Home » » RC ATOA SIKU 21 KWA TASAF III

RC ATOA SIKU 21 KWA TASAF III

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MKUU wa Mkoa wa Kagera, John Mongella ametoa siku 21 kwa watendaji, waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na maofisa maendeleo ya jamii kwenda kila kitongoji na kuitisha mikutano upya ya kuwatambua walengwa wa mpango wa Tasaf III walioingizwa mwanzoni kama ni kaya maskini kweli.

Mongella alisema ameamua kutoa agizo hilo jana baada ya kufanya ziara katika wilaya nne za mkoa huo za Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara na kutembelea walengwa wa mradi huo kuona maendeleo kutokana na fedha hizo na kuambulia malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu utaratibu uliotumika kutambua kaya maskini.

Wananchi hao walidai kuwa utaratibu haukuwa wazi na ulikiukwa. Pia alisema baadhi ya wananchi walisema baadhi ya walioingizwa kwenye mpango ni watu wenye uwezo, wengine wake za viongozi na wahamiaji haramu huku baadhi ya watu wakionesha kutoelewa vizuri malengo ya mradi huo.

Alisema pia ni vyema kutoa elimu vijijini juu ya lengo kuu la mpango wa Tasaf III kwani katika maelezo ya baadhi ya wananchi hasa walengwa wameonesha kutoelewa vizuri huku baadhi yao wakipata fedha na kuishia kwenye ulevi wa pombe bila kuanzisha mradi utakaowasaidia kujiondoa katika umaskini wa kipato pindi mradi utakapoisha.

Alisema pia wapo baadhi ya wananchi wenye uwezo ambao 
wanalalamika kuona wamebaguliwa kwa kutoingizwa kwenye mradi huo, jambo linaloonesha wananchi hawajapata elimu ya kutosha kuhusu walengwa wa mradi huo.
“Kwanza mnapaswa kabla ya kutoa fedha wakati wa zoezi la uhaulishaji, kutoa elimu kwa muda wa saa mbili na baada ya zoezi kuisha nendeni vijijini, kazi yenu sio kugawa fedha tu mkimaliza mnalala na kusubiri mpaka fedha nyingine iletwe mkagawe.
“Sasa nawaagiza baada ya wiki moja toka zoezi kumalizika nendeni vijijini mkawaelimisheni waanzishe miradi midogo midogo itakayo wasaidia baada ya mradi kuisha kwani baada ya miaka mitatu muda wao utaisha wataingizwa walengwa wengine wapya,” aliagiza mkuu wa mkoa.

Aidha, ameagiza watendaji wa Tasaf, watendaji wa kata na wakurugenzi wote wa Halmashauri za wilaya hasa Kyerwa na Karagwe ambako kumeonekana kuna ubadhirifu wa fedha, kukamata watuhumiwa na kuwahoji na endapo watabainika na tuhuma wafikishwe mahakamani.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa