Walioingiza mifugo ranchi ya Missenyi watozwa faini

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi , Festo Kiswaga

SERIKALI wilayani Missenyi mkoani Kagera imetoa siku 14 kwa wamiliki wa ng’ombe 240 waliokamatwa ndani ya ranchi ya Missenyi, Machi mwaka huu, kulipa faini na kukomboa mifugo yao, vinginevyo Serikali itaiuza kwa mnada.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo jana , Festo Kiswaga alipofanya mkutano na wafugaji ambao pia ni wamiliki wa mifugo hiyo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri mjini hapa .
Agizo hilo la Kiswaga amelitoa kutokana na mifugo hiyo kuendelea kushikiliwa kwa muda mrefu toka Machi mwaka huu huku wamiliki wake wakiweka msimamo wa kupinga utaratibu wa kuwachukua kwa kulipa faini.
“Taarifa niliyo nayo ni kwamba Machi mwaka huu, ng’ombe hao waliingia kinyemela katika Ranchi ya Missenyi huku baadhi yao wakidaiwa kutoka nchi jirani , kitu ambacho ni kinyume na sheria na hivyo kushikiliwa katika kitalu namba kumi na moja hadi leo hii. Sasa basi Serikali haiwezi kuvumilia kuendelea kuwalisha mifugo hao kwa kuwa mnafanya makusudi na kugoma tutawauza mapato yaingie serikalini endapo muda niliotoa utaisha bila kufuata agizo la serikali,” aliagiza Kiswaga.
Katika kikao hicho, wafugaji hao walidai hali hiyo haitakoma endapo serikali haitawapatia maeneo mbadala ya kufugia kutokana na idadi kubwa ya mifugo waliyonayo ukilinganisha na maeneo waliyotengewa kwa ajili ya malisho.
Mmoja wa wafugaji hao, Daniel Kwigizile, alisema kuwa wamepokea tamko hilo la Serikali kwa shingo upande na wanaishauri serikali kutenga maeneo makubwa zaidi kwa ajili ya malisho la sivyo hali hiyo haitakoma.
Chanzo Gazeti la Habari leo
 

RC: Tengeni maeneo ya vijana, wanawake

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salim Kijuu
VIONGOZI wa mitaa, vijiji na kata na wataalamu wa Serikali, wametakiwa kutenga maeneo ya vikundi vya uzalishaji vya vijana na wanawake ili wajikwamue katika umasikini wa kipato.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salim Kijuu wilayani Karagwe hivi karibuni alipofika kujitambulisha.
Alisema watendaji, wananchi, wadau wakiwamo viongozi wa dini, watoe ushauri na maoni kujua changamoto zinazowakabili ili Serikali izifanyie kazi kwa haraka.
“Katika suala zima la ajira kwa vijana na uwezeshaji kiuchumi, naagiza mamlaka husika ambao ni madiwani, serikali za vijiji na mitaa, wataalamu na wananchi katika ngazi za vijijini, mitaa na kata kutenga maeneo. Maeneo hayo ni kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana ili waweze kuanzisha miradi ya kilimo, ufugaji, viwanda vidogo na biashara, hii itasaidia waweze kuzalisha na kuondokana na umasikini wa kipato,” alisema Kijuu.
Alisema hiyo ni hatua za awali katika maandalizi ya mpango wa Serikali wa kutoa fedha za kuwezesha wanachi kiuchumi na kuwekeza katika miradi ya kuzalisha mali.
“Vijana washauriwe, wajengwe katika misingi ya kujitegemea na kuwatengenezea mbinu zitakazowawezesha kuibua miradi kama vile kilimo cha mboga ambapo watavuna kwa muda mfupi pia watafutiwe masoko, kuanzisha viwanda vidogo ambapo wakikusanyika kwa pamoja na kila mtu akaleta wazo lake na ujuzi wake wakaungana wanaweza kutengeneza kitu kizuri na kutokea hapo wakajikuta wanaingia katika viwanda vikubwa," alisema Kijuu.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
 

Watu 7 kortini kwa uchomaji makanisa

Imeandikwa na Angela Sebastian, Bukoba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi
POLISI mkoani Kagera imekamata watu saba na kuwafikisha mahakamani wakihusishwa na uchomaji moto makanisa kikiwemo Kigango cha Nyarwele Parokia ya Kimiza, Jimbo Katoliki la Kayanga wilayani Karagwe.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Augustine Ollomi alibainisha hayo jana ofisini kwake mjini Bukoba wakati akizungumza na gazeti hili ambalo lililenga kutaka kujua chanzo cha uchomaji wa makanisa, pia kama kuna waliokamatwa na wamechukuliwa hatua gani mpaka sasa.

Alisema tangu mwaka jana, zaidi ya makanisa 10 yamechomwa katika mkoa huo na Polisi waliunda kikosi kazi cha kusaka wanaojihusisha na vitendo, hivyo mpaka sasa watu saba wamefikishwa mahakamani huku jeshi hilo likiendelea kuwasaka wahusika wengine.

“Tumewakamata watu saba na kuwafikisha mahakamani. Uchunguzi wa kina unaendelea ili tuweze kubaini chanzo ni nini na wanatumwa na nani kuchoma nyumba za ibada na baada ya kupata chanzo ndipo tutatoa taarifa kamili. Tunaendelea na uchunguzi wetu,” alisema Kamanda Ollomi.

Alisema katika matukio ya hivi karibuni, makanisa mawili yalichomwa moto Januari mwaka huu katika kata ya Kihanga wilayani Karagwe yamechomwa ingawa kanisa moja ndilo liliathirika sana.

Alitaja makanisa hayo kuwa ni Tanzania Assemblies of God (TAG) na Pentekoste Assemblies of God (PAG) pia kuamkia Mei 2, mwaka huu watu wasiojulikana walichoma kigango cha Kanisa Katoliki wilayani humo na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 52.1.

Chanzo Gazeti la Habari leo
 
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa