WAKATI wanafunzi wengi wakikwama kujiunga kidato cha kwanza mwaka
huu kutokana na uhaba wa madarasa unaozikabiri baadhi ya halmashauri
nchini, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera imetamba kuwa na madarasa ya
ziada.
Mafanikio hayo yalibainishwa hivi karibuni na Ofisa Elimu Taaluma wa
wilaya hiyo, Mlashani Rwenyagira alipohojiwa na gazeti hili ofisini
kwake.
Alisema kuwa kwa sasa Wilaya ya Muleba inazo sekondari 35 za serikali
na nane za binafsi ambazo kwa pamoja zina wanafunzi 15,143 kabla ya
uteuzi wa kidato cha kwanza.
“Kwa mwaka huu, tulitarajia kupeleka sekondari asilimia 70 ya
wanafunzi kati ya 9,872 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka
jana.
“Kwa idadi hiyo ni kwamba tunahitaji vyumba 179 vya madarasa lakini
vilivyopo mpaka sasa ni 201, hivyo hatuna uhaba wa madarasa bali tuna
ziada,” alisema.
Kwa mujibu wa Rwenyegira kati ya idadi hiyo, shule mbili ni za kidato cha tano na sita ambazo ni Kishoju na Rutabo.
Kuhusu mahitaji ya walimu, alisema wana uhaba kwa mchepuo wa sayansi
kwani wengi wa wanaoletwa ni wale wanofundisha masomo ya sanaa.
Aliongeza kuwa licha ya kuwa na uhaba huo wa walimu wa sayansi,
mchakato wa ujenzi wa maabara unaendelea na sasa zimejengwa katika
shule 16 huku nyingine nne zikiwa kwenye ujenzi.
“Lakini pia ziko sekondari nne za Ibuga, Mayondwe, Kibanga na
Kanyeranyere zinatumia maabara inayotembea (mobile Laboratory).
Pia Rwenyagira aligusia fedha za maendeleo ya shule akisema kuwa
zinagawiwa kutegemeana na uwezo wa mfuko wa halmashauri na mahitaji ya
shule husika.
Alifafanua kuwa kwa mwaka juzi, mgawo ulikuwa sh milioni 7 na kwa
mwaka jana, shule 21 tayari zimepatiwa fedha hizo ambapo kila moja
alipata sh milioni 8.8.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, mwaka juzi bajeti ya elimu ya wilaya hiyo
ilikuwa sh bilioni 1.4 lakini walipatiwa sh milioni 700 pekee ambayo
iliunganishwa na ile wanayopewa na halmashauri kupitia vyanzo vyake.
Chanzo;Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment