VIONGOZI wa mitaa, vijiji na kata na wataalamu wa Serikali,
wametakiwa kutenga maeneo ya vikundi vya uzalishaji vya vijana na
wanawake ili wajikwamue katika umasikini wa kipato.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salim Kijuu wilayani Karagwe hivi karibuni alipofika kujitambulisha.
Alisema watendaji, wananchi, wadau wakiwamo viongozi wa dini, watoe
ushauri na maoni kujua changamoto zinazowakabili ili Serikali izifanyie
kazi kwa haraka.
“Katika suala zima la ajira kwa vijana na uwezeshaji kiuchumi,
naagiza mamlaka husika ambao ni madiwani, serikali za vijiji na mitaa,
wataalamu na wananchi katika ngazi za vijijini, mitaa na kata kutenga
maeneo. Maeneo hayo ni kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana ili
waweze kuanzisha miradi ya kilimo, ufugaji, viwanda vidogo na biashara,
hii itasaidia waweze kuzalisha na kuondokana na umasikini wa kipato,”
alisema Kijuu.
Alisema hiyo ni hatua za awali katika maandalizi ya mpango wa
Serikali wa kutoa fedha za kuwezesha wanachi kiuchumi na kuwekeza katika
miradi ya kuzalisha mali.
“Vijana washauriwe, wajengwe katika misingi ya kujitegemea na
kuwatengenezea mbinu zitakazowawezesha kuibua miradi kama vile kilimo
cha mboga ambapo watavuna kwa muda mfupi pia watafutiwe masoko,
kuanzisha viwanda vidogo ambapo wakikusanyika kwa pamoja na kila mtu
akaleta wazo lake na ujuzi wake wakaungana wanaweza kutengeneza kitu
kizuri na kutokea hapo wakajikuta wanaingia katika viwanda vikubwa,"
alisema Kijuu.
Chanzo Gazeti la Habari Leo
0 comments:
Post a Comment