WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, amewataka madiwani wa Halmashari ya Muleba, mkoani Kagera,
kujenga soko la ndizi la kisasa kwa ajili ya mahitaji ya wananchi na
kupanua ajira kwa jamii.
Tibaijuka alitoa kauli hiyo juzi mjini Muleba, katika kikao cha
Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa
halmashauri ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, ambaye pia ni mbunge wa Muleba
Kusini (CCM), madiwani wa wilaya hiyo wanatakiwa kuweka mikakati ya
ujenzi wa soko hilo, kwa kuzingatia zao hilo ni muhimu kwa wananchi wa
Muleba na mkoa kwa ujumla.
“Naamini sisi madiwani wa Muleba tukijenga soko la ndizi itasaidia
kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi wetu. Maana itawarahisishia
wananchi kupata mahitaji eneo sahihi,” alisema.
Aidha, waziri aliwataka madiwani kusimamia ardhi ya wananchi kwa
umakini, na kuongeza kuwa diwani yeyote haruhusiwi kugawa ardhi bali
anatakiwa kusimamia kwa uangalifu rasilimali hiyo.
Diwani wa Kamachumu, Dunstan Mutagywa (CCM) aliunga mkono wazo la
waziri huyo na kusema soko la ndizi linatakiwa kujengwa kwenye eneo
ambalo wananchi watapata wateja.
Alisema endapo watajenga soko hilo sehemu nzuri ambayo wananchi
atafanya biashara, itasaidia katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu
karibu na jamii yenyewe.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment