KAMATI YA BUNGE YATEMBELEA MAPORI YA AKIBA YA BIHARAMULO, BURIGI, KIMISI (BBK) MKOANI KAGERA


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye akiwaongoza baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kushuhudia maporomoko ya maji ya Rusumo yaliyopo wilayani Ngara ambapo moja ya vyanzo vyake vikubwa vya maji vimeanzia katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi (BBK) wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara mwishoni mwa wiki mkoani wa Kagera.
Wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakipewa maelezo kuhusu mipaka ya Pori la Akiba ya Biharamulo kutoka ziwa Victoria katika kituo cha Katete kutoka kwa Meneja wa Mapori ya Biharamulo, Burigi, Kimisi (BBK), Bw. Bigilamungu Kagoma (wa kwanza kushoto) wakati Kamati hiyo ilipotembelea mapori yaliyopo mkoani Kagera mwishoni mwa wiki
Meneja wa Mapori ya Biharamulo, Burigi, Kimisi (BBK), Bw. Bigilamungu Kagoma (wa kwanza kushoto) akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika ramani mahali ambako Pori la Akiba la Burigi lilipoanzia wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi (BBK), yaliyopo mkoani Kagera hayo mwishoni mwa wiki mkoani Kagera
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye akiwazungumza na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo mara baada ya kujionea Pori la Akiba la Burigi katika wilaya ya Karagwe ambayo ni moja ya kati avyanzo vyake vikubwa vya maji ambavyo vimeanzia katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi (BBK) wakati kamati hiyo ilipofanya ziara mwishoni mwa wiki mkoani wa Kagera.Wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiangalia hema ambalo askari wanyamapori hulitumia kumpumzika wakiwa katika Mapori wakati wanapofanya doria za kuwabaini majangili.Meneja wa mpaka katika Tanzania na Rwanda ambaye pia ni Afisa Mwandamizi wa Forodha, Polycarp Lashau akiwaongoza Wajumbe wa kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kushuhudia maporomoko ya maji ya Rusumo yaliyopo wilayani Ngara ambapo moja ya vyanzo vyake vikubwa vya maji vimeanzia katika Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi (BBK) wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara mwishoni mwa wiki mkoani wa KageraWajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakipewa maelezo kuhusiana na mali mbalimbali za watuhumiwa wa ujangili zikiwemo baiskeli na pikipiki zilizokamatwa katika kituo cha Katete kwenye Pori la Akiba ya Biharamulo kutoka kwa Meneja wa Mapori ya Biharamulo, Burigi, Kimisi (BBK), Bw. Bigilamungu Kagoma (wa kwanza kushoto) wakati Kamati hiyo ilipotembelea mapori yaliyopo mkoani Kagera hayo mwishoni mwa wiki
(PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA-MNRT)

Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo ipo mkoani Kagera imeridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) baada ya kutembelea Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi (BBK) kuangalia kazi za uhifadhi zinazofanywa ambapo wameipongeza TAWA kwa kitendo cha kurudisha hali ya mapori hayo ikiwemo kurejea kwa wanyamapori na uoto wa asili ambapo awali mapori hayo yalikuwa yameharibiwa kwa kasi kutokana na makundi ya mifugo kufanya malisho katika maeneo hayo.

Katika ziara hiyo,iliyoanzia katika Wilaya ya Biharamulo, Wajumbe wa Kamati hiyo waliweza kushuhudia eneo la Pori hilo lilipoanzia katika ziwa Victoria na baadaye kushuhudia Pori la Burigi lililopo katika wilaya za Karagwe na Biharamulo na badaye Pori la Kimisi ambalo lipo katika wilaya mbili za Karagwe na Ngara.

Hata hivyo,Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Nape Nnauye aliridhishwa na masuala ya uendeshaji wa mapori hayo huku akiahidi kuyasaidia mapori hayo kwa kuishauri serikali iweze kuwekeza miundombinu ili kukuza utalii katika ukanda wa ziwa Victoria

‘’Tunatambua kuwa TAWA ni changa haijaanzishwa muda mrefu lakini ndani ya kipindi kifupi imeweza kufanya mambo mazuri katika kulinda Maliasili zetu , Sisi kamati tumeridhisha na utendaji wake’’ alisema Mwenyekiti

Kutokana na utendaji kazi wa Mamlaka hiyo , ‘Mwenyekiti wa Kamati hiyo iliahidi kuwa watalishauri na pamoja na kuishawishi Serikali iweze kuongeza pesa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ili iweze kutimiza wajibu yake.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla aliielezea kamati hiyo kuwa TAWA ipo mbioni kubadili mfumo wake katika mapori hayo ambapo badala ya kuendelea kufanya shughuli za uwindaji wa kitalii pekee wamepanga kuanzisha utalii wa picha ili kufungua fursa za kiuchumi katika ukanda huo.

Aidha, Waziri Kigwangalla alisema kuwa kutokana na Mapori hayo kurejea katika uasilia wake baada kuharibiwa kwa kiasi kikubwa na uvamizi wa mifugo hali iliyopelekea hadi wanyamapori kuhama, Wizara inafanya utafiti ili kuongeza baadhi ya wanyama katika Mapori hayo ili kuweza kuwavutia watalii zaidi kutembelea maeneo hayo.

Aliongeza kuwa, mapori hayo yana sifa ya pekee za kumvutia mtalii yeyote aweze kutembelea katika maeneo hayo huku ukitaja wanyamapori wanne wakubwa kuwa wanapatika katika mapori hayo isipokuwa faru pekee.

Awali kamati hiyo ilipokea taarifa kutoka kwa Wenyeviti wa Kamati za ulinzi na usalama za wilaya ambapo miongoni mwa mambo yaliyojitokeza uvamizi wa maeneo ya mapori ya akiba kwa kuanzisha shughuli za kilimo pamoja na kulisha mifugo ndani ya hifadhi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TAWA, James Wakibara alisema moja ya mikakati ya TAWA ni kubadilisha aina ya biashara kwa kuanza kuchanganya ambapo TAWA itaendesha biashara ya uwindaji wa vitalu pamoja na utalii wa picha katika mapori hayo kwa lengo la kuiongezea serikali mapato

Alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuboresha miundombinu kwa kuanza na barabara ndani ya mapori hayo ili kuweza kuwavutia wawekezaji kujenga hoteli mbalimbali ambazo watalii watazitumia kwa ajili ya kupumzika.

MKUU WA MKOA KAGERA AAGIZA MKANDARASI KUKAMATWA NA KUFIKISHWA OFISINI KWAKE AKIWA NA PINGU MIKONONI BAADA YA KUITIA SERIKALI HASARA

 Baadhi ua Wabunge wa Mkoa wa Kagera Wakifuatilia Mada Katika kikao
 Baadhi ya Waandishi wa Habari Wakitekeleza Majukumu yao Katika Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoani Kagera  
 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Katikati Akiongea na Wajumbe wa Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoani Kagera Hawapo Pichani
Wajumbe Wakifuatilia Mada katika Kikao cha Bodi ya barabara Mkoani Kagera
Na Sylvester Raphael
Mkuu wa Mkoa wa Kagera aagiza  Mkandarasi wa Kampuni ya MECCO aliyeshinda zabuni  ya ujenzi wa barabara zenye thamani ya shilingi bilioni saba na kukataa kusaini mkataba wa  kuanza ujenzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kukamatwa  na kufikishwa  Ofisini kwake akiwa na pingu mikononi ili kutoa sababu za kuitia Serikali hasara.
Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu alitoa agizo hilo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa kwenye kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika Mkoani Kagera Machi 8, 2018 ambapo katika kuwasilisha hoja Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Chief Karumuna  kumuomba Mkuu Mkoa kumchukulia hatua Mkandarasi huyo baada ya kugoma kusaini mkataba wakati alishinda zabuni ya ujenzi wa barabara hizo.
Chief Karumuna alisema kuwa Manispaa ya Bukoba imepata hasara baada ya Mkandarasi kukataa kusaini mkataba wa kuanza ujenzi wa barabara zenye thamani ya shilingi bilioni saba na zabuni kutangazwa tena upya, pia alisistiza kuwa fedha hizo zilitolewa na Benki ya Dunia na utekelezaji wa miradi yake ni wa kipindi maalumu kwa hiyo Mkandarasi huyo amechelewesha muda wa utekelezaji.
Katika kikao hicho ambacho Mkuu wa Mkoa ni Mwenyekiti aliwasistiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini TARURA Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanatengeneza barabara za mipakani ili kuimarsha ulinzi na usalaama wa mkoa na na chi kwa ujmla. Barabara hizo ni Bubale-Missenyi Runch- Kakunyu  Kilomita 32.5, Bubale – Kamwema Kilomita 17.8  Wilayani missenyi na barabara ya Nyabishenge-Nyakanoni-Ibanda Game Reserve kilomita 15 Wilayani Kyerwa.
Vilevile Meneja wa Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA) Mkoa wa Kagera ameagizwa na kikao hicho kusitisha mara moja tozo ya shilingi 80,000/= ya ukaguzi wa magari ya Serikali pale yanapotakiwa kukaguliwa ili yakatengenezwe baada ya wajumbe kuwasilisha sheria kikaoni inayoelekeza kuwa magari ya Serikali yanatakiwa kukaguliwa bure. Hadi Mkuu wa mkoa atakapopata walaka unaoruhusu kutoza magari ya Serikali.
Mkoa wa Kagera unahudumia barabara zenye mtandao wenye jumla ya kilomita 7,505.42 kati ya hizo, kilometa 675.46 ni barabara za lami, kilometa 2,791.56 barabara za changarawe na kilometa 4,038.96 zikiwa in barabara za udongo.
Mkoa wa Kagera kwa mwaka wa fedha 2017/18 uliidhinishiwa shilingi Bilioni 10,710.05 kwajili ya matengenezo ya kazi za barabara na ujenzi wa madaraja. Pia mkoa umeidhinishiwa shilingi bilioni 14,180.937 kwa ajili ya matengenezo ya Barabara Kuu na Barabara za Mkoa kwa mwaka wa fedha 2017/18
Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Mkoani Kagera Mkuu wa Mkoa wa Kagera amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Godfrey Mheluka kumkamata na kumpeleka ofisini kwake kijana anayemtesa mama yake mzazi kwa kutaka kumnyanganya shamba lake na mama huyo ameshinda kijana huyo mara mbili Mahakamani.
“Mtafute kijana huyo na kumleta kwangu nijue ana matatizo gani ili tumsaidie maana atamuua mama yake, hana uchungu na mama yake mzazi. Mama huyoaliwasilisha kilio chake katika mkutano wa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mhe. Lukuvi Wilayani Karagwe lakini kijana huyo bado anaendelea kumsumbua mama yake mzazi.” Alifafanua Mkuu wa Mkoa Kijuu.

NAIBU WAZIRI NDUNGULILE ACHANGISHA ZAIDI YA MILIONI 17 KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI KITUO CHA WAZEE KIILIMA MKOANI KAGERA

 Dk. Faustine Ndungulile Kulia Akiongea na Mzee Mmojawapo Anaishi Katika Kituo cha Wazee Kiilima
 Naibu Waziri wa Afya  Dk. Faustine Ndungulile Akionesha Mfano wa Kufyatua Tofali Ili Nyumba za Watumishi Zijengwe Katika Kituo cha Wazee Kiilima
 Mkuu wa Mkoa Kagera Mhe. Kijuu (Kulia) Akipokea Ahadi ya Vifaa Vilivyohaidiwa na Redcross Wakati wa Harambee Mabati 20, Blanketi 20 na Vyandarua
 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Aliyesimama Kulia Akitoa Taarifa kwa Naibu Waziri wa Afya Dk. Ndungulile
 Naibu Waziri wa Afya  Dk. Faustine Ndungulile Akionesha Mfano wa Kufyatua Tofali Ili Nyumba za Watumishi Zijengwe Katika Kituo cha Wazee Kiilima
Nyumba za Watumishi (Kulia) Zinazotakiwa Kujengwa Upya Kwasababu ya Uchakavu Katika Kituo cha Wazee Kiilima Zikikaguliwa na Waziri Ummy Mwalimu
Na: Sylvester Raphael
Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia  Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndungulile afanikisha  kupatikana kwa zaidi ya  shilingi milioni 17 kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa  Nyumba ya Watumishi katika Kituo cha Wazee Kiilima Kata ya Nyakato Wilayani Bukoba Mkoani Kagera.

Katika Harambee hiyo iliyofanyika Februari 22, 2018 katika Kituo cha Wazee Kiilima Dk. Ndungulile akiwa  Mgeni Rasmi alichangisha fedha taslimu milioni 7,000,000/= na kiasi cha shilingi milioni 11 zikiwa ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali pamoja ahadi za vifaa kama magodoro, saruji,  baiskeli za wazee na mabati.

Katika hotuba yake kwa wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria harambee hiyo Naibu Waziri Dk. Ndungulile aliwasisitiza wananchi kuwa na moyo wa kujitolea kuchangia kituo hicho ili watumishi wanaowatunza wazee wapate mazingira mazuri ya kuishi baada ya kufanya kazi yao ya kuwahudumia wazee hao.

“Serikali itaendelea kuwaunga  mkono wananchi kwa kuleta fedha katika kituo hiki ili kikamilike ujenzi wake na Wazee wetu  waweze kuhudumiwa na watumishi  ambao watawaza ni wapi pa kuishi au kukaa salama mara baada ya kufanya kazi yao ya kuwahudumia Wazee wetu,” Alisisitiza Dk. Ndungulile.
Kituo cha Kutunza Wazee Kiilima ni kituo cha Serikali kilichopo chini ya Wizara ya  Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia  Wazee na Watoto.  Kituo Hicho kilijengwa upya na Serikali baada ya kuathiriwa na Tetemeko la Ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 Mkoani Kagera.

Majengo yaliyojengwa upya na Serikali ni pamoja na Mabweni mawili ya Wanaume na Wanawake, Jiko, stoo ya kutunzia chakula, Sehemu ya kulia chakula, sehemu ya kupumzikia wazee,  vyoo viwili vya wanawake na wanaume. Changamoto iliyokuwa imebaki ni nyumba za watumishi ambazo kwa sasa zina hali mbaya ya uchakavu na hazistahili tena kuishi watu.

Fedha zilizopatikana zinatarajiwa kujenga nyumba mbili za watumishi (Two in One) ili kutatua changamoto ya watumishi wanaoishi na kufanya kazi ya kuwahudumia wazee ili wapate mahali salama pa kuishi na kutimiza wajibu wao kikamilifu bila kuwa na changamoto za sehemu za kuishi.
Katika Hatua nyingine Naibu Waziri Dk. Ndungulile alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu kwa juhudi zake za kuipatia Bohari ya Dawa (MSD)  kiwanja cha kujenga Bohari ya dawa katika Manispaa ya Bukoba na Mkoani Kagera ili kurahisisha upatikanaji wa dawa zote hapa Kagera.

Pia Dk. Ndungulile alimuomba Mkuu wa Mkoa kuhamasisha wananchi kuitikia wito wa kuwapeleka watoto wa kike miaka 4 hadi 9 kwenda kwenye vituo vitakavyokuwa vimepangwa kupata chanjo ya kansa ya shingo na uzazi kwani imeonekana kuwa kuna ongezeko kubwa la Kansa ya Shingo na uzazi katika mkoa wa Kagera.

Akimshukuru Naibu Waziri kwa kuamua kufanya ziara ya kukagua shughuli za afya Mkoani Kagera Mkuu wa Mkoa Kijuu aliomba Wizara ya Afya kuangalia upya tatizo la ugonjwa wa Malaria katika Mkoa wa Kagera kwani pamoja na juhudi zote zinazofanyika laikini kiwango cha ugonjwa huo kinazidi kupanda ambapo Naibu Waziri Dk. Ndungulile alisema tayari Wizara imeliona hilo na linafanyiwa kazi.

Naibu Waziri Dk. Ndungulile akiwa Mkoani hapa katika ziara yake ya siku mbili alivitembelea pia vituo vya Afya Kabyaile Wilayani Missenyi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Kituo cha Afya Kaigara na Kituo cha Afya Kimeya Wilayani Muleba ili kukagua huduma za Afya zinavyotolewa kwa wananchi na kuongea na watumishi katika maeneo hayo.

MAAFISA HABARI NA TEHAMA WANOLEWA KUZIBORESHA TOVUTI ZA MIKOA NA HALMASAHURI ILI KUWA KITOVU CHA HABARI KWA WANANCHIMaafisa Habari na Tehama wakiwa katika mafunzo juu ya namna bora ya uandishi wa habari za Tovuti.

Na: Sylvester Raphael
Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Mradi wa kuboresha Mifumo ya Serikali PS3 waendesha mafunzo ya siku nne juu ya namna bora ya uandishi wa habari za Tovuti za Serikali kwa Maafisa Habari na Maafisa Tehama wa Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Bara.

Kutokana na umuhimu wa Tovuti za Serikali hasa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini kuwa chanzo kikuu cha habari kwa wananchi Serikali kwa kushirikiana na Mradi wa Maboresho ya Mifumo ya Serikali PS3 waliona kuna umuhimu wa kuendesha mafunzo juu ya uandishi bora wa habari katika Tovuti za Mikoa na Halmashauri  ili wananchi wapate habari muhimu na zenye uhakika juu ya maendeleo yao.

Kwakuwa siyo Mikoa yote na Halmashauri zote nchini zina Maafisa Habari na kazi za Habari zinafanywa na baadhi ya watu kama Maafisa Tehama, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mradi wa kuboresha Mifumo ya Serikali PS3 wameona kuna umuhimu wa Maafisa hao kupitishwa katika mafunzo ya namna bora ya uandishi wa habari za Tovuti kwa wananchi ili kuwa na uelewa wa pamoja na aina moja ya uandishi (House Style)

Katika Mafunzo hayo mada mbalimbali zihusuzo Uandishi wa Habari zinawasilishwa na wataalamu waliobobea katika mambo ya habari na uandishi wa habari pia ambapo mada hizo ni pamoja na Malengo ya Mwongoz wa  Tovuti, Sheria na Maadili ya Habari, Upigaji wa Picha za Kidijitali, Mbinu za Mahojiano, Uandishi wa Aya, Habari katika mfumo wa 5Ws + H (Piramidi iliyogeuka).

Mafunzo ya namna bora ya uandishi wa habari za Tovuti za Serikali yanaendeshwa katika makundi ya mikoa mbalimbali ambapo mikoa ya Geita, Tabora Kigoma na Kagera mafunzo hayo yanafanyika katika Mkoa wa Kagera Bukoba Hotel Manispaa ya Bukoba aidha, mafunzo hayo yalianza Februari 19 na yanatarajia kukamilika Februari 22, 2018.

Matarajio ya Serikali baada ya mafunzo hayo ni kuona Tovuti za Serikali zinakuwa kitovu cha habari kwa wananchi na si ilimradi habari tu bali habari zenye weledi, ukweli, uhakika na kuisemea Serikali inafanya nini katika kuwaletea wananchi maendeleo. Pia katika Tovuti hizo kuwa na taarifa muhimu mbalimbali zinazohusu taasisi husika mfano Mkoa au Halmashauri husika.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa