MADIWANI wa Manispaa ya Bukoba, wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa
manispaa hiyo, kuitisha kikao ndani ya siku saba ili wampigie kura ya
kutokuwa na imani na aliyekuwa meya, Dk. Anatory Amani.
Hatua hiyo inakuja zikiwa ni siku chache tangu Dk. Amani kukanusha
kauli yake, akidai hajajiuzulu baada ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kumtia hatiani kuhusu miradi ya
maendeleo katika manispaa hiyo.
Kufuatia kauli hizo tatanishi za Amani, madiwani wametaka kiitishwe
kikao cha baraza ili wamng’oe wao wakisema kuwa ndio wenye mamlaka ya
mwisho ya kufanya hivyo kwa sababu ndio waliomuweka madarakani.
Madiwani hao walitoa msimamo huo juzi kwenye mkutano wa hadhara mjini
hapa uliohutubiwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki
pamoja na Diwani wa Kata ya Bakoba, Felician Bigambo (CUF).
Akizungumza katika mkutano huo, Bigambo alisema kuwa Januari 22 mwaka
huu, kupitia vyombo vya habari walimwona Dk. Amani akikanusha kwamba
hakuwahi kujiuzulu.
Alisema kuwa kwa sababu Amani anadai kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi,
Aggrey Mwanri aliyesoma taarifa ya Waziri Mkuu ya kumshauri ajiuzulu
hana mamlaka ya kumwondoa, basi watamng’oa wao.
“Sisi ndio wenye kauli ya mwisho katika sakata hili la kumuondoa
Amani, kwa hiyo tunamtaka mkurugenzi Shemwela Ambakise aiitishe kikao
cha baraza ili tumpigie kura ya kutokuwa na imani na Amani,” alisema.
Balozi Kagasheki alitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa kujiuzulu
kwake katika nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii akisema hatua hiyo
ilitokana na matatizo yaliyotokea katika Operesheni Tokomeza Ujangili
ambapo watu walijeruhiwa na wengine 10 kuuawa.
“Katika tukio kama hilo hakuna mtu ambaye angeweza kufurahishwa nalo.
Hivyo mimi kama kiongozi wa wizara hiyo niliamua kuwajibika kisiasa
kwa kujiuzulu,” alisema.
Balozi Kagasheki alisema operesheni hiyo si ya kwanza bali katika
miaka ya 1980 ilishafanyika Operesheni Uhai ambapo tembo 30,000 kati ya
60,000 katika pori la Selous waliuawa na majangili.
Aliongeza kuwa baada ya operesheni hiyo, idadi ya tembo ilipanda tena
na kufikia 50,000 katika miaka ya 2000, kwamba ujangili huo wa kutisha
umejitokeza tena kwa sasa hadi tembo kupungua kutoka 70,000 katika
pori hilo na kubaki 13,0000.
Kwa mujibu wa Kagasheki, hali hiyo ndiyo iliilazimu serikali
kuanzisha Operesheni Tokomeza Ujangili maalumu kwa nchi nzima ili
kunusuru wanyama hao wasitoweke kabisa.
Alitoa mfano wa Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuwa
naye alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati wafungwa
walipokufa kutokana na msongamano gerezani.
“Kujiuzulu ni jambo la kawaida wala haliniumizi nafsi yangu, labda
ningeumizwa pale ambapo ningetuhumiwa kwa ufisadi au nimeiba mali za
umma,” alisema.
Balozi Kagasheki alisema kuwa kwa sasa anawaomba wananchi wa Bukoba
kumuunga mkono katika suala zima la kuleta maendeleo yao kwani sasa
atakuwa na muda mrefu wa kuwa nao jimboni.
Pia alisema kuwa kutokana na ubadhirifu wa zaidi ya sh bilioni mbili
uliobainika katika ripoti ya CAG, Ludovick Utouh, yeye pamoja na
madiwani hawataishia hapo bali wataendelea kuishauri serikali
kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao wote akiwemo aliyekuwa meya.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment