POLISI mkoani Kagera imekamata watu saba na kuwafikisha mahakamani
wakihusishwa na uchomaji moto makanisa kikiwemo Kigango cha Nyarwele
Parokia ya Kimiza, Jimbo Katoliki la Kayanga wilayani Karagwe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Augustine Ollomi alibainisha hayo jana
ofisini kwake mjini Bukoba wakati akizungumza na gazeti hili ambalo
lililenga kutaka kujua chanzo cha uchomaji wa makanisa, pia kama kuna
waliokamatwa na wamechukuliwa hatua gani mpaka sasa.
Alisema tangu mwaka jana, zaidi ya makanisa 10 yamechomwa katika mkoa
huo na Polisi waliunda kikosi kazi cha kusaka wanaojihusisha na
vitendo, hivyo mpaka sasa watu saba wamefikishwa mahakamani huku jeshi
hilo likiendelea kuwasaka wahusika wengine.
“Tumewakamata watu saba na kuwafikisha mahakamani. Uchunguzi wa kina
unaendelea ili tuweze kubaini chanzo ni nini na wanatumwa na nani
kuchoma nyumba za ibada na baada ya kupata chanzo ndipo tutatoa taarifa
kamili. Tunaendelea na uchunguzi wetu,” alisema Kamanda Ollomi.
Alisema katika matukio ya hivi karibuni, makanisa mawili yalichomwa
moto Januari mwaka huu katika kata ya Kihanga wilayani Karagwe
yamechomwa ingawa kanisa moja ndilo liliathirika sana.
Alitaja makanisa hayo kuwa ni Tanzania Assemblies of God (TAG) na
Pentekoste Assemblies of God (PAG) pia kuamkia Mei 2, mwaka huu watu
wasiojulikana walichoma kigango cha Kanisa Katoliki wilayani humo na
kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 52.1.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment