Home » » MGODI WA TULAWAKA SASA KUFUNGWA

MGODI WA TULAWAKA SASA KUFUNGWA



Na Audax Mutiganzi, Bukoba
KAMPUNI ya kuchimba dhahabu ya African Barrick Gold (ABG), inatarajia kufunga eneo la Mgodi wa Tulawaka ulioko wilayani Biharamulo mkoani Kagera, katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja kuanzia sasa.

Kauli hiyo ilisemwa na Mwanasheria wa ABG, Godson Killiza, wakati wa kikao cha pamoja cha na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya mkoa huo.

Alisema Barrick ikishafunga sehemu ya mgodi huo, wataukabidhi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Misitu na Nyuki wautumie kama msitu wa hifadhi.

Alisema kampuni hiyo imeanza hatua za awali za kufunga eneo la mgodi, ambazo ni pamoja na kuotesha miti katika maeneo ya Kijiji cha Mavota kinachozunguka mgodi huo, kusawazisha ardhi na kuotesha mimea na nyasi za asili.

Alisema kampuni hiyo ina mkakati mkubwa wa kuyashirikisha makundi mbalimbali kabla ya kuufunga mgodi kwa njia ya vikao.

Alisema kampuni hiyo tayari imeshafanya vikao na ujumbe wa Wizara ya Maji, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wizara ya Nishati na Madini, Baraza la Usimamizi wa Mazingira na Idara ya Misitu na Nyuki.

Alisema kampuni hiyo inaendelea na kuandaa vikao zaidi vya kujadili mikakati ya kuufunga mgodi huo.

Aidha, alisema watakutana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Wizara ya Fedha na Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), waandishi wa habari na wananchi wanaozunguka mgodi wa Tulawaka.

Alisema baada ya kufungwa eneo la mgodi huo, miundombinu na mali nyingine, ukiwamo uwanja wa ndege, mashine saba za kuzalisha umeme, eneo la makazi, karakana kubwa mbili, makontena na majengo ya utawala vyote vitakabidhiwa kwa Serikali.

Alisema Barrick inataka kuliacha eneo la mgodi likiwa na uasili wake.

Alisema mashimo yote yaliyokuwa yamechimbwa katika eneo la mgodi yatafunikwa.

Aidha, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, kuwa kabla ya kufunika mashimo hayo kampuni itahakikisha inafanya ukaguzi ndani ya mashimo hayo kwa ajili ya wavamizi wa machimbo wasifunikwe.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa