HALMASHAURI ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera imeshauriwa kusogeza
huduma za afya kwa wananchi kwa kutekeleza mpango wa serikali wa
kujenga zahanati kila kijiji sambamba na kuwa na mpango mkakati wa
kudhibiti mlipuko wa malaria pindi unapotokea.
Ushauri huo ulitolewa na mkuu wa wilaya hiyo Lembris Kipuyo baada ya
kutokea kwa mlipuko wa malaria wilayani humo kipindi cha mwezi Mei na
Juni mwaka huu na kusababisha vifo vya watoto wengi chini ya miaka
mitano.
Kipuyo alisema kwa sasa katika wilaya hiyo maambukizi ya malaria ni
asilimia 22 ambapo alidai kuwa kiwango hicho bado ni kikubwa na
kuwataka watendaji na viongozi wote wa halmashauri hiyo kuhamasisha
wananchi umuhimu wa kutumia vyandarua na kusafisha mazingira ili
kuharibu mazalia ya mbu.
Alisema ni wajibu wa halmashauri kuwasiliana na idara ya afya ili
iwapatie wataalam wa afya wa kutosha yakiwemo madawa na vifaa tiba
vya kutosha ili kukabiliana na tatizo la malaria katika wilaya hiyo.Chanzo:Tanzania Daima
1 comments:
Mungu ibariki wilaya ya muleba ikue katika kupambana na magonjwa yanayotokea wilayani hapo
Post a Comment