Waombolezaji wakijiandaa kushusha kaburini jeneza la aliyekuwa Meneja
Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura),
Julius Gashaza aliyezikwa kijijini kwao Mulukulazo, Ngara mkoani Kagera
jana.
Simanzi, majonzi na kila aina ya huzuni vilitawala makaburini
pamoja na minong’ono ya hapa na pale kuhusu mazingira ya kifo cha
aliyekuwa meneja wa biashara ya petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza.
Gashaza aliyefariki Mei 18 mwaka huu katika
mazingira ya kutatanisha jijini Dar es Salaam muda mfupi akitokea Dodoma
kikazi, alizikwa jana nyumbani kwao katika Kijiji cha Mulukulazo.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costa Kanyasu ni miongoni
mwa mamia ya waombolezaji, wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki,
viongozi wa dini na vyama vya siasa waliojitokeza kumzika Gashaza.
Akiongoza ibada ya mazishi hayo, Mchungaji Philipo
Mvunyi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kagera, alisema wanafamilia,
ndugu na jamaa wachukulie msiba huo kama mapenzi ya Mungu kwa kuwa kila
mwanadamu kapangiwa mazingira ya kuondoka duniani.
Alisema kila mmoja katika familia, Serikalini
alikokuwa akifanya kazi na hata watumishi wenzake na marafiki watakuwa
na maswali mengi kuhusu kifo hicho, lakini wamtumaini Mungu.
Mkurugenzi wa mafuta wa Ewura, Godwin Samwel
alisema kutokana na kifo cha mtumishi huyo, ofisi ya Ewura kwa
kushirikiana na vyombo vya dola wanashirikiana kufanya uchunguzi ili
kubaini chanzo cha kifo hicho.
Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alitangaza kuunda jopo hilo litakaloongozwa na mkuu wa
upelelezi wa kanda hiyo, Jaffary Mohamed atakayeshirikiana na wataalamu
wa Maabara Kuu ya Polisi, daktari bingwa wa polisi na maofisa wa
Serikali.
Alisema uchunguzi unafanyika ili kuondoa utata ulioanza kujitokeza kuhusu kifo hicho.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment