DIWANI wa Kata ya Magata Kalutanga, Geofrey Ezekiel (CCM),
aliyekamatwa juzi na kuwekwa ndani kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya
Muleba, Limbris Kipuyo, jana alisomewa shtaka akiwa kitandani katika
Kituo cha Afya Kaigara.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka wilayani humo, zilisema
kuwa Ezekiel alisomewa shtaka hilo namba 11/ 2014 saa 4:30 asubuhi
akidaiwa kutishia kumjeruhi mkuu wa wilaya kwa kummwagia tindikali.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, mtoa taarifa wetu alisema kuwa
diwani huyo alisomewa shtaka hilo na Kaimu Hakimu wa Mahakama ya
wilaya aliyetambulika kwa jina moja la Ngonyani.
“Anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 6, mwaka huu. Lakini mpaka sasa
tunashughulikia dhamana maana alishutukizwa, hakuwa ameandaa
wadhamini. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Febuari 3, mwaka huu,” alisema.
Ezekiel alikamatwa juzi akidaiwa kutishia kumuua mkuu wa wilaya na
baada ya mahojiano na polisi alipekuliwa nyumbani kwake kisha
kushikiliwa kituoni hadi saa 12:00 jioni afya yake ilipobadilika ghafla
na kukimbizwa hospitali.
Chimbuko la mzozo huo ni baada ya diwani huyo kuandika barua ya
kumshtaki mkuu huyo kwa uongozi wa CCM Wilaya ya Muleba kwa kile
kilichoelezwa ni kutuhumiwa kula fedha za miradi.
Kipuyo anadaiwa kumtuhumu diwani huyo katika kikao cha Kamati ya
Siasa ya Wilaya cha CCM cha Januari 5, mwaka huu, kuwa anatumia wadhifa
wake wa uenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira kufuja
fedha za miradi akishirikiana na wahandisi wa halmashauri.
Pia alidai kuwa diwani huo anakwamisha miradi ya maendeleo kwa
makusudi, tuhuma ambazo alizirudia mbele ya kikao cha Kamati Kuu ya
Wilaya cha Januari 6, mwaka huu.
Baada ya Kipuyo kubaini ameshtakiwa kwa uongozi wa CCM, alitumia
mamlaka yake kuagiza polisi wamkamate diwani huyo na kumchukulia hatua
za kisheria, akidai ametishia kumuua kwa tindikali.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment