Home »
» CHADEMA kususia Uchaguzi Mkuu 2015
CHADEMA kususia Uchaguzi Mkuu 2015
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa sharti ambalo kama
halitatekelezwa chama hicho hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wala hakitapiga
kura ya kupitisha rasimu ya katiba.
Sharti hilo lilitolewa mjini
Bukoba juzi na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, wakati akihutubia
katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo mikutano ya Operesheni ya
M4C Pamoja Daima uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa na kuhudhuriwa na
umati mkubwa wa watu.
Alisema chama hicho hakitashiriki uchaguzi
iwapo Serikali haitaboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura wakati huu
wa kuelekea uchaguzi mkuu na upigaji kura wa rasimu ya katiba.
Mbowe
alisema kwa jins hali inavyoonesha Serikali haioneshi nia ya kuboresha
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakati tunaelekea katika uchaguzi Mkuu
mwakani.
Alisema katika utafiti wao wamebaini kuwepo kwa vijana zaidi
ya milioni 5.3 ambao wamefikisha umri wa miaka 18 wanaotakiwa kushiriki
kupiga kura mwakani kuchagua viongozi wao.
Alisema katika hilo nchi
itasimama kwa vile kama tunahitaji mabadiliko hayawezi kufanyika bila
kuboresha daftari la kura. Kuhusu Rasimu ya Katiba, Mbowe aliapa mbele
ya mkutano huo kuwa mwaka huu ndio atang’olewa meno bungeni, kwani
hawatakuwa tayari kuburuzwa wakati wa Bunge la Katiba lijalo .
Alisema:“Suala
la katiba halina masihara ni maisha yenu, maisha ya watoto wenu, maisha
ya vizazi na vizazi, ni maisha ya taifa letu kila Mtanzania mwenye umri
wa miaka 18 wa kupiga kura lazima apige kura kukubali rasimu ya katiba
mpya, nasi Bungeni hatutakubali kuburuzwa. ”
Alisema kutokana na hali
hiyo, wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kujadili rasimu ya katiba
mpya. Alisema bunge lijalo la katiba wao wanaenda kujadili rasimu ya
Katiba Mpya ambayo tayari wameshaona .
“Tayari CCM wanampinga
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
kuhusiana na maoni ya wananchi kutaka serikali tatu, wakati wao haimo
kwenye sera yao, hapa kuna tatizo, kwani sisi tunaenda kujadili maoni
yawananchi wengi si kutetea sera za vyama vya siasa,” alisema.
Alisema
katiba si suala la kidini, sera za vyama vya siasa wala la kikabila ,
bali ni ya watu wote kwa ajili ya mustakabali wa maisha na taifa kwa
ujumla, hivyo hawaendi Dodoma kwa ajili ya kupinga Katiba hiyo, bali
kupitisha maoni ya wananchi wanavyotaka.
Pamoja na mambo mengi,
Mbowe aliwapongeza madiwani wa Manispaa hiyo bila kujali itikadi za
vyama kuungana kupinga ufujaji wa kodi za wananchi maskini wa Manispaa
uliokuwa ukifanyika ndani ya Manispaa hiyo.
“Mimi napenda kuwapongeza
Madiwani wa Manispaa ya Bukoba pamoja na Mbunge wao, Balozi Kagasheki,
ambao kwa pamoja walisimama kutetea maslahi ya wananchi wa Bukoba,
ukweli tuuseme na mnyonge mnyongeni na haki yake mpeni,” alisema.
Wakati
huo huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA),Tundu Lissu, amewaonya baadhi ya wanasiasa wanaotumia makanisa
na misikiti kuwashawishi wananchi ili wawachague kuwa viongozi katika
uchaguzi wa mwaka huu 2014/15.
Lissu aliyasema hayo wakati alipokuwa
akizungumza katika mikutano miwili iliyofanyika katika Kijiji cha
Ilongero na Mjini Singida juzi wakati akiwa kwenye siku ya kwanza ya
ziara ya ujumbe wa chama hicho ikiwa ni mwendelezo wa Operation M4C
Pamoja Daima itakayofanyika nchi nzima.
Alisema kuwa pamekuwa na
tabia ya baadhi ya wanasiasa Wakristo na Waislamu ambao hupita
makanisani na misikitini na kutoa fedha kwalengo la kujijengea umaarufu
jambo ambalo aliwataka wananchi wawe macho nao.
Alisema pamoja na
wanasiasa hao kujiwekea mazingira ya kushawishi wananchi ili wawachague,
Watanzania hawawakubali kwani hiyo inaweza kuleta tofauti za kidini.
“
Lazima tukumbuke mafundisho ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius
Nyerere ambayo yalisisitiza kuzingatia amani, upendo na mshikamano kwa
kuepuka kugawanywa na watu hao,” alisema.
Kuhusu Katiba Rasimu ya
Pili ya Katiba, alisema ni nzuri na kuzingatia vipengele vingi
vilivyotolewa maoni kurekebishwa kazi ambayo ilifanywa na CHADEMA pamoja
na wananchi wengine.
Alisema suala kubwa ni kuona kuwa Rasimu hiyo
haichakachuliwi kwa manufaa ya chama cha siasa au viongozi kwa ajili ya
maslahi yao.
“Tunasisitiza kuwepo kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga kura kuboreshwa ili wananchi wengi wakiwemo vijana waliofikia
umri huo na wale waliopoteza shahada zao waweze kushiriki katika zoezi
laku pigakura za maoni,”alisema.
Katika hatua zingine , Mwenyekiti
wa Baraza la Vijana wa CHADEMA Taifa, John Henje, alisema chama
hakitavumilia mtu yeyote anayetaka kukizamisha chama hicho. “Mtu yeyote
akileta
mchezo atafukuzwa, CHADEMA itaendelea kwani hakuna aliye
mkubwa au maarufu kuliko wanachama,” alisema. Alieleza kuwa chama hicho
kitaendelea kuwepo na kinachotakiwa sasa ni kuzungumzia mambo ya msingi
yanayokijenga na kukiendeleza.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment