Kilaini atoa neno la 2014

Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki nchini, Jimbo Kuu la Bukoba, mkoani Kagera, Method Kilaini ametoa wito kwa Watanzania kupiga vita viashiria vya uvunjifu wa amani.

Alisema mwaka 2014, Watanzania wote wanapaswa kuilinda amani iliyopo hasa kipindi hiki cha mchakato wa kupata Katiba Mpya kwani wapo baadhi ya watu wachache wanaoonesha
viashiri vya uvunjifu wa amani.

Askofu Kilaini aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Majira ili kupata maoni kwa Watanzania ambao leo saa sita usiku, watauanza mwaka mpya wa 2014.

"Amani tuliyonayo hatupaswi kuichezea hata kidogo, nchi nyingine wanaitafuta kwa muda mrefu na hawaipati hivyo tusiruhusu mtu yeyote aichezee amani yetu," alisema.

Aliwataka Watanzania kuendeleza umoja na mshikamano dhidi yao bila kujali dini, ukabila wala rangi

Chanzo;Majira

Wanasiasa wamchefua January Makamba

image

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw.January Makamba, amekemea tabia ya baadhi ya wanasiasa nchini kutumia mkondo wa dini kisiasa kwani hilo ni kosa
kubwa kwa mustakabali wa amani ya nchi.

Bw. Makamba aliyasema hayo juzi Mjini Bokoba, mkoani Kagera, wakati akizungumza kwenye Tamasha la Amani ambalo liliandaliwa na Nazareth Singers kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Alisema wanasiasa wenye tabia hiyo wanaamini kuwa waumini wa dini yake watamuunga mkono katika uchaguzi jambo ambalo ni hatari kwa sababu anapogombea uongozi, wananchi ndio wanaopiga kura bila kujali dini zao.

Aliongeza kuwa, viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa ya kulinusuru Taifa kutokana na chokochoko za kidini kupitia mahubiri yao kwani bila wao, hali ingekuwa mbaya zaidi.

Aliwaomba viongozi wa madhehebu ya dini nchini, kuendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania ili kudumisha amani iliyoasisiwa na Hayati Julius Nyerere.

"Baada ya kuibuka kwa chochoko za kidini nchini, viongozi wa dini wamefanya kazi kubwa ya kuhubiri amani, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi...mahubiri yao
yamesaidia kupunguza chokochoko hizo," alisema.

Bw. Makamba alisema madhara ya Taifa kukosa amani ni makubwa na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuheshimu imani za watu wengine.

Alikemea tatizo la ukosefu wa haki na usawa katika jamii juu ya upatikanaji wa huduma mbalimbali za msingi ikiwemo elimu na afya miongoni mwa Watanzania.

"Unapoona katika jamii hakuna haki na usawa hilo ni tatizo,kwa mfano, ukiona kuna watu wanapata elimu au huduma tofauti na wanayopata wengine, uhakika wa amani
unakuwa hatarini," alisema.

Aliwapongeza waandaaji wa tamasha hilo ambalo liliwakutanisha waumini wa dini mbalimbali mkoani humo na kusisitiza kuwa, ujumbe uliotolewa usambazwe nchi nzima.

Aliahidi kusaidiana na waandaaji hao kuhakikisha ujumbe huo wa amani unafika maeneo mbalimbali nchini.

Awali Mkuu wa Mkoa huo, Kanali mstaafu Fabian Massawe,alisema amani ya Tanzania ipo mashakani kutokana sababu mbalimbali kama malumbano ya kidini, kisiasa, matumizi ya dawa za kulevya kwa unyanyasaji wa kijinsia.

Chanzo;Majira

MISSENYI YATOA MIKOPO MIL 60

Halmashauri ya wilaya ya Missenyi mkoani Kagera imetoa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 60.1 kwa vikundi mbalimbali vya wanawake na vijana katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Elzaberth Kitundu imesema kuwa mikopo hiyo imetolewa kuanzia mwaka wa fedha 2007/2008 hadi 2012/2013.

Kitundu amesema kuwa katika kipindi hicho vikundi vya akina mama vilipatiwa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 40.8 ambapo  vikundi vya vijana vilipatiwa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 19.3.

Amesema kuwa lengo la halmashauri hiyo kuviwezesha vikundi vya wanawake na vijana kwa kuwapatia mikopo  ni kutaka  kuinua mitaji yao,  na kuwa hali ya marejesho kwa vijana sio mbaya isipokuwa kwa upande wa wanawake ndio wanarejesha kwa kusuasua.

Amesema kuwa katika kuhakikisha vikundi hivyo vinakuwa endelevu, wamekuwa wakiwashauri wanachama wake kuanzisha vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na kuwa katika wilaya hiyo hadi sasa kuna vyama vya ushirika 73, vikiwamo vya mazao 28, Saccos 36 ambapo vyama tisa ni vya mchanganyiko.

Wahamiaji warudi kwa kasi Kagera

Katika hali isiyo ya kawaida, wahamiaji haramu waliorejeshwa nchini mwao na serikali katika ‘Operesheni Kimbunga’ wameanza kurejea kwa wingi katika Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera wakijiita M23 na kupora mali za wananchi kwa nguvu.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Benedict Kitenga, aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa huo Kanali mstaafu, Fabian Massawe ambaye alitembelea wilaya hiyo kukagua shughuli za maendeleo na ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za kata.
Alisema wahamiaji hao wamejazana katika Kijiji na Kata ya Kibingo wakiwatisha wananchi ambao hivi sasa wanahofia usalama wa maisha yao na mali zao.
Aliongeza kuwa, baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kupata taarifa hizo, ilikwenda eneo la tukio na kufanya operesheni kubwa na kufanikiwa kukamata wahamiaji haramu zaidi ya 20 na baadhi ya Watanzaia waliokuwa wakiwahifadhi.
Mhandisi Kitenga alisema baada ya kukamatwa, wahamiaji hao walirudishwa katika nchi zao bila kutaja uraia wao na Watanzania waliohusika kuwahifadhi wamechukuliwa hatua za kisheria.
“Kutokana na hali ilivyo, wananchi wanapaswa kutoa taarifa wawaonapo wahamiaji haramu katika maeneo yao,” alisema.
Kwa upande wake, Bw. Massawe alisema, katika “Operesheni Kimbunga”, wahamiaji haramu walirudishwa katika nchi zao, lakini operesheni hiyo inaendelea ili kuhakikisha waliobaki wanakamatwa na kurudishwa nchini mwao.
“Chini ya Kaulimbiu ya Hakuna wa Kubaki na Hakuna wa Kurudi, tutahakikisha kila mhamiaji haramu anaondoka na Watanzania ambao watabainika kushirikiana nao pia watachukuliwa hatua za kisheria.
“Naiagiza Kamati za Ulinzi na Usalama kuendelea na operesheni hadi wahamiaji haramu wamalizike,” alisisitiza Bw. Massawe na kuwataka wananchi watoe taarifa kwa viongozi wanapowaona na kutoa namba zake za simu.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliohojiwa walisema tatizo la wahamiaji haramu linachangiwa na baadhi ya watendaji wa Serikali ngazi za chini ambao wanachukua hongo na kuwarudisha.
Walisema inavyoonekana, viongozi wa chini kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji hadi kata, wamepewa mamlaka makubwa pia wamekuwa wakikaa muda mrefu bila kubadilishwa vituo vya kazi na hivyo kujenga mazoea na wahamiaji hao.
“Serikali kuanzia ngazi ya Wilaya, iwe na utamaduni wa kuwatembelea viongozi wa vitongoji na kata kwa kushtukiza ili kukomesha tabia hii ambayo wamejijengea na kuonekana miungu watu katika maeneo yetu,” alisema mkazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Hivi karibuni Serikali ilifanya “Operesheni Kimbunga” na kushirikisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa wiki mbili kwa wahamiaji haramu wawe wameondoka nchini kwa hiari yao.

Chanzo;Majira

Waziri Magufuli atajwa kesi ya wizi wa pembejeo

Waziri wa Ujenzi, Dk,John Magufuli
 
Kesi ya ubadhilifu wa fedha za pembejeo za kilimo inayowakabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Chato, Hadija Nyembo, aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hamida Kwikwega na wenzao watatu, imechukua sura mpya baada ya mawakili wa washitakiwa kumtaja Waziri wa Ujenzi, Dk, John Magufuli, kuhusika.
Hatua hiyo imefuatia Mahakama hiyo kuanza kupokea ushahidi wa upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kelvin Murusuri.

Shahidi namba moja ambaye ni mchunguzi wa Takukuru, Said Bakari (39), alidai kuwa kwa kipindi cha mwaka 2010/11 washitakiwa hao walitenda makosa mbalimbali ikiwemo kutumia madaraka yao vibaya kisha kumteua wakala wa usambazaji wa pembejeo asiye na sifa.

Alisema mshitakiwa namba moja Nyembo ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Chato kabla ya kuhamishiwa Uvinza, akiwa Mwenyekiti wa kamati ya pembejeo ya wilaya hiyo alihusika kuwapitisha wazabuni wa usambazaji wa pembeo wasio na sifa katika kikao kilichofanyika Julai 6, mwaka 2010.

Alidai kuwa mshitakiwa namba mbili Kwikwega anayetetewa na wakali wa kujitegemea Deogratias Rutahindurwa, alidaiwa mahakamani kupitisha baadhi ya nyaraka za kuwatambulisha mawakala waliopitishwa kinyume cha sheria na kamati ya pembejeo ya wilaya kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Wengine waliofikishwa mahakamani ni aliyekuwa Ofisa Kilimo na Mifugo wa wilaya hiyo, Dk. Pheres Tongora, ambaye pia aanashitakiwa kuteua na kuwapitisha mawakala wasio na sifa.

Wengine ni mshitakiwa namba nne aliyekuwa wakala wa usambazaji wa pembejeo kata ya Buseresere, Mery David pamoja  na Kaimu mtendaji wa kijiji cha Mapinduzi, Mageni Mbassa.

Shahidi huyo aliwasilisha vielelezi vinne zikiwemo barua na mihutasari ya vikao vya kamati ya pembeo vilivyoketi na kupitisha maamuzi ya kuwapata mawalala wa usambazaji bila kufuata taratibu za manunuzi ya umma.

Baada ya mashahidi wa kwanza kumaliza kuwasilisha ushahidi wake, wakili wa Rutahindurwa alitaka kujua sababu za Waziri wa ujenzi na mbunge wa jimbo la Chato,Dk Magufuli kushindwa kuhusishwa katika mashitaka hayo licha ya kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya pembejeo ya wilaya hiyo.

Alisema iwapo kamati ya pembejeo ilifanya maamuzi yasiyo fuata taratibu kanuni na sheria za manunuzi iweje baadhi ya wajumbe wake akiwemo Dk. Magufuli wasihusishwe kwenye mashitaka hayo.

Wakili anayemtetea Mery David,Tuguta Fadhili alihoji kuwa kama kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kutokana na shinikizo la Waziri wa Ujenzi Dk. Magufuli.

Alidai kuwa iwapo kikao cha kamati ya pembejeo kiliyoketi Julai 6, 2010 kilikuwa halali iweje maamuzi yake yaonekane hayakuwa sahihi na kumhusisha pia mshitakiwa namba mbili (Kikwega) ambaye siku ya kikao hicho hakuwapo katika maamuzi hayo.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Jovith Katto baada ya upande wa washitakiwa kumaliza kuhoji maswali yao mahakama hiyo iliahilishwa kwa ajili ya kupokea ushahidi wa mashahidi namba mbili ambaye ni Ofisa Ugavi wa wilaya hiyo, Machage Mwema.
 
CHANZO: NIPASHE

Ulaji wetu na maradhi ya kisukari-3

Tulijifunza katika makala mbili zilizopita kuwa binadamu hawezi kuishi bila ya kula vyakula vyenye wanga, mafuta na protini.
 Njia za kuyakabili maradhi ya kisukari
Tunaweza kuyakabili maradhi ya kisukari kwa njia kuu nne. Mosi, kuwa na elimu kuhusu maradhi ya kisukari na mtu kuwa na uwezo wa kujipima kiwango cha sukari mwilini mwake.
Pili, ni kula mlo kamili, tatu kufanya mazoezi na nne ni kupata tiba sahihi ya maradhi ya kisukari.
Njia hizi ni muhimu kuzifahamu kwa wagonjwa wa kisukari na wale ambao hawajapatwa na maradhi hayo, yanayoongezeka kwa kasi duniani kutokana na maisha ya kisasa kama vile kula vyakula vyenye mafuta, sukari na chumvi nyingi.
Kama umepatwa na kisukari
Ingawa maradhi ya kisukari yana kishindo kikubwa, lakini watu waliopatwa na ugonjwa huo wanashauriwa wasichanganyikiwe wala kuhuzunika. Kufanya hivyo ni kuongeza maradhi katika miili yao.
Wanachotakiwa ni kuukabili ugonjwa huo kwa kujiamini. Na hilo litawezekana endapo wagonjwa hao wataelekeza nguvu zao katika kuujua ugonjwa huo kwa undani.
Kujua huko kutawafanya wabadili mtindo wa maisha yao kama vile kula mlo kamili, kufanya mazowezi, kuacha kunywa pombe, kunywa maji ya kutosha, kulala muda wa kutosha, kudhibiti hasira na msongo wa mawazo.
Wapi utapa elimu?
Elimu kuhusu maradhi ya kisukari inaweza kupatikana kwa njia mbalimbali kama vile kusoma vitabu na magazeti, kusoma katika mitandao ya kijamii, kuhudhuria semina, kusikiliza vipindi vya mada hiyo kutoka katika redio na luninga.
Vilevile, elimu ya ugonjwa wa kisukari inaweza kupatikana kwa wataalamu wa maradhi hayo waliopo katika kniniki za kisukari na hospitali mbalimbali.
Baadhi ya wagonjwa wa kisukari pia, wanaelimu kubwa ya maradhi hayo baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kuitafuta elimu hiyo na uzoefu wao wa maisha kama wagonjwa.
Kuujua ugonjwa wa kisukari
Kama tunavyofahamu, binadamu ameweza kuleta mapinduzi makubwa katika maisha yake tangu enzi za zana za mawe mpaka sasa, enzi za dijitali kutokana na elimu.
Ni dhahiri pia, kuwa tutaweza kuyakabili maradhi ya kisukari kikamilifu kama tutakuwa na uwelewa wa kutosha juu ya maradhi hayo.
Tufahamu nini kama wananchi?
Kujua tunakokukusudia hapa sio kama vile wanavyofahamu wataalamu wa afya.
Wananchi wajue maana ya ugonjwa wa kisukari, aina za kisukari, sababu za kupata maradhi ya kisukari na dalili za kisukari.
Halikadhalika, watu wanatakiwa watambue hali gani mtu akiwa nayo (risk factors) yuko katika hatari ya kupata maradhi ya kisukari kama vile unene uliopitiliza, kuwa na shinikizo la damu, kuwa na msongo wa mawazo, ujauzito, kutokufanya mazoezi au kazi za kutoka jasho, na kuwa na miaka arobaini au zaidi.
Zaidi ya hayo, watu wanatakiwa wazijue athari mbaya za ugonjwa wa kisukari kama vile kuharibika kwa viungo vingine mfano macho, viungo vya uzazi, figo, mishipa ya fahamu na moyo.
Chanzo;Mwananchi

UWK: Wanawake pazeni sauti zenu

UMOJA wa Wanawake Wajane (UWK) Wilayani Karagwe umesema unyanyasaji wa kijinsia katika jamii unaweza kutokomezwa iwapo wanawake watavunja ukimya na kupaza sauti zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mwenyekiti wa umoja huo, Grace Mahumbuka, alisema kuwa unyanyasaji wa kijinsia  utakoma ikiwa wanawake watavunja ukimya na kupaza sauti zao na kuripoti matukio  ya kikatili.
Alisema kuwa baadhi ya wanawake na watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kubakwa, ukatili wa kingono, kulawitiwa, ndoa za utotoni na kutakaswa kwa wajane lakini matukio hayo yanashindwa kuripotiwa.
“Matukio ya unyanyasaji wa kijinsia  ni sawa na majanga mengine ya kitaifa, kwa wanawake wengi na baadhi ya watoto wamefanyiwa vitendo vya kikatili,” alisema.
Alisema ukatili huo wa kijinsia unahusiana zaidi na vipigo kwa wanawake kutoka waume zao na hata baadhi  kujeruhiwa, kukatwa viungo vyao vya mwili hali inayoweka rehani ubinadamu wao.
Alisema kuwa kuna umuhimu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kusambaza elimu vijijini ili kusaidia kupunguza matukio hayo.
Naye Diwani viti maalum (CCM) kata ya Kayanga, Joyce Mirembe aliwataka waandishi wa habari kuhakikisha hawaegemei upande wowote wanaporipoti matukio hayo.
Alisema mfumo wa kisheria uliopo unaoonekana kutokuwa na usawa huchangia wanawake kufanyiwa vitendo hivyo kushindwa kuchukua hatua za kisheria.
Chanzo;Tanzania Daima
UMOJA wa Wanawake Wajane (UWK) Wilayani Karagwe umesema unyanyasaji wa kijinsia katika jamii unaweza kutokomezwa iwapo wanawake watavunja ukimya na kupaza sauti zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mwenyekiti wa umoja huo, Grace Mahumbuka, alisema kuwa unyanyasaji wa kijinsia  utakoma ikiwa wanawake watavunja ukimya na kupaza sauti zao na kuripoti matukio  ya kikatili.
Alisema kuwa baadhi ya wanawake na watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kubakwa, ukatili wa kingono, kulawitiwa, ndoa za utotoni na kutakaswa kwa wajane lakini matukio hayo yanashindwa kuripotiwa.
“Matukio ya unyanyasaji wa kijinsia  ni sawa na majanga mengine ya kitaifa, kwa wanawake wengi na baadhi ya watoto wamefanyiwa vitendo vya kikatili,” alisema.
Alisema ukatili huo wa kijinsia unahusiana zaidi na vipigo kwa wanawake kutoka waume zao na hata baadhi  kujeruhiwa, kukatwa viungo vyao vya mwili hali inayoweka rehani ubinadamu wao.
Alisema kuwa kuna umuhimu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kusambaza elimu vijijini ili kusaidia kupunguza matukio hayo.
Naye Diwani viti maalum (CCM) kata ya Kayanga, Joyce Mirembe aliwataka waandishi wa habari kuhakikisha hawaegemei upande wowote wanaporipoti matukio hayo.
Alisema mfumo wa kisheria uliopo unaoonekana kutokuwa na usawa huchangia wanawake kufanyiwa vitendo hivyo kushindwa kuchukua hatua za kisheria.
Chanzo;Tanzania Daima

`Sheria ya kuzuia shughuli za siasa vyuoni itazamwe upya`

Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Kagera,Pius Ngeze.
 
Serikali imeshauriwa kuiangalia upya Sheria ya Vyuo namba 7 ya mwaka 2005 inayozuia kufanya mikutano na shughuli za vyama vya siasa ndani ya maeneo ya vyuo.
Ushauri huo ulitolewa na mwakilishi wa wanachuo wa Chuo Kikuu cha St. Augustine (Saut) tawi la Sokoine Kampasi ya Bukoba, wakati wa hafla ya kukabidhi kadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wanachuo 42 wa chuo hicho waliojiunga na chama hicho.

Risala ya wanachuo hicho ilisomwa na mwakilishi wao, Silas Malima, mbele ya mgeni rasmi, Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Kagera, Pius Ngeze.

Malima alisema wanakabiliana na changamoto ya Sheria Vyuo Vikuu Namba 7 ya mwaka 2005.

Kwa mujibu wa Malima, sheria hiyo inayozuia kufanya mikutano na shughuli za vyama vya siasa ndani ya maeneo ya chuo.

Kwa msingi huo, Malima aliishauri serikali kuitazama upya sheria hiyo kwa lengo la kuirekebisha.

Kwa upande wake, mgeni rasmi Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoani Kagera, Ngeze, mbali ya kukabidhi kadi hizo kwa wanachama wapya 42 wa chuoni hapo, pia aliwataka wanachama hao wapya  pamoja na wa zamani, kuhakikisha kwamba wanawaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi.

Ngeze alisema vile vile, viongozi wa Chama wanapaswa kuwaeleza wananchi ukweli huo kwani  vinginevyo viongozi wa upinzani watawaeleza  na kupindisha mafanikio hayo au kuyafanya ni yao.

Ngeze aliyataja baadhi ya mafanikio hayo yalifanywa na serikali chini ya CCM kuwa ni pamoja na usambazaji wa umeme vijijini na mijini, usambazaji wa maji safi na salama mijini na vijijini, mawasiliano ya simu, ujenzi wa barabara za lami na changarawe vijijini na mijini.

Mengine ni usafiri na usafirishaji wa barabara, reli na anga, upanuzi na uboreshaji wa elimu ya msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu.

Aidha, Ngeze alisema jukumu la tawi la CCM katika vyuo vikuu hususani tawi la Saut Bukoba, ni pamoja  na kujenga na kukiimarisha Chama ndani ya Jumuiya ya Chuo Kikuu; kuongeza idadi ya wanachama na kufanya vikao kwa mujibu wa katiba.

Pia aliwataka viongozi na wanachama waendelee kujiendeleza ili kuwaongoza watu; wasome magazeti wasikilize redio, waangalie televisheni na washiriki majadiliano mbalimbali.

 
CHANZO: NIPASHE

Mhandisi adaiwa kumuua afisa mauzo wa Sigara

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania,(IGP) Said Mwema
 
Jeshi la polisi mkoani Kagera linamshikilia mhandisi wa ujenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Nassoro Robert (56), kwa tuhuma za kumuua afisa mauzo wa kampuni ya Sigara kwa kumpiga risasi ya kichwa.
Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe, alimtaja aliyeuawa kuwa ni Hassan Mhongoli (38) na kuwa mauaji hayo yalitokea Jumamosi iliyopita saa 3:45 usiku katika eneo la hoteli ya Bukoba Coop inayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU 1990 Ltd).

Mwaibambe alisema kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumetokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambapo walianza kumfuatilia na kufanikiwa kumkamata juzi saa 9:00 mchana akiwa amejificha nyumbani kwake eneo la Uzunguni katika Manispaa ya Bukoba.

Alisema baada ya kumkamata alionyesha bastola aina ya Glock yenye namba PCH589 anayoimiliki kihalali ambayo inadaiwa aliitumia katika mauaji hayo na kudai kuwa alifikia uamuzi huo baada ya kupigwa ngumi na marehemu.

Alisema kuwa kampuni ya Sigara siku hiyo walikuwa na sherehe ya familia ambayo ilimalizika saa moja jioni na kwamba baadhi ya wafanyakazi waliondoka katika eneo hilo na kumwacha Hassan akiwa na mfanyakazi mwenzake, Amon Lyimo (40).

Alisema watu hao walikaa katika hoteli hiyo hadi saa 3:45 ndipo waliingia katika gari la kampuni, lakini walipoanza kuondoka ghafla ilitokea teksi na kuziba njia. Alisema  walipiga honi, lakini  haikuwapisha.

Alisema kutokana  na kitendo hicho wafanyakazi hao wa Sigara walishuka katika gari na kuanza kuzozana na waliokuwa katika gari hilo na kwamba baadaye alishuka mtu mmoja na kuanza kupigana nao na baadaye kutoa bastola na kumpiga risasi Hassan  kichwani na kufariki dunia papo hapo.

Alisema katika purukushani hizo mfanyakazi mwingine wa Sigara, Amon Lyimo, alitaka kuwamua, lakini  naye alipigwa risasi mkono wa kulia na ametibiwa katika Hospitali ya Mkoa na kuruhusiwa jana.

Mwaibambe alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi na kuwa bastola hiyo ilikutwa na risasi tano na waliokota maganda mawili ya risasi eneo la tukio.
Mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi  umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera ukisubiri kuchukuliwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi.
 
CHANZO: NIPASHE

Maofisa ugani watakiwa kuwa na mavazi ya shamba

MKUU wa Wilaya ya Muleba, Lembris Kipuyo, amewaagiza maofisa ugani wa halmashauri hiyo kuwa na mavazi ya shambani yaliyowekewa nembo ili watambulike kwa wakulima.
Kipuyo alitoa agizo hilo katika kongamano la mtandao wa vikundi vya wakulima wadogowadogo (Mviwata) mkoani Kagera la kuibua changamoto za kilimo lililofanyika wilayani hapa.
Mkuu huyo wa wilaya (DC), alisema lengo la kutaka kuwepo na vazi maalum la kuwatambua maofisa ugani linatokana na maafisa ugani walio vijijini kufanana na wakulima, hivyo kuwapa wakati mgumu baadhi ya wakulima kuwatambua pindi wanapowahitaji.
Alisema wataalam hao wa kilimo ni wachache katika halmashauri hiyo yenye vijiji 161 ambao hawatoshelezi mahitaji ya wakulima kwa wakati kutokana na ukosefu wa miundombinu ya usafiri.
Alisema wilaya hiyo iko kwenye mkakati wa kuwawezesha maofisa ugani wachache ambapo mmoja ataweza kuhudumia vijiji vitatu na kuwafikia wakulima kwa ukaribu zaidi kwa kuwapatia pikipiki.
Alisema mpango huo utasaidia ukusanyaji wa takwimu za kilimo kupitia maafisa ugani kwa kuwezeshwa usafiri na vitendea kazi vya kutosha.
Mbali na hilo, aliwatahadharisha wakulima kuhusu kuhifadhi mazingira na kuwataka kuacha tabia ya kulima kwenye vyanzo vya maji.
Chanzo;Tanzania Daima

Wafugaji wawasusia DC,DAS

Mbunge wa Kahama,James Lembeli,
 
Kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inayosikiliza na kuchunguza athari zilizotokana na Operesheni tokomeza Ujangili katika maeneo mbalimbali ya nchi, imejikuta katika wakati mgumu baada ya Chama cha Wafugaji Kanda ya Ziwa kukataa kukutana nayo katika kikao kilichowashirikisha  Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Richard Mbeho, na Katibu Tawala wa wilaya, Venant Belege, kwa madai kuwa hawana imani na viongozi hao.
Kamati  hiyo ipo wilayani Biharamulo, mkoani Kagera kusikiliza na kuchunguza athari zilizotokana na operesheni hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli, na jana ililazimika kuzungumza na kusikiliza hoja za wafugaji bila viongozi hao kuwapo.

Mbali na kuwakataa viongozi hao, walisema uongozi mzima wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na askari wa hifadhi ya wanyamapoli na Jeshi la Polisi, ndiyo walikuwa mstari wa mbele kuwahujumu wafugaji wakati wa operesheni hiyo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Juvenary Mlashani, alisema licha ya Rais Jakaya Kikwete, kusitisha operesheni hiyo kutokana na baadhi ya viongozi kukiuka taratibu na madhumuni yake, jambo la kushangaza zoezi hilo kwa wilaya ya Biharamulo linaendelea.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakipuuza kwa makusudi maagizo ya Rais Kikwete kutokana na kutafuta maslahi binafsi. Projestus Rutimwa, alisema kuwa suala la  ufugaji wa ng’ombe ndani ya Hifadhi ya Biharamulo hautakwisha iwapo viongozi waliopewa dhamana na serikali wataendelea kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji.
 
CHANZO: NIPASHE

Mwalimu jela miaka saba kwa kumkata kiganja mwanafuzi

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Rwambai Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Alliamin Mtabuzi (25), amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana na kosa la kumkata kiganja cha mkono mwanafunzi wake wa kidato cha nne.
Mtabuzi alipatikana na kosa la kumsababishia ulemavu mwanafunzi huyo, Annocietha Theobart (16), kutokana na wivu wa mapenzi.

Mbali ya kifungo hicho, pia ameamriwa kumlipa mlalamikaji huyo fidia ya Shilingi milioni tano.

Hukumu hiyo ilitolewa na Novemba 27, mwaka huu na Jaji Peragia Hadai wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji Hadai alisema itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali, Wakili wa Serikali, Safina Simba, alidai  kuwa mshatakiwa alitenda kosa hilo mwaka 2008 katika kijiji cha Rwambai wilayani Karagwe nyumbani kwa mlalamikaji kwa madai kwamba mwanafuzi huyo alikuwa na mchumba mwingine.

Baada ya kufika nyumbani hapo, mshtakiwa alianza kumshabulia mama mzazi wa mlalamkaji kabla ya kumshambulia malalamikaji kwa panga na kumkata kiganja cha mkono wa kulia pamoja na kidole cha mkono wa kushoto.

Hata hivyo, mwanafunzi huyo katika ushahidi wake alidai mahakamani hapo kuwa hakuwa na makubaliano ya uchumba na mshtakiwa.

Naye wakili wa utetezi, Alliamini Chamani, alidai kuwa mahakama inastahili kumpunguzia adhabu mshtakiwa kwa kuzingatia kuwa alikuwa mchumba wa mlalamkaji kwa makubaliano angemuoa baada ya kumaliza shule.

Alidai kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akimgharimia mlalamikaji karo ya shule na mahitaji mengine yote muhimu hivyo alikasirishwa baada ya kubaini  alikuwa na mchumba mwingine.

Hata hivyo, Mahakama iliotupilia mbali utetezi huo na kumpa mshtakiwa adhabu ya kifungo cha miaka saba pamoja na kumlipa mlalamikaji fidia ya Sh.milioni 5.
CHANZO: NIPASHE

DKT.BILAL AENDESHA ZOEZI LA HARAMBEE YA KUCHANGIA MADAWATI MFUKO WA MAENDELEO YA ELIMU JIMBO LA NKENGE

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi chaeti, Mkurugeniz wa Kagera Sugar, Bw. Hamadi Yahaya, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake wa kuchangia maendeleo ya Elimu ya Jimbo la Nkenge mkoa wa Kagera,wakati wa hafla ya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Nkenge kununua madawati ili kusadia shule za msingi za Jimbo hilo. Harambee hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Asumpta Mshana na (kushoto kwa Makamu) ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali (mst) Fabian Masawe. Jumla ya Shilingi milioni 114, pesa taslimu milioni 65.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza wakati wa hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Nkenge kununua madawati ili kusadia shule za msingi za Jimbo hilo. Harambee hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam, jana usiku. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Asumta Mshana na (kushoto kwa Makamu) ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanal Fabian Masawe. 
 - Sehemu ya wageni waalikwa kutoka mkoa wa Kagera waliohudhuria harambee hiyo
 Baadhi ya wageni waalikwa kutoka mkoa wa Kagera waliohudhuria harambee hiyo
 Meza Kuu wakijumuika kuimba wimbo maalumu wa mkoa wa Kagera wa kuhamasisha maendeleo ya mkoa huo, hususan katika suala la elimu na kuchangia madawati.
Msanii Saida Karoli na kundi lake wakiburudisha wakati wa hafla ya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Nkenge kununua madawati ili kusadia shule za msingi za Jimbo hilo. Harambee hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo. Picha na OMR.



Tibaijuka ataka soko la ndizi Muleba

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amewataka madiwani wa Halmashari ya Muleba, mkoani Kagera, kujenga soko la ndizi la kisasa kwa ajili ya mahitaji ya wananchi na kupanua ajira kwa jamii.
Tibaijuka alitoa kauli hiyo juzi mjini Muleba, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, ambaye pia ni mbunge wa Muleba Kusini (CCM), madiwani wa wilaya hiyo wanatakiwa kuweka mikakati ya ujenzi wa soko hilo, kwa kuzingatia zao hilo ni muhimu kwa wananchi wa Muleba na mkoa kwa ujumla.
“Naamini sisi madiwani wa Muleba tukijenga soko la ndizi itasaidia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi wetu. Maana itawarahisishia wananchi kupata mahitaji eneo sahihi,” alisema.
Aidha, waziri  aliwataka madiwani kusimamia ardhi ya wananchi kwa umakini, na kuongeza kuwa diwani yeyote  haruhusiwi kugawa ardhi bali anatakiwa kusimamia kwa uangalifu rasilimali hiyo.
Diwani wa Kamachumu, Dunstan Mutagywa (CCM) aliunga mkono wazo la waziri huyo na kusema soko la ndizi linatakiwa kujengwa kwenye eneo ambalo wananchi watapata wateja.
Alisema endapo watajenga soko hilo sehemu nzuri ambayo wananchi atafanya biashara, itasaidia katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu karibu na jamii yenyewe.
Chanzo;Tanzania Daima

WASSIRA: SERIKALI HAINA AJIRA ZA KUTOSHA KWA VIJANA




Vijana kote nchini wametakiwa kubuni mbinu mbadala ya kujiajiri wenyewe ili waweze kujikwamua katika umaskini, badala ya kutegemea ajira za serikali pekee ambazo hazitoshelezi mahitaji yaliyopo.

Rai hiyo imetolewa na waziri ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira wakati akikagua miradi ya mfuko wa maendeleo ya jamii nchini (TASAF) katika wilaya ya Ngara.

Waziri Wassira alisema kuwa serikali haina uwezo wa kuajiri vijana wote hapa nchini,  inachokifanya ni kubuni namna wananchi watakavyotumia fursa zilizopo kujiajiri kupitia sekta mbalimbali hasa ya kilimo.

Miongozi mwa miradi ya Tasaf aliyoitembelea ni pamoja na mradi wa kikundi cha vijana 25 walioibua mradi wa kufuga mbuzi  katika kijiji cha Ibuga kata Kabanga, ambao wamejiinua kiuchumi kupitia mradi huo.

Akisoma risala katibu wa kikundi hicho Bahati Philmon, amesema kuwa  baada ya kuona kupata ajira za serikali kumeshindikana, wao kama vijana walijiunga katika kikundi na kupatiwa fedha kutoka Tasaf kwa ajili ya kuanzisha mradi huo wa ufugaji wa mbuzi, ulioibuliwa katika mkutano wa hadhara mwaka 2009.

Philmon amesema kuwa  walipata shilingi milioni 11 kutoka Tasaf, na kununua mbuzi 105, ambapo  kila mmoja wao alipata mbuzi wanne, na kuwa sasa wana jumla ya  mbuzi 200, na kila mmoja amekwishafikisha mbuzi kumi.

Amesema kuwa jumla ya gharama ya mradi huo ni zaidi ya shilingi milioni 12.5 na kuwa mbali na fedha zilizotolewa na Tasaf, wananchi walichangia nguvu zao zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5.

Amesema kuwa kutokana na ufugaji huo vijana  kumi miongoni mwao wameweza kuanzisha kilimo cha mazao mbalimbali katika shamba lenye ukubwa wa ekari nane, ikiwamo mashamba ya migomba ya kisasa, kahawa na magimbi.


Muleba yashauriwa kusogeza huduma za afya kwa wananchi


HALMASHAURI ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera imeshauriwa kusogeza huduma za afya  kwa wananchi  kwa kutekeleza mpango wa serikali  wa kujenga  zahanati kila kijiji sambamba na kuwa na mpango mkakati  wa kudhibiti  mlipuko wa malaria pindi unapotokea.
Ushauri huo ulitolewa na mkuu wa wilaya hiyo Lembris Kipuyo baada ya kutokea kwa mlipuko wa malaria wilayani humo  kipindi cha mwezi Mei na Juni mwaka huu na kusababisha vifo vya watoto wengi chini ya miaka mitano.
Kipuyo alisema kwa sasa katika wilaya hiyo maambukizi ya malaria ni asilimia 22 ambapo alidai kuwa kiwango hicho bado ni kikubwa na kuwataka watendaji na viongozi wote wa halmashauri hiyo kuhamasisha wananchi umuhimu wa kutumia vyandarua na kusafisha mazingira ili kuharibu mazalia ya mbu.
Alisema ni wajibu wa  halmashauri kuwasiliana na idara ya afya  ili iwapatie wataalam wa  afya wa kutosha yakiwemo madawa na vifaa tiba vya kutosha ili kukabiliana na tatizo la malaria katika wilaya hiyo.Chanzo:Tanzania Daima



 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa