Vijana kote nchini wametakiwa kubuni mbinu mbadala ya kujiajiri wenyewe
ili waweze kujikwamua katika umaskini, badala ya kutegemea ajira za serikali
pekee ambazo hazitoshelezi mahitaji yaliyopo.
Rai hiyo imetolewa na waziri ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen
Wassira wakati akikagua miradi ya mfuko wa maendeleo ya jamii nchini (TASAF)
katika wilaya ya Ngara.
Waziri Wassira alisema kuwa serikali haina uwezo wa kuajiri vijana wote
hapa nchini, inachokifanya ni kubuni namna wananchi watakavyotumia fursa
zilizopo kujiajiri kupitia sekta mbalimbali hasa ya kilimo.
Miongozi mwa miradi ya Tasaf aliyoitembelea ni pamoja na mradi wa kikundi
cha vijana 25 walioibua mradi wa kufuga mbuzi katika kijiji cha Ibuga
kata Kabanga, ambao wamejiinua kiuchumi kupitia mradi huo.
Akisoma risala katibu wa kikundi hicho Bahati Philmon, amesema kuwa
baada ya kuona kupata ajira za serikali kumeshindikana, wao kama vijana
walijiunga katika kikundi na kupatiwa fedha kutoka Tasaf kwa ajili ya kuanzisha
mradi huo wa ufugaji wa mbuzi, ulioibuliwa katika mkutano wa hadhara mwaka
2009.
Philmon amesema kuwa walipata shilingi milioni 11 kutoka Tasaf, na
kununua mbuzi 105, ambapo kila mmoja wao alipata mbuzi wanne, na kuwa
sasa wana jumla ya mbuzi 200, na kila mmoja amekwishafikisha mbuzi kumi.
Amesema kuwa jumla ya gharama ya mradi huo ni zaidi ya shilingi milioni
12.5 na kuwa mbali na fedha zilizotolewa na Tasaf, wananchi walichangia nguvu
zao zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5.
Amesema kuwa kutokana na ufugaji huo vijana kumi miongoni mwao
wameweza kuanzisha kilimo cha mazao mbalimbali katika shamba lenye ukubwa wa
ekari nane, ikiwamo mashamba ya migomba ya kisasa, kahawa na magimbi.
0 comments:
Post a Comment