa kuwa Amani alijiuzulu Januari, mwaka huu mbele ya viongozi wa mkoa wa Kagera, lakini baadaye alitangaza kuwa kurejea madarakani kinyemela.

Hata hivyo, alimshukuru Rais Jakaya Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuingilia katika kuchukua hatua katika mgogoro huo kwa kuagiza mamlaka husika kuchukua hatua, lakini ofisi ya Waziri Mkuu ilishindwa kuchukua hatua zozote na kwamba haikuwatendea haki wananchi wa manispaa hiyo.

Alisema CAG alitoa ripoti yake na kutokana na ripoti hiyo, Amani alitamka mbele ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), CAG, Mkuu wa mkoa wa Kagera  na viongozi wengine kisha alitangaza kuwa alijiuzulu, lakini baada ya muda alikana maamuzi yake na kudai kuwa bado ni meya.

”Hakuishia hapo, aliitisha kikao na waandishi wa habari na kusema hajajiuzulu na hakuishia hapo, alimtukana, akamtukana CAG na serikali na hivi sasa ninapozungumza anaendelea na uongozi...inasikitisha kwa serikali yetu katika kusimamia na uendeshaji wa mambo, hakuna kilichofanyika wala kauli ya serikali kuwa alishajiuzulu,” alisema Balozi Kagasheki.

Alisema Aprili 30, mwaka huu, Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera alimwandikia Katibu Mkuu Tamisemi, akieleza kuwa ofisi ya Mkuu wa mkoa inaelewa kuwa meya huyo alijiuzulu katika nafasi yake na kueleza kuhusu yanayoendelea ili kama kuna maamuzi yoyote yatolewe.

Balozi Kagasheki alisema maamuzi yamefanyika, lakini utekelezaji umekuwa tabu na kwamba wakati wa kuhitimisha Bajeti hiyo, Pinda atoe maelezo kama serikali inamtambua kama Amani ni meya au la kwa kuwa mgogoro huo hauna manufaa yoyote.

Balozi Kagasheki alisema Manispaa ya Bukoba  haina bajeti bali imepachikwa kwenye bajeti ya Mkuu wa Mkoa kwa miaka miwili sasa na hakuna vikao vya madiwani vilivyofanyika na kusema kwamba hiyo ni aibu.

Balozi Kagasheki alisema kuwa inashangaza mgogoro huo kutofanyiwa kazi licha ya maamuzi na mapendekezo ya CAG kufanyika, lakini hatua zinashindikana kuchukuliwa na Waziri Mkuu.

”Wananchi wa Manispaa ya Bukoba wamekuwa ni watoto wapweke ambao ofisiya Waziri Mkuu haikuwajali sana, mgogoro umekuwapo tangu Aprili mwaka 2012 …mwaka 2014 ni zaidi ya miaka miwili,” alisema na kuongeza:

“Mgogoro umekuwapo bila kuwa na suluhisho, bila uwezo wa kulitatua...bado mnataka watu wa Bukoba wafurahie kuwa mnawajali, Rais anazungumzia maamuzi yakifanywa yasikilizwe, leo huwezi kuwaambia serikali inawajali wakati hakuna kinachofanyika."

”Mimi mwenyewe nilikuwa waziri kwenye serikali, haya yakanikuta sasa mbunge wa kawaida itakuwa namna gani...suala hili lipo kwenye Kamati Kuu ya CCM kwa muda mrefu,” alisema.

Mara baada ya Balozi Kagasheki kuzungumza, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Paulina Gekul, alisema kuwa suala hilo lililetwa kwenye Kamati ya LAAC ikapitishwa kinyemela baada ya kujadiliwa juu juu, lakini wakati Mbunge wa Jimbo hilo anazungumza Waziri Mkuu alikuwa anapiga 'story' na kwamba tatizo kama hilo lipo Halmashauri ya Ilemela na kuomba mwongozo kama Pinda anaruhusiwa kuendelea kuongea wakati mambo ya msingi yanazungumziwa.

Naibu Spika, Job Ndugai, alikemea baadhi ya wabunge wanaokwenda kuzungumza naWaziri Mkuu wakati masuala muhimu anayopaswa kuyasikia yanazungumzwa na kwamba ataanza kuwakataza wabunge wanaozungumza na Waziri Mkuu na kumfanya asisikilize vizuri.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema Waziri Mkuu ndani ya Bunge hilo ni Mbunge, Kiongozi wa Shughuli za serikali Bungeni na kwamba shughuli za serikali zinaendelea na ndani ya Bunge hilo kuna pande mbili za walioko serikalini na wasiokuwapo.

”Kuna consultation (mashauriano) muhimu sana, lazima ziendelee, haiwezekani kiongozi wa shughuli za serikali kwenye jengo hili na siyo nje, kwa vyovyote nakubalina na ushauri wenu kwa wenye maoni ya kauwaida ya kiofisi wanaweza kusubiri na kwenda ofisini kwake,” alisema Lukuvi.

SHABIBY, KESSI WAMVAA PINDA
Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, alisema hataunga mkono bajeti ya Waziri Mkuu kwa kuwa kwenye jimbo lake serikali imekuwa ikitoa ahadi hewa za kukabiliana na tatizo la maji.

”Kila mwaka kwenye Bajeti ya Waziri Mkuu najibiwa serikali imefikia asilimia 80 hadi 84, wananchi wangu wananunua maji galoni la lita 20 kwa Shilingi 1,000, kila Waziri ni ahadi na mipango mingi isiyotekelezeka,” alisema.

Shabiby alisema Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, alifika kwenye jimbo hilo akiwa ameambatana na wataalamu mbalimbali, lakini hadi sasa hakuna maji na kwamba hataunga mkono bajeti ya wizara yoyote ambayo haitekelezeki.

Alisema Waziri Mkuu ndiye hajafika kwenye jimbo hilo kutoa ahadi na kwamba baadhi ya viongozi wa CCM wanamshutumu kuwa amekula fedha hizo.

Mbunge wa Nkasi (CCM), Alli Kessy, alisema Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, aliwadanganya wananchi wa vijiji vya Namanyere na Machi kuwa watapata majisafi na salama.

Alisema serikali inafanya sherehe kubwa kwa gharama kubwa na kuacha kupeleka huduma muhimu kwa wananchi na wao kuishi peponi na wananchi kuishi mbunguni na kwamba bajeti ya Waziri Mkuu kwa kiasi kikubwa ielekezwe kwenye majimbo yaliyoaachwa nyuma kimaendeleo.
CHANZO: NIPASHE

FLAVIANA MATATA MV Bukoba May 21st, 1996






On May 21st 1996, Tanzania encountered an overwhelming tragedy when MV Bukoba ship sank, leading to the loss of hundred of lives one of them being my dearly beloved mother.
I hearby invite you all to join my family along with all those who lost their loved ones on a mass to commemorate them to be held on 21st May 2014, 12:00pm, at the MV Bukoba Cemetry Nyakato Mwanza.
It will also be a day to remind and emphasize ourselves on the significance of routine marine vehicles safety inspection.
MAy the Lord God rest in peace the souls of those who lost lives, Amen 
Credit:Gonga Mx 

ALIYEJIFUNGUA PACHA WANNE AOMBA MSAADA

MKAZI wa Kijiji Chakijage, Kata ya Rwabwere, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, aliyejifungua watoto wanne pacha, Jodephina Rugambwa (30), ameiomba serikali kumpatia msaada ili kumsaidia kulea watoto wake.
Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea nyumbani kwake jana, alisema furaha ya kupata watoto wake hao aliojifungua Machi 23, mwaka huu inaanza kutoweka kwa kuwa anashindwa kuwatunza kutokana na kipato duni alichonacho.
“Mimi na mume wangu ni wakulima wadogo wenye kipato kisichoweza kutusaidia kwa
wakati huu kuwatunza watoto hawa, hivyo tunaomba msaada wa hali na mali kutoka serikalini na kwa wasamaria wema,” alisema.
Alisema mbali na watoto hao wanne, familia yake imejaliwa watoto wengine watatu ambao wawili wanasoma.
Hata hivyo, mama huyo pamoja na mumewe Donati Anatory (38), wameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, wasamaria wema pamoja na wajumbe wa Baraza la Madiwani wilayani humo kwa msaada wao wa hali na mali uliofikia hadi sasa kiasi cha sh 400,000.
Watoto hao pacha, wa kike wakiwa watatu na mvulana mmoja walizaliwa salama wakiwa na afya njema.
Chanzo:Tanzania Daima 

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AZINDUA RASMI SHEREHE ZA MBIO ZA MWENGE WA UHURU MKOANI KAGERA LEO.



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwasha Mwenge wa Uhuru wakati wa Sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge huo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba Mkoa wa Kagera leo Mei 2, 2014. Mwenge huo unatarajia kuitimisha mbio zake Oktoba 14 mkoani Tabora, ambapo zinatarajia kufungwa na mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete. Picha na OMR


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Mwenge wa Uhuru, Kiongozi wa mbio za Mwenge Taifa, Rachel Kasanda, baada ya kuuwasha rasmi wakati wa Sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge huo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba Mkoa wa Kagera leo Mei 2, 2014. Mwenge huo unatarajia kuitimisha mbio zake Oktoba 14 mkoani Tabora, ambapo zinatarajia kufungwa na mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete. Picha na OMR
 
 Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Masawe, akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge Taifa, Rachel Kasanda, baada ya kukabidhiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati wa Sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge huo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba Mkoa wa Kagera leo Mei 2, 2014. Mwenge huo unatarajia kuitimisha mbio zake Oktoba 14 mkoani Tabora, ambapo zinatarajia kufungwa na mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete. Picha na OMR

 Vijana wenye dhamana ya kukimbiza mwenge wa Uhuru 2014, wakianza rasmi mbio hizo baada ya kuwashwa na kukabidhiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati wa Sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge huo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba Mkoa wa Kagera leo Mei 2, 2014. Mwenge huo unatarajia kuitimisha mbio zake Oktoba 14 mkoani Tabora, ambapo zinatarajia kufungwa na mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete. Picha na OMR
 Makamu wa Rais Dkt. Bilal, akishiriki kuimba wimbo wa Taifa.
 Vijana wa Haraiki wakionyesha umahiri wao kwa kutoa burudani.
 Wasanii wa bendi ya Kakao ya mjini Bukoba, wakitoa burudani wakati wa sherehe hizo.
 Msanii wa muziki wa Kizazi kipya kutoka mjini Zanzibar, It, akiimba wimbo maalumu wa kuhamasisha mbio za mwenge.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wananchi wa Mkoa wa Kagera, wakati wa Sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge huo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba Mkoa wa Kagera leo Mei 2, 2014. Mwenge huo unatarajia kuitimisha mbio zake Oktoba 14 mkoani Tabora, ambapo zinatarajia kufungwa na mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete. Picha na OMR



Baadhi ya wageni waalikwa, Wakuu wa Wilaya za mkoa ya Tanzania Bara na Visiwani, waliohudhuria sherehe hizo za uzinduzi. Picha na OMR

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL, AWASILI MJINI BUKOBA MKOA WA KAGERA JIONI HII KUWASHA MWENGE WA UHURU KESHO



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara, mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa mjini Bukoba jioni hii kwa ajili ya kuwasha Mwenge wa Uhuru kesho katika hafla itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Mkoa wa Kagera.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akivishwa Skafu na Vijana wa 'Scout' wa mkoa wa Kagera, baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa mjini Bukoba jioni hii kwa ajili ya kuwasha Mwenge wa Uhuru kesho katika hafla itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Mkoa wa Kagera.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na baadhi ya viongozi, waliompokea kwenye uwanja wa Ndege wa mjini Bukoba leo jioni.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhingo Rweyemamu, baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa mjini Bukoba jioni hii kwa ajili ya kuwasha Mwenge wa Uhuru kesho katika hafla itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Mkoa wa Kagera.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, mkewe Mama Zakhia Bilal, wakifurahia ngoma ya asili ya kabila ya Wahaya baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa mjini Bukoba jioni hii kwa ajili ya kuwasha Mwenge wa Uhuru kesho katika hafla itakayofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Mkoa wa Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Masawe, akisoma Taarifa ya Mkoa mbele ya Makamu wa Rais Dkt. Bilal.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa