Home » » Walioingiza mifugo ranchi ya Missenyi watozwa faini

Walioingiza mifugo ranchi ya Missenyi watozwa faini

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi , Festo Kiswaga

SERIKALI wilayani Missenyi mkoani Kagera imetoa siku 14 kwa wamiliki wa ng’ombe 240 waliokamatwa ndani ya ranchi ya Missenyi, Machi mwaka huu, kulipa faini na kukomboa mifugo yao, vinginevyo Serikali itaiuza kwa mnada.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo jana , Festo Kiswaga alipofanya mkutano na wafugaji ambao pia ni wamiliki wa mifugo hiyo katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri mjini hapa .
Agizo hilo la Kiswaga amelitoa kutokana na mifugo hiyo kuendelea kushikiliwa kwa muda mrefu toka Machi mwaka huu huku wamiliki wake wakiweka msimamo wa kupinga utaratibu wa kuwachukua kwa kulipa faini.
“Taarifa niliyo nayo ni kwamba Machi mwaka huu, ng’ombe hao waliingia kinyemela katika Ranchi ya Missenyi huku baadhi yao wakidaiwa kutoka nchi jirani , kitu ambacho ni kinyume na sheria na hivyo kushikiliwa katika kitalu namba kumi na moja hadi leo hii. Sasa basi Serikali haiwezi kuvumilia kuendelea kuwalisha mifugo hao kwa kuwa mnafanya makusudi na kugoma tutawauza mapato yaingie serikalini endapo muda niliotoa utaisha bila kufuata agizo la serikali,” aliagiza Kiswaga.
Katika kikao hicho, wafugaji hao walidai hali hiyo haitakoma endapo serikali haitawapatia maeneo mbadala ya kufugia kutokana na idadi kubwa ya mifugo waliyonayo ukilinganisha na maeneo waliyotengewa kwa ajili ya malisho.
Mmoja wa wafugaji hao, Daniel Kwigizile, alisema kuwa wamepokea tamko hilo la Serikali kwa shingo upande na wanaishauri serikali kutenga maeneo makubwa zaidi kwa ajili ya malisho la sivyo hali hiyo haitakoma.
Chanzo Gazeti la Habari leo
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa