Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo jana wakati wa makabidhiano ya mgodi wa Tulawaka kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), uliokuwa ukiendeshwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG).
Profesa Muhongo alisema kuna kampuni za nje na ndani zilizochukua vitalu vya madini na kuviacha kwa muda mrefu bila kuviendeleza na kuonya kuwa serikali itawanyang'anya na kuwapa wachimbaji wadogo.
Alisema taratibu za kisheria zimeanza kuchukuliwa ili watu wanaohodhi vitalu hivyo wanyang'anywe.
Aidha, alisema ABG na Stamico zimefikia makubaliano na mgodi wa Tulawaka kuanza uchimbaji wa madini na faida itakayopatikana hisa zitaanza kutolewa kwa Watanzania ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo.
Alisema kuanzia sasa migodi yote mipya inayoanzishwa ni lazima serikali iwe na hisa ambazo zitakuwa zikisimamiwa na Stamico.
Profesa Muhongo alisema kilio cha wachimbaji wadogo serikali imekisikia na kuwatengea maeneo kwa ajili ya uchimbaji wa madini.
Alisema pia imekuwa ikiwapatia vifaa pamoja na mikopo kutoka benki ya rasilimali (TIB) ili waweze kufanyakazi zao katika mazingira bora pamoja na vijana hao kupata ajira ikiwa ni sehemu ya kukuza uchumi wao.
Alisema katika kuwasaidia wachimbaji madini wadogo, maeneo yatakayonyang’anywa watapewa ili kuyaendeleza.
Alisema kuna idadi kubwa ya wachimbaji madini wadogo na tayari serikali inawatambua kwa kuwaunganisha katika vyama vyao kuanzia ngazi za chini hadi ya taifa ili Stamico iweze kuwapatia mafunzo dhidi ya kazi yao.
Alisema kumekuwa na tatizo la ulipaji wa kodi kwa wachimbaji hao “Kwa mfano Mirerani zipo kampuni kama 595 lakini kampuni 10 ndizo zinalipa kodi, ndio maana huwa nasema muuguzi kwa mwaka analipa kodi kubwa zaidi ya mchimbaji wa madini,” alisema.
Profesa Muhongo alisema mikataba iliyosainiwa ipo wazi haifanywi kwa kificho kama inavyodaiwa.
Aliongezea kuwa kwa wale wabunge ambao wanataka kuiona mikataba wanaweza kuipata kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Stamico, Rumisha Kimambo, alisema amefurahishwa na tukio hilo na kuyatekeleza yote waliyotakiwa kuyasimamia.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment