Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara Atembelea Shamba la Kahawa na Migomba ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana kutoka SACCOS ya Ibwera Bukoba


 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Dk. Fenella Mukangara (kushoto) akiangalia kahawa katika shamba darasa
inayolimwa na Ibrahim Mulokozi (kulia) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ibwera
wilayani Bukoba aliyenufaika na mkopo wa shilingi laki nne kutoka mfuko wa
maendeleo ya vijana. Waziri Dk. Mukangara alilitembelea shamba hilo la kahawa
na migomba jana ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana kutoka SACCOS ya
Ibwera zimewanufaishaje kimaisha.
 Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kushoto)
akimuangalia samaki mwenye umri wa miezi mitatu anayefugwa katika bwawa la
Kikundi cha Msifuni kilichopo kijiji cha Kemondo wilayani Bukoba ambacho
kilipata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana. Waziri Dk. Mukangara
alilitembelea bwawa hilo jana ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana
kupitia mfuko wa Halmashauri nimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kushoto) akipokea
taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo wilayani Bukoba kutoka kwa Benedicta Peter
ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo ilipata mkopo wa shilingi milioni tano
kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na kuvikopesha vikundi mbalimbali vya
maendeleo vya vijana.

----

Na Anna Nkinda –Maelezo, Kagera

Serikali
imeombwa kuongeza kiasi cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko
wa maendeleo wa vijana na Halmashauri za wilaya kwani kiwango
kinachotolewa kwa sasa cha shilingi milioni tano kwa vyama vya Kuweka
Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo ukilinganisha na mahitaji ya mkopo
huo.



Ombi hilo limetolewa jana na baadhi ya vijana
waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na halmashauri ya wilaya
ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.



Vijana
hao walisema kuwa fedha za mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua
kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya
biashara zao, kulipa karo za shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha
tofauti na ilvyokuwa awali kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za
ujasiriamali. 



Kwa
upande wake mkazi wa kijiji cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata
mkopo wa shilingi laki nne kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa
ameweza kununua matandazo na kulipa wasaidizi wanaohudumia shamba lake la migimba na kahawa ambalo ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni na Nyakibimbili na kwenda kujifunza na kuchukua miche ya migomba.



Alisema
kuwa anakabiliwa na changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza
shughuli za kilimo, kutoka na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba,
bei ya miche ya kahawa kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche
mmoja, kuendelea kutumia jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika
hasa soko la ndizi na magonjwa ya migomba.



Naye katibu wa kikundi cha Msifuni Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na laki tano kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba alisema kuwa kikundi chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa samaki na walianza na bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha kuwa kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.



“Changamoto
zinazotukabili ni kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na
elimu ya kuendesha na kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma
kwa mradi wetu wa samaki ikiwa ni pamoja na kuibiwa na kuharibiwa kwa mabwawa hasa nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za maendeleo”, allisema Joel. 



Kwa
upande wake waziri Dk. Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho
kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga katika vikundi vya maendeleo jambo
ambalo litawafanya waweze kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana na halmashauri ya wilaya na hivyo kuweza kujishughulisha na kazi za upandaji wa miti, kilimo cha samaki na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki.



Dk. Mukangara alisema, “Vijana ni lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya uvivu, kufanya
kazi si lazima uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa
Ibwera kunahali ya hewa nzuri na milima mingi haina miti mnaweza kuwa na
mradi wa kupanda miti na kufuga nyuki ambao watawapatia asali na
mkiiuza mtapata fedha nahivyo kujikwamua kiuchumi”. 



Kwa
upande wa mafunzo ya ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa
wizara yake inavituo vya kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika
ambao ni vijana watakuwa tayari kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi, stadi za maisha watayapata na yatawasaidia katika maisha yao.



Waziri Dk. Mukangara alikuwa mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na vikundi vya vijana vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha hizo zimewasaidiaje vijana
kujikwamua kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba alilitembelea shamba la
mfano la kahawa na migomba, kikundi cha burudani cha Rugazi na shamba la samaki la kikundi cha Msifuni.

WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO DK MUKANGARA AMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA KAGERA




Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara (kushoto) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu Fabian Massawe mara baada ya kumtembelea ofisini kwake jana mjini Bukoba. Waziri Dk. Mukangara yupo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe alipomtembelea ofisini kwake jana mjini Bukoba. Waziri Dk. Mukangara yupo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kushoto ) akiongea na viongozi wa mkoa wa Kagera (hawapo pichani) jana mjini Bukoba jinsi Serikali inavyoangalia uwezekano wa kuongeza mkopo kwa SACCOS zinazolenga shughuli za maendeleo ya vijana kutoka shilingi milioni tano hadi kumi kutokana na mahitaji ya fedha hizo kuwa makubwa. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana James Kajugusi.(Picha na Anna Nkinda – Maelezo)

TAMASHA LA SHANGWE LAFANA MJINI BUKOBA




 Mwimbaji wa
Nyimbo za Injili,Rose Muhando akitumbuiza kwenye Tamasha la shangwe
Kagera katika uwanja wa Kaibata mjini Bukoba mwishoni mwa wiki,tamasha
hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Beula Communication kwa ajili ya
kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika mkoa wa kagera.




 Mwimbaji wa
Nyimbo za Injili,Enock Jonas(Zunguka) akitumbuiza kwenye Tamasha la
shangwe Kagera katika uwanja wa Kaibata mjini Bukoba mwishoni mwa
wiki,tamasha hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Beula Communication kwa
ajili ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika mkoa
wa kagera.




 Masista wa
Kituo cha Tumaini Children’s Centre, Sr.Adventina Kyamanywa (kushoto) na
Sr.Esther  wakijadiliana jambo  wakati wa tamasha la shangwe Kagera
katika viwanja vya Kaitaba mjini Bukoba.






Mkurugenzi wa
Beula Communication, Melkzedek  Mutayabarwa akizungumza kwenye Tamasha
laShangwe Kagera,ambapo kampuni hiyo ndio iliyoandaa tamasha hilo.  




Mkuu wa
Wilaya  Bukoba,Zippora Pangani akihutubia kwenye  Tamasha la shangwe
Kagera katika uwanja wa Kaibata mjini Bukoba mwishoni mwa wiki,tamasha
hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Beula Communication kwa ajili ya
kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika mkoa wa kagera.




 Waimbaji wa kwaya ya Vijana ya KKKT Usharika wa kanisa Kuu la Mjini Bukoba wakitumbuiza kwenya tamasha la Shangwe Kagera.




Rose Muhando akiwaburudisha viongozi walioudhuria Tamasha la Shangwe Kagera katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

*TAMKO - STATEMENT YA ASKOFU METHOD KILAINI DHIDI YA GAZETI LA MWANANCHI LEO 16 NOV





Askofu Method Kilaini

TAMKO – STATEMENT

Kwa masikitiko makubwa nimesoma katika gazeti la Mwananchi kwamba nimeiponda safu ya uongozi na sekretariati ya CCM. Mimi sijaongea na gazeti lolote juu ya uongozi wa CCM na wala sina nia au sababu ya kuuponda uongozi huo. Ni vibaya kwa gazeti lo lote lile kutumia jina la mtu kwa kueneza maoni yake. Kama ni waugwana natumaini watasahihisha waliyoyaandika. Nasikitika sana kwa walikwazwa na hilo. Askofu Kilaini

Askofu Method Kilaini
Bukoba Catholic Diocese


Boti yazama,saba wafa

Watu saba wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Victoria eneo la hifadhi ya kisiwa cha Rubondo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Ajali hiyo ilitokea Novemba 10, mwaka huu majira ya usiku wakati watu hao wakiwa katika shughuli za uvuvi jirani na eneo la hifadhi ya kisiwa cha Rubondo.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Diwani wa Kata ya Ikuza, Fortunatus Wazia, alisema kuwa watu hao walikuwa ni wavuvi kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Wilaya ya Muleba.

Wazia alifafanua kuwa wavuvi hao walikumbwa na mkasa huo baada ya chombo walichokuwa wakisafiria kuzama.

Kwa mujibu wa diwani huyo, wavuvi hao walikwenda kuvua samaki kwenye kisiwa cha Rubondo kinyume cha sheria kwa kuwa ni eneo la hifadhi na boti hiyo ilizama kutokana na kutokuwa na ubora.

Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo, ilianza kuvuja maji wakati wakirejea kisiwani Ikuza kabla ya kuzama.

Kwa mujibu wa Wazia, watu hao waliondoka katika kisiwa cha Ikuza kwenda kwenye hifadhi ya Rubondo Novemba 8, mwaka huu na walipita njia za panya wakikwepa walinzi wa hifadhi wasiwakamate kwa kuwa walikuwa wanafanya ujangili.

Diwani huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Baruya Masala, mkazi wa Muganza wilayani Chato; Alex Mwita, mkazi wa Tarime; Kipara Kasukari, mkazi wa Kata ya Mushabago wilayani Muleba na mwingine amejulikana kwa jina moja la Niko, mkazi wa Sengerema.

Wengine ni Obadia Yohana, mkazi wa Muganza; Juma Kengere, mkazi wa Itale Chato; na mwinge aliyetambuliwa kwa jina moja la Robert, mwenyeji wa Wilaya ya Biharamulo.

Wazia alisema kuwa baadhi ya miili ya marehemu hao ilitambuliwa na ndugu na jamaa zao na tayari ilimeshachukuliwa kwa ajili ya mazishi.

Hata hivyo, alisema maiti watatu hawakutambuliwa na ndugu mapema na kulazimika kuzikwa katika eneo la ufukweni mwa Ziwa Victoria katika kisiwa cha Ikuza wilayani Muleba.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Philip Kalangi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na wavuvi hao kufariki dunia.

Kamanda Kalangi aliongeza kuwa Jeshi la Polisi mkoani Kagera linaendelea kuchunguza kwa lengo la kubaini chanzo cha ajali hiyo.

WADAU WA ELIMU CHATO WALALAMIKIA ELIMU YA AWALI



Watoto wa awali wa shule ya msingi Kalema.
 Watoto wa awali wa shue ya msingi Chato.
-
Na Daniel Limbe,Chato

LICHA ya serikali kuhamasisha
uanzishwaji wa elimu ya awali katika shule zote za msingi hapa nchini
kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kimaarifa watoto
ambao hawajafikia umri wa kuanza elimu ya msingi,hatua hiyo imeonekana
kulalamikiwa sana na baadhi ya wadau wa elimu katika wilaya ya chato
mkoani geita kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu mbalimbali ya
kufundishia.

Wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi Kalema,Kitela na Chato
wamesema upatikanaji wa elimu ya awali kwa
watoto ni changamoto kubwa kwa serikali kutokana na ukosefu mkubwa wa
vitabu vya kufundishia,vifaa vya kujifunzia na uhaba wa walimu.

Kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule ya
msingi Chato Mwita Chacha shule yake inawanafunzi wa awali 300 na
kwamba watoto hao wanamwalimu mmoja na kwamba
hakuna madawati ya kukalia wala vifaa vya kujifunzia kwa vitendo hali
inayosababisha watoto wengi kushindwa kupata elimu iliyokusudiwa.

Amesema kitendo cha mwalimu mmoja
kufundisha watoto 300 hakiendani na mpango wa kitaifa wa utoaji elimu
ambao unamtaka mwalimu mmoja kufundisha watoto
40 huku akiiomba serikali kuimalisha miundombinu ya kufundishia
itakayosaidia kuboresha elimu kwa watoto wa shule za awali.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule
ya msingi Kalema Tano Bara amesema ili elimu ya awali iweze kupatikana
kwa ufanisi kuna haja kubwa kwa serikali
kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua vitendea kazi vya
kufundishia na kufundishiwa hatua itakayorahisisha upatikanaji wa elimu
bora kwa watoto wa awali ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.

Aidha uchunguzi wa Mwandishi wa habari
hizi umebaini aslimia 95 ya shule za awali wilayani chato hakuna vitabu
vya kufundishia watoto badala yake
walimu wa madarasa hayo hulazimika kutumia mihutasari inayotoa miongozo
ya kutolea elimu hiyo huku madawati na vifaa vingine vya kujifunzia
vikionekana kitendawili.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya watoto
wa awali imeonekana ni vigumu kwao kujifunza kwa ufasaha kutokana na
baadhi yao kukaa chini na wengine kukalia
mawe wakati wa kujifunza hivyo kusabisha watoto kuwa na miandiko
isiyofaa.

Alipotakiwa kujibu malalamiko hayo
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato Shaban Ntarambe alidai kuwa
yeye siyo msemaji licha ya kudai kuwa
serikali inayafahamu mapungufu yaliyopo na kwamba taratibu bado
zinafanyika ili kutatua hali hiyo.

Aidha amedai kuwa mwongozo alionao
unamuelekeza kusimamia uandikishwaji wa watoto wa shule za awali kila
kijiji na kwamba hatua zingine zitafuatwa
kulingana na mpango wa serikali.

BUKOBA HII!

















Picha na mtaa kwa mtaa blog

WAZIRI MKUU PINDA AHUDHURIA KUZIKWA KWA MARA YA PILI KWA KARDINALI RUGAMBWA


Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akiweka shada la maua kwenye kaburi la hayati
Mwadhama Laurian  Kardinali Rugambwa kwenye kanisa kuu katoliki la
Bukoba Oktoba 17, 2012.  

Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Mazishi Ya Kardinali Rugambwa, katika picha



Picha kutoka Bukobawadaublog

MAANDALIZI MAZISHI YA KARDINAL RUGAMBWA YAMEKAMILIKA

Na Renatha Kipaka, Bukoba
KANISA Katoliki Jimbo la Bukoba,liko mbioni kukamilisha kuhamisha masalia ya mwili wa marehemu Muadhama Kardinali Laurian Rugambwa. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba jana,Askofu Msaidizi Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini alisema shughuli za maandalizi ya kuhamisha masalia ya mwili wa marehemu Kardinali Rugambwa inaendelea vizuri.

Alisema mbali ya kukamilika kwa maandalizi hayo, ujenzi wa kanisa jipya uko hatua za mwisho kabisa kumalizika.

Alisema shughuli ya kuhamisha masalia ya mwili wa marehemu Kardinali Rugambwa, itafanyika Jumamosi ya wiki hii kutoka Kanisa la Mama Bikira Maria la Kashozi lililoko nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba.

Alisema sherehe hizo, zitaambana na sherehe zingine mbili ambazo ni maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa marehemu Rugambwa na sherehe ya kutabaruku kanisa la Kiaskofu la Jimbo ambayo itafanyika Jumapili.

Alisema akiwa Askofu wa Jimbo la Bukoba,marehemu Rugambwa aliweza kuchangia maendeleo mbalimbali mkoani Kagera,mojawapo ikiwa kuchangia shule za msingi,sekondari ya Rugambwa,hospitali za Mugana na Kagondo.

“Na mimi najivunia kuhazimisha sherehe hizi, kwani mmojwapo ya watu waliofaidika na mhadhama Kardinali Rugambwa,kwani niliweza kupelekwa Roma kusoma kwa maamuzi yake,”alisema Askofu Kilaini.

Marehemu Rugambwa,anakumbukwa kuwa askofu wa kwanza Mtanzania na Kardinali wa kwanza barani Afrika.

Maadhimisho ya sherehe hizo, yanatarajiwa kuhudhuriwa wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi takribani 15,000,huku Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Chanzo: Mtanzania

Picha Ya Nyumba Za Asili Za Wahaya, Nyegera Waitu Bukoba


Ujenzi wa nyumba za asili za wahaya nyumba maarufu kama 'Omushonge' (msonge) Picha kwa hisani ya J. Kempanju ambae ni mdau nambari moja wa MjengwaBlog kwenye kijiji cha Itahwa- Bukoba.
Picha  zote na Mjengwa Blog

Mwenyekiti Wa Bavicha Taifa John Heche, Aendelea Na Mikutano Mkoa Wa Kagera


Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, akihutubia Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nsisha, Kagoma, Wilayani Muleba, Mkoa wa Kagera.
Picha na Mjenngwa blog

AJABU LAKINI KWELI: BINTI AJIFUNGUA AKIFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA, NI HUKO MULEBA

Binti ajifungua akifanya mtihani wa Darasa la Saba.. alipata uchungu akiwa katika mtihani wa Hisabati, Aliomba ruhusa atoke nje lakini msimamizi akatia ngumu.. Mtoto apewa jina la OMR ....soma zaidi

‘VIJANA JISHUGHULISHENI’

na Antidius Kalunde, Bukoba
VIJANA mkoani Kagera wameshauriwa kujishugulisha na kazi mbalimbali za kuwaletea maendeleo na kutakiwa kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwasaidia kutatua matatizo ambayo yanawakabili kimaisha na kukabiliana na tatizo kubwa la ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa shirika la Maejor Alliance Education Center (MAEC) la mkoani Kagera linalojishugulisha na kupambana na dawa za kulevya hasa kwa vijana, Godfrey Innocent, alitoa ushauri huo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo ikiwemo utawala bora wa asasi na usimamizi wa fedha kwa wanachama wa shirika hilo.
Alisema kuwa kwa hivi sasa nguvu kazi nyingi ya vijana imepotea kutokana na kujihusisha na madawa ya kulevya ikiwemo uvutaji wa bangi unywaji wa pombe uliokithiri jambo ambalo limesababisha vijana kukumbwa na wimbi la umaskini.
Innocent aliongeza kuwa shirika hili la MAEC linajitahidi kwa kasi kubwa kuhakikisha linawashawishi vijana kutambua athari za utumiaji wa madawa ya kulevya na kuwataka wapinge utumiaji huo na kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Edwin Sebastian alisema jumla ya wanachama 45 wamenufaika na kupata mafunzo ambayo yamefadhiliwa na shirika la the Foundation for Civil Society ambao wao ndio watakuwa mabalozi wazuri kwa vijana wengine mkoani Kagera na kuongeza kuwa mbali na kutoa elimu watapata uongozi bora usimamizi wa fedha na uandishi bora wa miradi.
Aliongeza kuwa shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2007 mkoani Kagera limewanufaisha jumla ya vijana 1250 kwa kuwapa elimu bora na kuwanusuru na utumiaji wa dawa za kulevya na wao kuendelea kuwashauri vijana wengine.
Chanzo: Tanzania Daima

MBUNGE AWAPELEKA WAKULIMA 120 KUJIFUNZA UGANDA

Mwandishi wetu, Kagera Yetu
Wakulima 120 kutoka Wilaya ya Bukoba Mkoa Kagera wamepata fursa ya kwenda kujifunza jinsi ya kupambana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba huko Mbarara nchini Uganda.

Akizungumza na waandishi wa habari mjinji Bukoba Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba vijijini Bw. Ahmed Kyobya amesema kila kijiji kimewakilishwa na mkulima mmoja ambao idadi yao ni 92 baada ya kurudi watakuwa walimu wa wakulima kwenye vijiji vyao.

Bw. Kyobya amesema katika msafara huo wamo Madiwani kumi kutoka Halmashauri ya wilaya Bukoba, Maafisa Kilimo wanne,Maafisa wawili kutoka chuo cha utafiti wa kilimo Maruku na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mh,Jasson Rweikiza.

Katibu wa Mbunge huyo amesema ziara hiyo ya siku tatu itaanza Jumanne (Septemba, 18 mwaka huu) kuelekea Mbarara Uganda ambako watapata fursa ya kuwatembelea wakulima mbalimbali na kuwaonyesha jinsi wanavyopambana na ugonjwa huo wa mnyauko.

Aidha safari hiyo imedhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Mh.Jasson Rweikiza baada ya kuona ugonjwa huo unazidi kuongezeka Mkoani Kagera.
Blogzamikoa

USAFIRI KUTOKA KAGERA KWENDA KIGOMA WAREJEA

Na Renatha Kipaka, Bukoba
WAKAZI wa Kagera wanaotegemea huduma ya usafiri kati ya Miji ya Bukoba na Kigoma wamepewa uhakika wa kuwapo na huduma hiyo, baada ya kumalizika kwa mgogoro baina ya Kampuni za Bukoba Express na Vislam, uliodumu kwa mwezi mmoja.

Akizungumza mjini hapa jana, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) mkoani Kagera, Japhet ole Simaye, alisema huduma hiyo imerejeshwa na itakuwa ya uhakika kwa kila wiki.

Alisema tatizo la upatikanaji wa huduma ya usafiri wa kila siku kati ya Mji wa Bukoba na Kigoma lilisababisha abiria wa sehemu hizo kukosa huduma ya usafiri.

Alisema mgogoro uliokuwapo kati ya watoa huduma hiyo ni wa kupinga kuingiliwa katika ratiba zake za kusafirisha abiria ambazo ni Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ambao ulipingwa na Kampuni ya Bukoba Express.

Kutokana na mgogoro huo, ushauri uliopata muafaka ni kuishauri Kampuni ya Bukoba Express kusafirisha abiria Jumanne, Alhamisi na Jumamosi, utaratibu uliotolewa hapo awali na kampuni hiyo kuupinga.

Julai, mwaka huu, SUMATRA walichukua hatua kwa kuwanyang’anya leseni ya usafirishaji wa abiria na kuwarudishia Agosti, baada ya kuomba msamaha na kukubali masharti ya kulipa faini ya Sh 250,000.

Aidha, amewataka wasafiri mkoani Kagera kuondoa shaka juu ya huduma za usafiri, kwa kuwa ofisi hiyo iko tayari kusimamia sheria.
Chanzo: Mtanzania

WANANCHI WAVAMIA MAHABUSU, WAUA MTUHUMIWA

na Ashura Jumapili, Bukoba
WANANCHI wamevamia mahabusu ya Mahakama ya Mwanzo ya Muhutwe, wilayani Muleba na kuvunja milango na kumtoa mtuhumiwa, Faustine Rweyemamu (60), mkazi wa Ndolange-Kamachumu na kisha kumpiga hadi kumuua baada ya kufanya jaribio la kutaka kumwiba mtoto kwa kumpeleka maeneo ya msituni.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mtendaji wa Kijiji cha Bisore, Dominic Damasenyi, alisema mahabusu huyo ameuawa na wananchi kwa kutuhumiwa kuiba mtoto mwenye umri wa miaka 15, aitwaye Zakhia  Hashimu.
Damasenyi alisema wananchi walimuona mwanaume huyo akiondoka na mtoto huyo wakiwa wamefuatana kwa karibu kutokea maeneo ya Muhutwe stendi kuelekea Muleba mjini.
Alisema baada ya wananchi kuona hivyo, walishituka na kuanza kumfuatilia na walipomkamata, askari walimpeleka katika mahabusu hiyo.
“Hali hiyo ilisababisha wananchi wenye hasira kuvamia selo hiyo na kisha kumtoa mtuhumiwa huyo na kuanza kumpiga kwa kutumia mawe hadi kufa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, alithibitsha kutokea kwa tukio hilo.
Chanzo: Tanzania Daima

MWANAFUNZI UAWA, ACHUNWA NGOZI

na Ashura Jumapili, Bukoba
MWANAFUNZI wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyarigamba iliyoko Kata ya Muhutwe wilayani Muleba, mkoani Kagera, Beatha James (12), ameuawa kikatili na kisha kunyofolewa baadhi ya viungo vyake vya mwili na kung’olewa meno.
Mwili wa marehemu ambao ulipatikana baada ya siku nane maeneo ya kambi ya Jeshi la Wananchi Kaboya, ulikutwa umechunwa ngozi, shingo imekatwa, ulimi umetolewa, meno yameng’olewa, sehemu zake za siri zikiwa zimeondolewa na kunyolewa nywele huku akiwa na matundu kichwani.
Kwa mujibu wa maelezo ya mama mkubwa wa marehemu, Eyudosia  Salvatory, aliyekuwa akiishi naye katika Kitongoji cha Bitende, mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani Agosti 29 mwaka huu majira ya saa 3.30 asubuhi akielekea kwa mama yake mdogo mwingine aitwaye Mariagoleti Ishengoma.
Eyudosia alisema baada ya kufika huko alitumwa akafuate maziwa kwa jirani yao aitwaye Erasmo Sostenes, lakini akatumia muda mrefu bila kurejea ndipo walipopiga simu sehemu wanayochukua maziwa  wakaambiwa kuwa hajafika na maziwa bado hayajachukuliwa.
Alisema ilipofika saa saba za mchana walianza kumtafuta ndipo alijitokeza mama mmoja aliyemtaja kwa jina la mama Anneth, akawaeleza kuwa  wakati akiwa shambani majira ya saa nne asubuhi alimuona Beatha akiwa amefuatana na mwanaume mmoja aliyekuwa amebeba mfuko wa ‘safulet’ akamuuliza anakwenda wapi, akamjibu kuwa anamwelekeza mwanaume huyo njia ya kwenda Maziba ziwani maeneo ya Bubabo.
Aliongeza kuwa wananchi waliamua kufuatilia njia hiyo wakishirikiana na wanafamilia kumtafuta mtoto huyo na walipofika Maziba walielezwa kuwa walimuona akiwa amefuatana na mwanaume, lakini hawakujua walikoelekea.
Kwamba wakati  wakielezea  wasifu wa  mwanaume  anayedaiwa  kumchukua mtoto huyo, walielezwa kuwa watu  hao wanatunzwa  kwenye nyumba ya mkazi wa eneo hilo waliyemtaja kwa jina la Jacob na wakati wakielekea huko walikutana na mtoto wake ambaye alikimbilia kwa baba yake.
Eyudosia alifafanua kuwa walipofika kwa Jacob walimhoji ataje walipo watu anaoishi nao, lakini akadai hajui walipo kwani walifika hapo kutafuta kazi na kwamba mmoja wao alimueleza kuwa ana dili la fedha la kwenda kuiba mabati maeneo ya Igurubiri.
Wananchi hao walimchukua Jacob hadi eneo la Muhutwe akiambatana na mtoto wake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 13, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba, na kwamba walipombana alikiri kuwa mwanaume huyo anayetafutwa alifika kwao akiwa na binti, wakalala lakini waliondoka usiku akiwa ameshikwa na vijana.
Eyudosia alisema kuwa baada ya maelezo hayo, walipiga simu polisi ambao walifika na kumpeleka Jacob kituo cha Muleba kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa mtoto.
Alisema Septemba 7 mwaka huu, ndipo walipopata taarifa za kupatikana maiti ya mtoto huyo katika maeneo ya Kaboya karibu na kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwamba taarifa za mwili huo zilitolewa na wawindaji wanaowinda wanyama waharibifu na kuwa walipofika walikuta mwili wa Beatha ukiwa umechunwa ngozi, shingo imekatwa, ulimi umetolewa, meno yameng’olewa, sehemu zake za siri zikiwa zimeondolewa na kunyofolewa nywele huku akiwa na matundu kichwani.
Alisema sura ilikuwa imeharibika hivyo waliweza kumtambua kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa kabla ya kukutwa na mauti.
Mtendaji wa kijiji hicho, Dominic Damasenyi, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba taarifa zilitolewa kwake na wanafamilia.
Damasenyi alisema madaktari walifika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi mwili huo kisha wakaruhusu shughuli za mazishi kuendelea.
Chanzo: Tanzania Daima

WANASIASA WANAOKATAZA WANANCHI KUTOA MAONI YA KATIBA MPYA WAONYWA

Na Mwandishi Wetu, Kigoma Yetu

Viongozi wa Vyama vya Siasa Mkoani Kigoma wameonywa kuacha kuwakataza wananchi wasiende kwenye mikutano ya kutoa maoni yao juu ya mchakato wa katiba mpya.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kigoma Khamis Bitese  alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari Mkoani hapo, ambapo alisema kutokana na mchakato wa utoaji wa maoni wanasiasa wengi wamekuwa wapotoshaji wa jamii, kwa kuwapotosha wanajamii wasiweze kutumia fursa hiyo ili hali wao wanaenda kwenye mikutano mbalimbali ambayo hutolewa na baadhi ya asasi zilizopo.

Bitese aliwataka wananchi kutambua haki zao pasipo kufuata utashi wa vyama vya siasa kwani kwa kufanya hivyo ni kujidhulumu haki zao wenyewe.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Miriam Mbaga alisema wamejipanga vyema kuhamasisha jamii kutoa maoni yao na tayari wameshatoa katiba 18 kwa baadhi ya madiwani ikiwa na chachu ya kuwaelimisha wakazi wa kata zao.

Pia alizitaka asasi zisizo za kiserikali kutumia nafasi zao kuelimisha wakazi wa Mkoa huo. Tume ya kukusanya maoni itaanza kazi zake Mkoani Kigoma kuanzia Septemba 13-28 mwaka huu.

Blogzamikoa

WAJAWAZITO 60% HUFARIKI KWA KUJIFUNGULIA NYUMBANI

na Mbeki Mbeki, Karagwe
DAKTARI Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Nyakahanga, Andrew Cesari, amesema vifo vya wajawazito na watoto wadogo ni asilimia 60 katika Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera kutokana na wanawake kujifungulia nyumbani.
Dk. Cesari alibainisha hayo alipokuwa akisoma risala katika maadhimisho ya miaka 100 ya hospitali hiyo yaliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Nyakahanga wilayani humo.
Alisema hali hiyo inatokana na wajawazito hao kukosa elimu ya afya ya uzazi, hivyo kutoona umuhimu wa kujifungulia hospitali.
Dk. Cesari alisema hospitali hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, wamejipanga kuboresha huduma ya afya kwa kutoa elimu katika makundi yote.
Alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo upungufu wa dawa, waganga, madaktari na watumishi wengine.
Dk. Cesari alisema katika maadhimisho hayo watu zaidi ya 3,000 wamepewa huduma ya matibabu bure, pamoja na kupatiwa vipimo mbalimbali wakiwemo wanawake 108 wa saratini ya matiti na uzazi wa mpango 73.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema serikali inatambua mchango wa kanisa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kiroho na kwamba haitasita kuwaunga mkono.
Alisema serikali imedhamiria kuboresha huduma ya afya kwa kushirikiana na madhehebu ya dini.
Chanzo: Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa