Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Murshid Ngeze amesema
aliyekuwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo (DMO), Dk Hamza
Mgula hahusiki na tuhuma za kubadili matumizi ya fedha za Halmashauri
hiyo zilizosababisha watumishi saba kusimamishwa kazi.
Januari 28, mwaka huu, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya
Bukoba lilipendekeza kusimamishwa kwa watumishi saba kwa lengo la
kupisha uchunguzi kutokana na kubadili matumizi ya fedha Sh milioni 851
za miradi ya maendeleo na ukosefu wa baadhi ya nyaraka za uhamisho wa
fedha hizo.
Awali, Mwenyekiti huyo alilieleza gazeti hili kwa simu kuwa Dk Mgula
ambaye sasa yuko Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa watumishi hao ambao
wamesimamishwa kazi, lakini baadaye alieleza kuwa DMO huyo hahusiki,
kwani Baraza hilo liliamua kuwasimamisha watumishi hao saba.
“Katika taarifa zilizotolewa mwanzo na kuandikwa katika vyombo
mbalimbali zilimhusisha aliyekuwa DMO wa Halmashauri hiyo kwa kipindi
cha nyuma ambaye sasa ni Mganga wa Manispaa ya Bukoba Dk Hamza Mgula,
mtumishi huyo hahusiki na tuhuma hizo na si mtumishi wa Halmashauri
hii,” alieleza Mwenyekiti Ngeze katika barua ambayo aliviandikia vyombo
vya habari kufafanua suala hilo.
Kwa mujibu wa Ngeze, waliosimamishwa ni Mweka Hazina wa Wilaya,
Jonathan Katunzi, Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya, Selialis Mutalemwa,
Mhandisi wa Wilaya, Robert Massoro na Fundi Sanifu Mkuu wa Wilaya, Desu
Bizibu. Aliwataja wengine kuwa ni Ofisa Elimu Sekondari Wilaya, Lucas
Mzungu, Ofisa Mipango wa Wilaya, Mustapha Sabuni na Mganga wa Mifugo wa
Wilaya, Dk Kisanga Makigo.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema Mkurugenzi Mtendaji (DED) aliyekuwepo
Gladys Ndyamvunye ambaye amehamishiwa mkoani Pwani akitakiwa kurudishwa
kujibu tuhuma zinazomkabili.
Alisema baraza hilo limewasimamisha kazi watumishi saba wa Idara
mbalimbali kutokana na mapendekezo ya timu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, John Mongella ili kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za ubadhirifu
wa zaidi ya Sh milioni 851 zilizokuwa zimepangwa katika utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi hao, Baraza hilo
la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba limemtaka Katibu Mkuu
Tamisemi kumchukulia hatua za kinidhamu Ndyamvunye kwa kosa la
kutosimamia ipasavyo fedha hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi chini ya uenyekiti wa Mhandisi
Wambura Sabora, fedha zinazodaiwa kufujwa ama kubadilisha matumizi ni Sh
milioni 168 za Mfuko wa Jimbo, Sh milioni 200 kama ombi maalum la
ujenzi wa Daraja la Kyamabale, Sh milioni 176 za Mfuko wa Barabara na Sh
milioni 307 zilizotolewa na wafadhili katika Mfuko wa Afya.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment