MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe, amewapongeza madiwani wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM ), CHADEMA
na Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamisi Kagasheki kwa kusimama kidete
kutetea masilahi ya wananchi wa Bukoba kuhusu tuhuma za ufisadi dhidi
ya Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani.
Mbowe alisema hayo wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Bukoba
waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa
kumbukumbu wa Mayunga (UHURU PLATFOM ), hali iliyosababisha vijana wa
ulinzi wa chama hicho kuwazuia wananchi kuendelea kuingia ndani ya
uwanja huo kutokana na idadi kubwa ya watu.
Alisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), ilibaini kuwa ubadhirifu uliosimamiwa na meya ni zaidi ya sh
bilioni mbili, ambazo ni fedha za wananchi zinazotokana na kodi.
Alisema mtu yeyote akifanya jambo jema lazima apongezwe bila kujali anatoka chama gani hata kama si wa chama chako.
Hata hivyo alifafanua kuwa CCM ina mng’ang’ania Meya Amani wakati
kuna uchafu mwingi unaofanywa na viongozi wa juu, ukiwemo wizi wa
sh bilioni mbili, fedha zilizofujwa na Amani ni fedha chache
ukilinganisha na zinazoibwa na viongozi wa ngazi ya juu na
hawachukuliwi hatua yoyote.
Alisema sakata la Bukoba limewagawa watu katika misingi ya udini kwa
waumini wa dini anayoabudu meya huyo na kumtetea wakati amefanya
ubadhirifu wa fedha za umma, kitu ambacho si sawa na hata dini hazisemi
hivyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, alisema
viongozi wa serikali wanafanya ufisadi mkubwa lakini hawachukuliwi
hatua na matokeo yake wananchi wanaumizwa kwa kupandishiwa gharama za
maisha.
Mnyika alisema mawaziri waliojiuzulu kwa kashfa za kifisadi kwa
kusaini mikataba mibovu ikiwamo ya Richmond wanaendelea kutamba kwa
fedha za wananchi wa Tanzania.
Aidha, alisema kujiuzulu kwa Kagasheki katika nafasi ya uwaziri
haitoshi, kwani anapaswa kujiuzulu na ubunge kwa kushindwa kusimamia
wizara yake na wananchi waliomtuma kuwawakilisha bungeni kwa
kupeleka kero zao ili zitatuliwe.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment