Home » » ASILIMIA 40 KYERWA WAHAMIAJI HARAMU

ASILIMIA 40 KYERWA WAHAMIAJI HARAMU

na Mbeki Mbeki, Kyerwa
MKUU wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Luteni Kanali (mstaafu) Benedict Kitenga amesema asilimia 40 ya wakazi wake wapatao laki saba ni wahamiaji haramu kutoka nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.
Alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya wilaya kwa Waziri wa Shirikisho la Afrika Mashariki, Samwel John Sitta aliyekuwa katika ziara yake ya kiserikali wilayani humo.
Kitenga alisema kuwa katika kata za Kibingo, Murongo na Kaisho asilimia 70 ya wakazi wake ni wahamiaji haramu kutoka nchi hizo.
Mbali na tatizo hilo, wilaya hiyo pia inakabiliwa na uharibifu wa mazingira na kuharibika kwa migomba inayoshambuliwa na ugonjwa wa mnyauko na uvuvi haramu uliokithiri.
Mkuu huyo aliongeza kuwa tatizo jingine ni kuongezeka kwa usafirishaji magendo ya kahawa kwenda nje ya nchi kunakofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wa Kitanzania.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo ya wakazi, kumekuwa na ongezeko kubwa la utekaji wa magari ya abiria na migogoro ya ardhi na kuonya kuwa vitendo hivyo visipodhibitiwa vinaweza kuharibu uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.
Kitenga alisema kuwa uhamiaji huo haramu unaweza pia kuathiri mradi wa NIDA wa utolewaji wa vitambulisho kwa Watanzania kutokana na mwingiliano wa watu kuwa mkubwa hasa kwa wilaya zilizo mpakani.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alisema kutokana na takwimu za sensa mwaka 2002, wilaya hiyo ina wakazi zaidi ya laki nne na kuwa inasadikiwa kwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kwa ongezeko la watu kwa asilimia 2.9 idadi yao itakuwa ni zaidi ya laki sita.
Kwa upande wake, Waziri Sitta amewataka wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana na serikali kudhibiti vitendo vya uhamiaji haramu, ambapo alisema kuwa Mkoa wa Kagera unasadikiwa kuwa na wahamiaji haramu 18,000.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa