RC ATOA SIKU 21 KWA TASAF III

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MKUU wa Mkoa wa Kagera, John Mongella ametoa siku 21 kwa watendaji, waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na maofisa maendeleo ya jamii kwenda kila kitongoji na kuitisha mikutano upya ya kuwatambua walengwa wa mpango wa Tasaf III walioingizwa mwanzoni kama ni kaya maskini kweli.

Mongella alisema ameamua kutoa agizo hilo jana baada ya kufanya ziara katika wilaya nne za mkoa huo za Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara na kutembelea walengwa wa mradi huo kuona maendeleo kutokana na fedha hizo na kuambulia malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu utaratibu uliotumika kutambua kaya maskini.

Wananchi hao walidai kuwa utaratibu haukuwa wazi na ulikiukwa. Pia alisema baadhi ya wananchi walisema baadhi ya walioingizwa kwenye mpango ni watu wenye uwezo, wengine wake za viongozi na wahamiaji haramu huku baadhi ya watu wakionesha kutoelewa vizuri malengo ya mradi huo.

Alisema pia ni vyema kutoa elimu vijijini juu ya lengo kuu la mpango wa Tasaf III kwani katika maelezo ya baadhi ya wananchi hasa walengwa wameonesha kutoelewa vizuri huku baadhi yao wakipata fedha na kuishia kwenye ulevi wa pombe bila kuanzisha mradi utakaowasaidia kujiondoa katika umaskini wa kipato pindi mradi utakapoisha.

Alisema pia wapo baadhi ya wananchi wenye uwezo ambao 
wanalalamika kuona wamebaguliwa kwa kutoingizwa kwenye mradi huo, jambo linaloonesha wananchi hawajapata elimu ya kutosha kuhusu walengwa wa mradi huo.
“Kwanza mnapaswa kabla ya kutoa fedha wakati wa zoezi la uhaulishaji, kutoa elimu kwa muda wa saa mbili na baada ya zoezi kuisha nendeni vijijini, kazi yenu sio kugawa fedha tu mkimaliza mnalala na kusubiri mpaka fedha nyingine iletwe mkagawe.
“Sasa nawaagiza baada ya wiki moja toka zoezi kumalizika nendeni vijijini mkawaelimisheni waanzishe miradi midogo midogo itakayo wasaidia baada ya mradi kuisha kwani baada ya miaka mitatu muda wao utaisha wataingizwa walengwa wengine wapya,” aliagiza mkuu wa mkoa.

Aidha, ameagiza watendaji wa Tasaf, watendaji wa kata na wakurugenzi wote wa Halmashauri za wilaya hasa Kyerwa na Karagwe ambako kumeonekana kuna ubadhirifu wa fedha, kukamata watuhumiwa na kuwahoji na endapo watabainika na tuhuma wafikishwe mahakamani.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

MGANGA MKUU ASAFISHWA KASHFA YA FEDHA BUKOBA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela (wa pili kutoka kushoto) akishuhudia mgao wa fedha kwa kaya masikini mkoani humo.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Murshid Ngeze amesema aliyekuwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo (DMO), Dk Hamza Mgula hahusiki na tuhuma za kubadili matumizi ya fedha za Halmashauri hiyo zilizosababisha watumishi saba kusimamishwa kazi.
Januari 28, mwaka huu, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba lilipendekeza kusimamishwa kwa watumishi saba kwa lengo la kupisha uchunguzi kutokana na kubadili matumizi ya fedha Sh milioni 851 za miradi ya maendeleo na ukosefu wa baadhi ya nyaraka za uhamisho wa fedha hizo.
Awali, Mwenyekiti huyo alilieleza gazeti hili kwa simu kuwa Dk Mgula ambaye sasa yuko Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa watumishi hao ambao wamesimamishwa kazi, lakini baadaye alieleza kuwa DMO huyo hahusiki, kwani Baraza hilo liliamua kuwasimamisha watumishi hao saba.
“Katika taarifa zilizotolewa mwanzo na kuandikwa katika vyombo mbalimbali zilimhusisha aliyekuwa DMO wa Halmashauri hiyo kwa kipindi cha nyuma ambaye sasa ni Mganga wa Manispaa ya Bukoba Dk Hamza Mgula, mtumishi huyo hahusiki na tuhuma hizo na si mtumishi wa Halmashauri hii,” alieleza Mwenyekiti Ngeze katika barua ambayo aliviandikia vyombo vya habari kufafanua suala hilo.
Kwa mujibu wa Ngeze, waliosimamishwa ni Mweka Hazina wa Wilaya, Jonathan Katunzi, Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya, Selialis Mutalemwa, Mhandisi wa Wilaya, Robert Massoro na Fundi Sanifu Mkuu wa Wilaya, Desu Bizibu. Aliwataja wengine kuwa ni Ofisa Elimu Sekondari Wilaya, Lucas Mzungu, Ofisa Mipango wa Wilaya, Mustapha Sabuni na Mganga wa Mifugo wa Wilaya, Dk Kisanga Makigo.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema Mkurugenzi Mtendaji (DED) aliyekuwepo Gladys Ndyamvunye ambaye amehamishiwa mkoani Pwani akitakiwa kurudishwa kujibu tuhuma zinazomkabili.
Alisema baraza hilo limewasimamisha kazi watumishi saba wa Idara mbalimbali kutokana na mapendekezo ya timu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella ili kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh milioni 851 zilizokuwa zimepangwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi hao, Baraza hilo la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba limemtaka Katibu Mkuu Tamisemi kumchukulia hatua za kinidhamu Ndyamvunye kwa kosa la kutosimamia ipasavyo fedha hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi chini ya uenyekiti wa Mhandisi Wambura Sabora, fedha zinazodaiwa kufujwa ama kubadilisha matumizi ni Sh milioni 168 za Mfuko wa Jimbo, Sh milioni 200 kama ombi maalum la ujenzi wa Daraja la Kyamabale, Sh milioni 176 za Mfuko wa Barabara na Sh milioni 307 zilizotolewa na wafadhili katika Mfuko wa Afya.
CHANZO : HABARI LEO.

BENKI YASUASUA MALIPO YA KAYA MASIKINI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WALENGWA wa Mpango wa Uhawilishaji wa fedha za ruzuku kwa kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) III wa kunusuru kaya masikini wilayani Kyerwa, wamelalamikia ucheleweshwaji wa fedha kutoka benki wakati wa malipo ambao umeonekana kuwa kero na kuwakatisha tamaa wahusika hao.
Walitoa malalamiko hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella aliyefanya ziara ya siku moja kwa lengo la kupata maelezo juu ya maendeleo ya mpango na mafanikio yaliyofikiwa na kutafuta ufumbuzi juu ya changamoto zinazokabili mpango huo ili malengo ya Serikali ya kupunguza umasikini yafikiwe kwa asilimia 100.
Mkazi wa kijiji cha Mulongo, Adelina Danstan alisema mwanzoni wakati wanaingizwa katika mpango huo walielezwa kuwa dirisha la malipo linafunguliwa na kufungwa ndani ya siku nne, lakini kwa Wilaya ya Kyerwa ni tofauti ambapo hufunguliwa siku nne lakini malipo hufanyika siku mbili au moja usiku na mchana.
“Wenzetu wakianza kupata malipo sisi hushinda vituoni siku mbili jua kali au mvua ikiwa halali yetu tukisubiri malipo ambapo tunalazimika kuwauliza wahusika wa Tasaf ambao tunaelezwa kuwa benki ndiyo inayokwamisha na kusababisha hali hiyo hata wao hawapendi hali hiyo itokee,” alieleza Dastan.
Mkazi wa kijiji cha Rwabikagati, Catherine Binomutonzi alisema kutokana na adha hiyo inayoelezwa kuwa inasababishwa na benki kutotoa kipaumbele kwa wilaya hiyo husababisha walengwa kuhudhuria vituoni siku mbili na kutoka patupu; na siku ya tatu jioni ndipo fedha zinapoletwa na kuanza kugawiwa mpaka usiku.
“Hali hii inakatisha tamaa na kuona kama tunadharauliwa kwa kuwa ni masikini, kwa hiyo tunakuomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati na kuona ni sababu zipi zinakwamisha. Kumbuka ucheleweshwaji huo unasababisha msongamano, wazee hapa wanashindwa kubaki mpaka usiku wakihofia maisha yao kuwa hatarini kwani wanaweza kukabwa na vibaka usiku kwa hiyo wanalazimika kuondoka na kuiacha fedha,” alisema Binomutonzi.
CHANZO ; HABARI LEO.

MAUAJI YA DIWANI MULEMA YACHOCHEA VURUGU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Kimwani, Muleba mkoani Kagera, wamevamia, kuharibu mali na kuchoma moto nyumba nane katika tukio linalohusishwa na ulipaji kisasi na chuki za kisiasa.
 
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya kutokea mauaji ya diwani wa kata hiyo. Sylvester Muliga (55) kupitia CUF.
 
Mwenyekiti wa kijiji Kyota lilipotokea tukio hilo, Daud Kiluma, alisema wananchi hao walivamia nyumbani kwa aliyekuwa mgombea udiwani wa CCM, Alex Rwakayonza, wakimtuhumu kuhusika na mauaji hayo na kuharibu mashine ya kusaga nafaka pamoja na mashine nyingine ya jirani.
 
Kiluma alisema wananchi hao walivamia nyumba hiyo na kuanza kubomoa milango na kuingia ndani kisha kuchoma moto mali zilizokuwamo na hatimaye kufyeka migomba na kuvunja vioo vya gari lake.
 
Alisema baada ya hapo, wananchi hao walikwenda kwa washirika wa karibu wa Rwakayonza, akiwamo mtoto wake, na kuchoma moto nyumba nane za watu hao.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi limeimarisha ulinzi katika eneo hilo.
 
Aidha, Kamanda Ollomi alisema katika tukio la mauaji ya diwani huyo, hadi jana watu watatu walikuwa wamekamatwa, baada ya mmoja kukamatwa jana. Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni Adelard Anthony (42) na Shilanga Gunzari (22)
Diwani Muliga alivamiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia juzi na  kukatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Ollomi alisema diwani huyo, wakati akiangalia taarifa ya habari saa mbili usiku nyumbani kwake, watu wasiofahamika waliingia wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na kuanza kumshambulia.
 
Majirani walipopata taarifa za kuvamiwa kwa diwani huyo, walifika nyumbani kwake kwa lengo la kumpatia msaada lakini walikuta tayari amejeruhiwa vibaya, hivyo kumuwahisha katika hospitali ya Kagondo  kwa ajili ya matibabu. 
 
Kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa ameyapata, ilipofika saa saba usiku, alifariki dunia wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake.
CHANZO: NIPASHE
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa