Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, akiwa mkoani Kagera, alisema yuko tayari kuwa wa kwanza kufungwa kwa kosa la kudai katiba mpya itumike ikiwa serikali italazimisha kuendelea kutumia katiba ya zamani.
Mbowe alisema hayo jana wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa wilaya ya Ngara.
Alisema wananchi wengi wamependekeza kuwapo kwa Muungano wa wa serikali tatu katika rasimu ya katiba mpya, lakini zipo njama zinayofanywa kuchakachua maamuzi ya wananchi kuhusu mfumo huo wa Muungano.
Alisema kama maamuzi hayo ya wananchi walio wengi yatachakachuliwa, yuko tayari kuzunguka nchi nzima kuwahamasisha wananchi waikatae katiba hiyo.
Aliongeza kuwa ikiwa wananchi wataikataa katiba hiyo, pia hawatakuwa tayari kuendelea kutumia katiba ya zamani inayotumika hivi sasa kama serikali ilivyokwishasema.
“Nitakuwa wa kwanza kufungwa endapo katiba inayoandaliwa sasa itachakachuliwa na baadhi ya watu ambao hawataki shirikisho la serikali tatu kwa kuwa nitazunguka nchi nzima kuhamasisha wananchi kuikataa na baada ya kuikataa, pia hatutakuwa tayari kurudia ile ya zamani,” alisema Mbowe na Kuongeza:
“Haiwezekani Watanzania walio wengi wakatoa maoni kuhusu katiba wanayoitaka wao halafu wengine wakaichakachua eti tu kwa sababu ya maslahi yao binafsi ya kutaka kujitengenezea mazingira ya ulaji. Katiba ni uhai wa Watanzania siyo ya chama chochote cha siasa au ya mtu fulani, mbona Zanzibar wenyewe wametengeneza katiba yao kwa nini na sisi tusingeneze Tanganyika.”
Aliongeza kuwa haiwezekani kutumia muda mwingi na gharama kubwa ya fedha kuandaa katiba hiyo, halafu watu wengine wakaichakachua, na kwamba hata kama rasimu ya katiba mpya itakataliwa haiwezekani kuendelea
ya sasa na kwamba itailazimisha serikali kuangalia utaratibu mwingine wa kuhakikisha Katiba mpya inapatikana.
“Wazo la kurudi katika katiba ya zamani haipo kabisa, kama serikali ya CCM inajidanganya kwamba watachakachua katiba inayoandaliwa sasa halafu tukarudi kutumia ile ya zamani hiyo haipo na itawagharimu,” alisisitiza.
Kadhalika, Mbowe alisema atazunguka nchi nzima kuwahamasisha watanzania kususia zoezi la upigaji kura ya maoni ya katiba endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itashindwa kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.
Alisema kupiga kura ni haki ya msingi ya Watanzania, na kwamba mpaka sasa zaidi ya Watanzania 5,300,000 hawana uwezo wa kupiga kura kwa sababu hawana shahada ya kupigia kura.
Akizungumza mjini Bukoba jana jioni, Mbowe alisema hivi sasa ni wakati wa Chadema kuwang’oa madiwani wa CCM waliohusika katika ufisadi uliobainishwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
MNYIKA: MJADALA WA GESI BADO
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, kutofunga mjadala wa gesi ili kujadiliwa na wananchi kwanza.
Alisema hayo wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Kigoma mjini baada ya wakazi hao kutofahamu kama mkoa wao una gesi wakati Serikali ilishatangaza kunadi leseni za vitalu.
“Wakati Sera, Katiba na Sheria imeweka msingi wa kuhakikisha rasilimali za Taifa zinalindwa na wananchi hususani wazawa wana nufaika, wananchi hawafahamu kama wana gesi. Hivyo kama Rais na Waziri Muhongo hawatasitisha, nitachukua hatua za kisheria kuhakikisha mjadala huu unarudishwa kwa wananchi,” alisema Mnyika.
Aidha Chama hicho kimetangaza kuwa hakitakubali uchaguzi wa vijiji na mitaa 2014 na uchaguzi mkuu 2015 ufanyike huku kukiwa na mfumo wa usiyo kuwa huru wa uchaguzi.
Mnyika alisema wanapinga rasimu kutoa mwanya kwa wakurugenzi, watendaji na wateule wa Serikali ambao pia wanahusika na kashfa mbalimbali kusimamia uchaguzi badala ya watumishi huru wa Tume ya Uchaguzi, kwani ni vigumu kusimamia uchaguzi huru na wa haki.
“Pamoja na kushinikisha ushindi wa nguvu ya umma kuna haja ya kuhakikisha kwenye mchakato wa katiba mpya kuna kuwa na tume huru ya uchaguzi, pamoja na kuunga mkono rasimu ya katiba juu ya muundo wa Muungano wa Shirikisho Serikali tatu, lakini ukweli ni kwamba bado haijaweka mfumo huru wa uchaguzi,” alisema Mnyika.
Akizungumza mjini Bukoba jana jioni, aliwataka Watanzania washikamane kupinga ongezeko la gharama za umeme ambazo ongezeko lake limechangiwa na baadhi ya viongozi wa serikali kusaini mikataba mibofu na kuitaja ya IPTL, Richmond na Songas.
LEMA ALIA NA ZITTO
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema kuwa juzi walipata mapokezi makubwa mjini Kigoma na kwamba kila mtu akiwa katika chama afanye kazi ya kukijenga badala ya kukibomoa.
Alisema licha ya kuwapo na madai kuwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, ana umaarufu mkubwa mkoani humo, jambo hilo halina ukweli.
Alidai mwaka 2010 walitegemea kupata ushindi katika Jimbo la Mpanda, lakini Zitto aliandika barua akieleza kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, awe mgombea pekee.
Alisema baada ya chama kupata taaarifa na kutaka kumwajibisha Zitto, Mwenyekiti Mbowe, aliingilia kati na kusitisha uamuzi huo.
Alisema kutokana na waraka walioukamata aliodai uliokuwa na malengo ya kukisambaratisha chama, waliona hawana sababu za kuendelea na Zitto na kumvua nyadhifa zake na kwamba kitendo cha kuweka pingamizi mahakamani asijadiliwe kinamfanya awe mbunge wa Mahakama.
Alisema mwaka 2000 walikuwapo madiwani 11 katika jimbo la Zitto la Kigoma Kaskazini, lakini mwaka 2005 alipogombea walipungua na kubakia sita na kwamba mwaka 2010 walipungua zaidi na kubakia wawili, hivyo hakuna ukweli kuwa amekijenga chama katika jimbo lake.
Umati mkubwa wa wakazi wa Manispaa ya Bukoba jana walimiminika kwa wingi katika uwanja wa Uhuru kuwasikiliza Viongozi wa Chadema waliohutubia mkutano wa hadhara.
Kabla ya mkutano huo, yalifanyika maandamano makubwa yaliyokuwa yakiongozwa na vijana waendesha pikipiki.
LISSU ASISITIZA UADILIFU
Akihutubia mkutano wa hadhara jana jioni katika viwanja vya Shule ya Msingi Ukombozi mjini Singida, Lissu aliwataka Watanzania wasikubali kuchonganishwa kwa kutumia misingi ya udini kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CCM wenye uchu wa madaraka.
Alisema wananchi waangalie kiongozi ambaye ni mwadilifu na anayeichukia rushwa na kwamba wamchague kiongozi mwadilifu ambaye atatoka Chadema.
Alisema hakuna mtu mashuhuri chadema bali wanachama na kuongeza kuwa Chadema wakichukua nchi hawatakuwa waoga wa kufanya maamuzi magumu na kuwa watafukuza waziri yayote anayekiuka kanuni na taratibu za nchi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment