Mkoa wa Kagera umetangaza oparesheni
maalum ya kutokomeza ugonjwa wa unyanjano unaoshambulia migomba kwa mwaka 2014,
kwa lengo la kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka huu ugonjwa huo uwe
umekwisha kabisa.
Katibu
tawala wa mkoa wa Kagera Nassor Mnambila amesema kuwa oparesheni hiyo iliyopewa
jina la “oparesheni tokomeza unyanjano”, itafanyika katika wilaya zote za mkoa
huo, kuanzia ngazi za vitongoji.
Mnambila
amesema kuwa kuanzia Januari hadi Juni ni kipindi cha wananchi kung’oa na
kuchoma moto migomba iliyoathirika kwa hiari na kuwa baada ya hapo kuanzia
mwezi Julai kikosi kazi kitavamia mashamba yote yaliyoathirika na kung’oa
migomba hiyo kwa nguvu.
Amesema
kuwa wananchi na watendaji watakaobainika kukwamisha zoezi hilo watashtakiwa
kwa sheria ndogo zilizotungwa na halmashauri kwa ajili ya kupambana na ugonjwa
huo na sheria ya kilimo ya kudhibiti magonjwa.
Amesema
wana mpango wa kutoa elimu kwa maafisa ugani ili waujue vizuri ugonjwa huo,
ndipo wataweza kushiriki kikamilifu, na kuwa pia wananchi wataendelea
kuelimishwa kuhusu njia bora za kupambana na ugonjwa huo kwa kushirikiana na
kituo cha utafiti wa kilimo cha Maruku.
Akizungumzia
oparesheni hiyo mkuu wa mkoa wa Kagera kanali mstaafu Fabian Massawe amesema
kuwa tayari halmashauri zote zimekwishaandaa sheria ndogo kwa ajili ya
kudhibiti ugonjwa huo.
0 comments:
Post a Comment