Home » » Minara ya simu sababu ya raia kunyanyaswa Kagera

Minara ya simu sababu ya raia kunyanyaswa Kagera

Hati ya uamuzi iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, R. Leonard inaelekeza kwamba katika makubaliano hayo, Mzee Tibahulila atachukua asilimia 75 ya mapato yatakayotokana na mnara huo, wakati Serikali ya Kijiji cha Musheshe itachukua asilimia 25


Kyerwa. Mapato yanayotokana na ujenzi wa minara ya simu, yanadaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kunyanyaswa kwa wakazi 41 wa Kijiji cha Murongo, wilayani Kyerwa katika Mkoa wa Kagera.
Usiku wa kuamkia Januari 22 mwaka huu, wananchi hao wengi wakiwa ni wa familia moja, walikamatwa na Maofisa wa Idara ya Uhamiaji ambao wanadaiwa kwamba waliwatesa kwa kuwapiga na kuwafungia kwa siku nne katika daraja linaloziunganisha Tanzania na Uganda kwa madai kwamba si raia wa Tanzania.
Miongoni mwa waliofanyiwa vitendo hivyo ni Mzee Elika Tibahulila (88), mke wake, Mole Tibahulila (58), watoto watatu wanaosoma shule ya msingi na watoto wadogo na wachanga saba, wakiwamo watatu ambao bado wananyonya.
Tibahulila alipigwa kiasi cha kupata jeraha kubwa chini ya goti la mguu wake wa kulia, na alitibiwa katika Hospitali ya Nyakahanga, Karagwe kisha akaruhusiwa.
Mzee huyo aliliambia gazeti hili: “Kwa kweli bado nina maumivu makali, natembea kwa tabu, nasaidiwa na fimbo (mkongojo)”.
Juzi Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna, Abbas Irovya alisema ofisi yake ilikuwa bado inafuatilia kwa karibu kuhusu taarifa za kupigwa kwa watu hao na kuahidi kutoa taarifa rasmi baada ya kufahamu ukweli wa suala hilo.
Chimbuko la mgogoro
Wakati watu hao 41wakidaiwa kuwa siyo Watanzania bali raia wa Uganda, gazeti hili limedokezwa kuwa chanzo ni mgogoro kuhusu ujenzi wa mnara wa simu wa Kampuni ya Vodacom ambao ulijengwa katika eneo la Mzee Tibahulila.
Mkazi wa Kitongoji cha Rwamatete, Kijiji cha Murongo, Antony Kakende alisema anamfahamu Mzee Tibahulila tangu 1959, ijapokuwa hakumbuki alikotokea. “Ni mzee wa siku nyingi,tumekuwa naye kwa miaka mingi...watoto wake ni watu wazima sasa,”alisema Kakende.
Mwingine ni Raymond Rwezaula ambaye alisema: “Tunafahamu kwamba huyu mzee wanamsumbua kwa sababu ya mali, maana viongozi wa kijiji walitaka kumnyang’anya ardhi ambako umejengwa mnara wa simu lakini akawashinda mahakamani.”
Naye Maria-Clavera Mansisi ambaye amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Murongo, alisema: “Tatizo ni mnara wa simu, maana sisi tumekuwa naye (Tibahulila) kwa miaka yote, hatujawahi kusikia kwamba siyo raia.”
Imebainika kuwa tangu 2009 mzee huyo amekuwa kwenye mvutano na Serikali ya Kijiji cha Murongo baada ya viongozi wake kusaini mkataba na Kampuni ya Vodacom ili kujenga mnara katika eneo ambalo alikuwa analimiliki.
Lakini wakati huohuo, vijiji vya Masheshe na Murongo viliingia katika mzozo vikiwania eneo la Mzee Tibahulila, ambalo Vodacom wamejenga mnara wa mawasiliano. Uongozi wa Murongo ulisaini mkataba na kampuni hiyo ya simu, jambo ambalo Uongozi wa Musheshe ulilipinga.
Mvutano huo ulizaa makubaliano baina ya pande hizo mbili yaliyofanyika chini ya usimamizi wa Uongozi wa Kata ya Murongo, Aprili 2, 2009 na kuandikishiana kwamba eneo ulipo mnara huo ni la Kijiji cha Musheshe, hivyo kubatilisha mkataba wa awali.
Kwa upande wake Mzee Tibahulila alipeleka suala hilo katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Bukoba, ambako hukumu ilitolewa Mei 5, 2010 kwamba pande husika zimalize nje ya mahakama.
Hati ya uamuzi iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, R. Leonard inaelekeza kwamba katika makubaliano hayo, Mzee Tibahulila atachukua asilimia 75 ya mapato yatakayotokana na mnara huo, wakati Serikali ya Kijiji cha Musheshe itachukua asilimia 25.
Hati hiyo ya Baraza la Ardhi na Nyumba pia imesainiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Musheshe, Thobias Justinian na Mzee Tibahulila ambaye baada ya kumaliza mgogoro huo, aliingia makubaliano mapya na Vodacom, Juni 2012 kwa malipo ya Sh450,000 kwa mwezi.
Mkataba huo ambao gazeti hili limeona nakala yake, ni wa miaka kumi (Juni 1, 2012 – Mei 31, 2022) na unaweza kufanyiwa mapitio baada ya miaka mitano.
Baada ya mgogoro huo kumalizika, Serikali ya Kijiji cha Murongo ilisaini mkataba na Kampuni ya Airtel kwa ajili ya kujenga mnara katika eneo hilohilo, hali ambayo ilisababisha Mzee Tibahulila kufungulia kesi nyingine katika Baraza husika.
Hadi Mzee Tibahulila alipokumbwa na msukosuko wa kutaka kufukuzwa kwenda Uganda kwa madai kwamba siyo raia, shauri hilo bado lipo mahakamani na limepangwa kusikilizwa Februari 14 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Murongo, Martin Mwasi alisema kufukuzwa kwa wananchi hao hakuna uhusiano wowote na mgogoro wa eneo ulikojengwa mnara.
“Sisi tulipewa maelekezo na uongozi wa juu kwamba tuwataje watu wote ambao siyo raia wa Tanzania hata kama walikuja kabla ya uhuru, na sisi tulipeleka majina maana tuna uhakika kwamba hao siyo raia,” alisema Mwasi na kuongeza:
“Kwa hiyo si kweli kwamba eti tumeasingizia kwa sababu ya mapato ya mnara wa simu, Uhamiaji ndiyo wenye sheria ya kuwaondoa.”
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa