Home » » WAJAWAZITO 60% HUFARIKI KWA KUJIFUNGULIA NYUMBANI

WAJAWAZITO 60% HUFARIKI KWA KUJIFUNGULIA NYUMBANI

na Mbeki Mbeki, Karagwe
DAKTARI Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Nyakahanga, Andrew Cesari, amesema vifo vya wajawazito na watoto wadogo ni asilimia 60 katika Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera kutokana na wanawake kujifungulia nyumbani.
Dk. Cesari alibainisha hayo alipokuwa akisoma risala katika maadhimisho ya miaka 100 ya hospitali hiyo yaliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Nyakahanga wilayani humo.
Alisema hali hiyo inatokana na wajawazito hao kukosa elimu ya afya ya uzazi, hivyo kutoona umuhimu wa kujifungulia hospitali.
Dk. Cesari alisema hospitali hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, wamejipanga kuboresha huduma ya afya kwa kutoa elimu katika makundi yote.
Alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo upungufu wa dawa, waganga, madaktari na watumishi wengine.
Dk. Cesari alisema katika maadhimisho hayo watu zaidi ya 3,000 wamepewa huduma ya matibabu bure, pamoja na kupatiwa vipimo mbalimbali wakiwemo wanawake 108 wa saratini ya matiti na uzazi wa mpango 73.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema serikali inatambua mchango wa kanisa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kiroho na kwamba haitasita kuwaunga mkono.
Alisema serikali imedhamiria kuboresha huduma ya afya kwa kushirikiana na madhehebu ya dini.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa