MFAHAMU MAMA SHUJAA WA CHAKULA KUTOKA MKOA WA KAGERA ANAYETARAJIA KUINGIA KIJIJI CHA MAISHA PLUS SIKU YA JUMAPILI WIKI HII!

GRACE G.D MAHUMBUKA (46) mkazi wa Karagwe Kagera nambari yake ya ushiriki ni MS 08, ni mkulima wa shamba la ekari 18 na na mfugaji wa ng’ombe, kondoo na mbuzi.


ANADHANI YEYE NI MFANO WA KUIGWA: Kwa sababu anawahamasisha wana kijiji kutumia vyema mvua za kwanza na kupanda miti kwa ajili ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kutunza mazingira."Nina shamba lenye ukubwa wa ekari 18. Kwa mwaka ninavuna mazao gunia 35"

MAISHA PLUS /MAMA SHUJAA WA CHAKULA

HARAMBEE YABUGADEA YAKUSANYA MIL.8/-

SHILINGI milioni 8.8 zimekusanywa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Buganguzi, wilayani Muleba iliyoratibiwa na Umoja wa Maendeleo ya Buganguzi (Bugadea).
Akizungumza katika harambee hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa umoja huo ulioasisiwa na wakazi wa Kata ya Buganguzi waishio Dar es Salaam, Rodrick Lutembeka, alisema kiasi hicho kilitokana na michango ya wananchi, pia ofisi  ya mkuu wa mkoa imechangia  sh milioni 1.8 na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba imeahidi kuchangia sh milioni 30.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye harambee hiyo iliyofanyika kwenye makao makuu ya kata hiyo, amehimiza wakazi mkoani humo kuepuka tabia ya kusubiri misaada na badala yake  wachangie miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Alisema juhudi za wananchi lazima zionekane kwanza katika miradi yao kabla ya kuomba misaada.
Alisema ni aibu kuomba misaada kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali hata kwa vitu ambavyo viko ndani ya uwezo wa wananchi.
Massawe alisema miradi mingi ya maendeleo katika Wilaya  ya Muleba ukiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, haikutekelezwa kwa kasi ya kuridhisha kwa kile alichodai ni wananchi kurubuniwa na kushindwa kuchangia nguvu zao.
Katika kuhamasisha ujenzi wa Kituo cha Afya Buganguzi kinachokadiriwa kugharimu zaidi ya sh milioni 600,  Mkuu wa Mkoa ameshauri kila kaya kuchangia sh 20,000 au vitu vyenye thamani hiyo, ili kufikia lengo la kata hiyo kuwa na huduma hiyo.
Alipongeza wakazi wa Buganguzi walioko nje ya mkoa  chini ya mwavuli wa Bugadea kwa kuwa na wazo la kukumbuka nyumbani na kushiriki kuchangia maendeleo. Kata ya Buganguzi iliyo katika Tarafa ya Nshamba, ina vijiji vya Buhanga, Bushemba, Katare na Kashozi.
Mwenyekiti wa Bugadea, Lutembeka, alihimiza wakazi wa kata hiyo kuunganisha nguvu katika ujenzi wa kituo hicho na miradi mingine ya maendeleo.
Alisema hakuna sababu  ya kushindwa kufanya hivyo kwa kuwa fursa zilizopo,  ikiwemo ardhi na rasilimali  vinatosheleza kutekeleza ujenzi huo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Rembris Kipuyo, alisema serikali itaendelea kushirikiana na wananchi wa kata hiyo hadi kukamilika kwa kituo hicho.
Diwani wa Buganguzi, Onesmo Yegira alipongeza uamuzi wa Bugadea kuandaa tamasha hilo la maendeleo lililopambwa na burudani pamoja na michezo mbalimbali ikiwa ni njia ya kukutanisha wakazi kuchangia maendeleo. 
Chanzo:Tanzania Daima

WAATHIRIKA WA MAFURIKO WADAI KUTELEKEZWA

BAADHI ya wakazi wa Kijiji cha Bulembo ambao walikumbwa na maafa ya nyumba zao kuanguka na nyingine kuezuliwa na mazao yao kuharibiwa na mvua, wamedai kutelekezwa na serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema walipatwa na maafa hayo Machi 20, mwaka huu, lakini hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kimekaa kimya wakati hawana chakula wala mahala salama pa kuishi na kwamba baadhi yao wanalala katika magofu.
Pia wameulalamikia uongozi wa kijiji hicho kwa kugawa misaada kwa upendeleo.
Walisema misaada inayotolewa wanagawiwa hata ambao hawakuathiriwa na mvua hizo huku walioathiriwa wakiachwa.
Mmoja wa wananchi hao, Elipidius Christopher, mkazi wa kitongoji cha Bulembo, alisema nyumba yake ilianguka, mazao yake yote ikiwamo migomba, mibuni, magimbi na mihogo yameharibika, lakini amekuwa akibaguliwa wakati wenzake wanapopatiwa misaada.
“Sikupewa hema, nalala kwenye gofu nikiwa na watoto wangu, viongozi wangu wana taarifa kuwa nami ni mmoja wa watu walioathirika, lakini sifahamu kwa nini nabaguliwa,” alisema Christopher.
Pia walilalamikia uongozi wa kijiji hicho kupokea misaada ya vyakula na kuifungia stoo wakati wao hana chakula.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bulembo, Longinus Clement, alikiri baadhi ya wananchi wake kutopatiwa misaada inayopelekwa kijijini hapo kutokana na kutoorodheshwa katika orodha ya awali ambayo inatumika kugawa misaada hiyo.
“Wakati wanapita kuorodhesha wananchi walioathirika katika kitongoji changu, mimi nilipewa kazi ya kuhesabu miti iliyoangushwa na upepo, niliporejea nilikuta viongozi wenzangu wamekwishaorodhesha waathirika, nikagundua kuwa kuna ambao walibaki bila kuorodheshwa,” alisema.
Clement alisema baada ya kugundua hilo aliwasiliana na viongozi wenzake lakini cha kushangaza walikataa kuwapatia misaada wakidai wanagawa kwa kutumia orodha ya awali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulembo, Trazias Kyabona, alisema wanaolalamika kuwa misaada inayotolewa imefungiwa stoo ni majungu, kwani kinachofanyika wanakusanya misaada midogomidogo na kuiweka pamoja  na baadaye kuigawa kwa wananchi.
Kyabona pia alikana misaada hiyo kuwagawia watu ambao hawajaathirika na kuwa misaada hiyo wanapewa kulingana na walivyoorodheshwa na kamati ya maafa ya kijiji kwa kushirikiana na kamati ya maafa ya wilaya.
 Chanzo;Tanzania Daima 

WAATHIRIKA WA MAFURIKO WADAI KUTELEKEZWA

BAADHI ya wakazi wa Kijiji cha Bulembo ambao walikumbwa na maafa ya nyumba zao kuanguka na nyingine kuezuliwa na mazao yao kuharibiwa na mvua, wamedai kutelekezwa na serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema walipatwa na maafa hayo Machi 20, mwaka huu, lakini hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kimekaa kimya wakati hawana chakula wala mahala salama pa kuishi na kwamba baadhi yao wanalala katika magofu.
Pia wameulalamikia uongozi wa kijiji hicho kwa kugawa misaada kwa upendeleo.
Walisema misaada inayotolewa wanagawiwa hata ambao hawakuathiriwa na mvua hizo huku walioathiriwa wakiachwa.
Mmoja wa wananchi hao, Elipidius Christopher, mkazi wa kitongoji cha Bulembo, alisema nyumba yake ilianguka, mazao yake yote ikiwamo migomba, mibuni, magimbi na mihogo yameharibika, lakini amekuwa akibaguliwa wakati wenzake wanapopatiwa misaada.
“Sikupewa hema, nalala kwenye gofu nikiwa na watoto wangu, viongozi wangu wana taarifa kuwa nami ni mmoja wa watu walioathirika, lakini sifahamu kwa nini nabaguliwa,” alisema Christopher.
Pia walilalamikia uongozi wa kijiji hicho kupokea misaada ya vyakula na kuifungia stoo wakati wao hana chakula.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bulembo, Longinus Clement, alikiri baadhi ya wananchi wake kutopatiwa misaada inayopelekwa kijijini hapo kutokana na kutoorodheshwa katika orodha ya awali ambayo inatumika kugawa misaada hiyo.
“Wakati wanapita kuorodhesha wananchi walioathirika katika kitongoji changu, mimi nilipewa kazi ya kuhesabu miti iliyoangushwa na upepo, niliporejea nilikuta viongozi wenzangu wamekwishaorodhesha waathirika, nikagundua kuwa kuna ambao walibaki bila kuorodheshwa,” alisema.
Clement alisema baada ya kugundua hilo aliwasiliana na viongozi wenzake lakini cha kushangaza walikataa kuwapatia misaada wakidai wanagawa kwa kutumia orodha ya awali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulembo, Trazias Kyabona, alisema wanaolalamika kuwa misaada inayotolewa imefungiwa stoo ni majungu, kwani kinachofanyika wanakusanya misaada midogomidogo na kuiweka pamoja  na baadaye kuigawa kwa wananchi.
Kyabona pia alikana misaada hiyo kuwagawia watu ambao hawajaathirika na kuwa misaada hiyo wanapewa kulingana na walivyoorodheshwa na kamati ya maafa ya kijiji kwa kushirikiana na kamati ya maafa ya wilaya.
Chanzo:Tanzania Daima

ASKOFU AUNGANA NA KAKOBE KUTAKA TANGANYIKA

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe
 
Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Severin NiweMugizi ameungana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe kupigia debe Serikali ya Tanganyika.
Akizungumza katika mahojiano ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita, NiweMugizi alitaka Serikali kutobeza maoni ya wananchi wanaotaka Serikali ya Tanganyika kwa kuwa muungano uliopo unaunganisha nchi mbili.
Kauli hiyo inarandana na ile iliyotolewa na Askofu Kakobe juzi wakati akitoa mahubiri ya Pasaka, aliposema anaungana na Watanzania wanaodai Serikali ya Tanganyika na kuahidi kuwapa ari na shauku ya kuhakikisha inapatikana.
NiweMugizi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), alisema ukosefu wa elimu ya uraia kwa Watanzania wasomi na wananchi, ndiyo kikwazo cha kutetea uzalendo kwenye muundo wa Muungano.
Alisema katika miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kumeibuka mambo mengi ya mpasuko wa umoja uliokusudiwa na waasisi wa kufanya mataifa mawili kuwa moja.
Alisema ili kuhakikisha Tanganyika inapatikana, lazima Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikubali kuwa shirikisho, kwa kila nchi kupoteza baadhi ya mamlaka na masilahi ya taifa.
Pia, alisema katika kuanzisha Taifa la Tanzania, mamlaka zilizokuwapo Umoja wa Mataifa (UN), ziliondolewa kwa nchi ya Tanganyika na Zanzibar na kuunda kiti kimoja cha Tanzania.
“Zanzibar kutangaza kuwa ni nchi ndani ya nchi nyingine kwa mamlaka kamili ya Serikali na kutaka kujiunga na taasisi za kimataifa, inaonyesha kuwa Tanzania imemeguka kipande katika Muungano,” alisema Askofu NiweMugizi.
Alisema Muungano wa sasa una nyufa nyingi zaidi ya zile alizoona Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine.
Alisema miongoni mwa mambo yanayosukuma wananchi kudai Tanganyika ni kupewa elimu ya uraia kufahamu vyema historia ya Muungano na nyufa zilizopo, hasa baada ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya dola.
Alisema wananchi wanatakiwa kuelimishwa zaidi manufaa ya Muungano, fursa zinazopatikana na changamoto zake katika kuutetea na kuulinda.
Askofu NiweMugizi alisema serikali mbili ni maoni ya viongozi waliopo ndani ya CCM, ambao asilimia kubwa hawawakilishi Watanzania, ingawa ni sehemu ya Wazanzibari na Watanganyika.
Kuhusu mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba, huyo alisema kupatikana kwa Katiba Mpya lazima kuwepo misingi inayotetea haki za raia, demokrasia ya kweli na utashi wa watawala bila kuingiliwa na msimamo kisiasa.

Alionyesha wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya, kwani wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanatetea misimamo ya vyama vyao na hawapo tayari kumsaliti aliyewateua kwa sababu alitangaza msimamo wake alipolizindua.

“Rais (Jakaya Kikwete) wakati anazindua Bunge hilo kwa sababu ana mamlaka kisheria, alivunja taratibu, kwani asingelihutubia Bunge kwa kushinikiza Jaji (Joseph) Warioba kutangulia kuwasilisha Rasimu ya Katiba,” alisema Askofu NiweMugizi na kuongeza:

“Hotuba ilijikita kutangaza msimamo na mtazamo wa CCM kutaka serikali mbili, kwa kile tunachokiona ni kukumbatia madaraka ili viongozi waliopo wasipoteze nafasi, watawale milele, hata waanzilishi wa Tanganyika wapo hadi leo.”

Alisema mchakato wa kuwapata wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ulipata hitilafu baada ya kuingiza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambao kwa kiwango kikubwa ndiyo wasemaji kuliko wajumbe 201 waliotokana na taasisi mbalimbali za kiraia.
Chanzo:Mwananchi

ZAIDI YA MIL.500/- ZAHITAJIKA SHEREHE ZA MWENGE KGERA

Zaidi ya Mil. 500/- zahitajika sherehe za mwenge KageraMKUU wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, amesema zaidi ya sh milioni 500 zinahitajika kukamilisha sherehe za kuwasha mwenge kitaifa, Mei 2, mwaka huu.
Kanali Massawe aliwaomba wadau walioahidi kuchangia katika sherehe hiyo kukabidhi michango yao mapema ili maandalizi yaweze kukamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa hivi karibuni, Kanali Massawe alisema sherehe hizo zitafanyika katika Uwanja wa Kaitaba na mgeni rasmi atakuwa  Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali.
Alisema wakati wa mbio za mwenge, miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii itazinduliwa ambapo kwa sasa wanaendelea kuorodhesha miradi hiyo katika kila wilaya.
Kanali Massawe alisema baada ya mwenge kuwashwa, mbio zake zitaanza katika Manispaa ya Bukoba na kumalizia Wilaya ya Biharamulo.
“Naishukuru sana serikali  kuona umuhimu wa mwenge wa uhuru  kuwashwa Kagera kwa lengo la kuchochea maendeleo ya wananchi,” alisema Massawe.
Alisema wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wiki kuupokea mwenge huo na kusema kuwa patakuwepo na michezo mbalimbali katika sherehe hizo.
Chanzo:Tanzania Daima

WAHAMIAJI 32 WAKAMATWA KAGERA

Wahamiaji haramu 32 raia wa Burundi wamekamatwa na idara ya uhamiaji mkoni Kagera wakidaiwa kuingia nchini kinyume na sheria.

Afisa uhamiaji mkoani Kagera,  George Kombe amesema kuwa wahamiaji hao walikamatwa jana kutokana baada ya kupata taarifa kutoka kwa  raia wema .

Kombe amesema kuwa wahamiaji hao haramu walikuwa wakisafirishwa kwa gari aina ya Hiace lenye namba T633 CPZ , na kuwa walipohojiwa baadhi yao walisema walikuwa wakielekea nchini Burundi huku wengine wakidai walikuwa wakielekea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma.

Amesema kuwa utaratibu wa kuwasafirisha wote hadi mpakani mwa nchi yao umekamilika na kuahidi kumchukulia hatua za kisheria dereva wa gari hilo  kutokana na kuwasaidia wahamiaji haramu hao kuingia nchini kinyume na sheria.

Baadhi ya wahamiaji hao walipohojiwa na vyombo vya habari wamesema  kuwa wametoroka kutoka kambi ya wakimbizi ya Nyakivary nchini Uganda kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu.

SHULE YA MUGEZA MSETO HAINA VYOO

SHULE ya Msingi Mugeza Mseto inakabiliwa na ukosefu wa vyoo na bafu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Philemon Coelestine, alibainisha hayo juzi alipokuwa akitoa taarifa ya shule kwa Balozi wa China nchini aliyetembelea shule hiyo na kutoa vitabu vyenye thamani ya sh milioni tano.
Coelestine alisema mabweni yanayotumiwa na wanafunzi ambao ni walemavu hayakidhi mahitaji ya wahitaji.
Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa nyumba za watumishi, usafiri kwa wanafunzi na uchakavu wa miundombinu ya majengo, umeme na viwanja vya michezo.
Alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 650 kati yao walemavu wasioona 40, walemavu wa ngozi ni 40 na walemavu wa viungo ni 52.
Hata hivyo alisema pamoja na changamoto hizo shule hiyo imekuwa ikiendelea kufanya vizuri katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2010/13.
Alisema mwaka 2013 wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi walikuwa 66, kati yao wanafunzi 40 ambayo ni asilimia 61 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Balozi wa China Tanzania, Dk. Lu Youging, alisema wanafunzi wenye ulemavu wanao uwezo wa kujitegemea na kutoa mchango wao kwa maendeleo ya taifa.
Aliwashauri wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Ado Mapunda, alisema atasimamia msaada huo uliotolewa na Ubalozi wa China ili utumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Chanzo:Tanzania Daima

HALI YA HEWA KAGERA YAVUTA WAWEKEZAJI

HALI ya hewa na mandhari ya Mkoa wa Kagera  imeelezwa  kuwa ni kivutio kwa wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji na viwanda.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Youging katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe kilichokuwa kikielezea fursa za uwekezaji  mkoani hapo.
Dk. Youging  alisema Mkoa wa Kagera una ardhi nzuri  yenye rutuba inayofaa kwa kilimo licha ya kuwepo kwa vyanzo mbalimbali vya maji ambavyo husaidia katika kilimo cha umwagiliaji bila kusubiri kipindi cha masika.
Alisema pia mkoa wa Kagera una sehemu nzuri ya utalii ambayo ni fursa nzuri ya kuendeleza na kuinua uchumi wa mkoa.
Alisema pamoja na kuwepo kwa fursa nyingi za uwekezaji mkoani hapo, bado soko si zuri  na kueleza kuwa soko likiwa zuri wawekezaji zaidi watajitokeza.
Chanzo:Tanzania Daima

VIJANA WAISHI VYOONI KWA UGUMU WA MAISHA

VIJANA wanne wakazi wa mji wa O’murushaka, Kata ya Bugene, wilayani Karagwe, wanaishi kwenye vyoo vya huduma vya wasafiri vilivyopo katika mji  huo kwa miezi sita sasa kwa madai ya ugumu wa maisha.
Vijana hao walikutwa wamelala katika vyoo hivyo juzi wakati abiria walipotaka kujisaidia ili kujiandaa na safari zao.
Mmoja wa vijana hao, Bosco Venance (30), alisema shughuli zao kwenye eneo hilo ni kubeba mizigo na wamelazimika kuweka makazi kwenye vyoo kutokana na ugumu wa maisha.
Venance alisema kipato wanachopata ni kidogo, hivyo hawawezi kupanga nyumba na kununua chakula, ndiyo maana wamelazimika kuishi kwenye vyoo ili kukabiliana na ugumu wa maisha.
“Tumeishi kwenye choo hiki zaidi ya miezi sita sasa. Vyumba vya mji huu ni kati ya sh 15,000 hadi 20,000 unavyoona hali hii na wingi wa magari, wakiwemo wapiga debe hizo pesa tutazipata wapi?” alihoji Venance.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa kata hiyo, Vegirance  Kahungya, alikiri vijana hao kutumia vyoo hivyo kama makazi  yao.
Alisema ofisi yake kwa kushirikiana na uongozi wa kata, wamekuwa wakiwafukuza, lakini baada ya muda wanarudi.
Kahungya alisema ingawa kuna kufuri, vijana hao hutumia funguo bandia  na wakati mwingine kutumia nguvu kuvunja milango hiyo.
Msimamizi wa vyoo hivyo, Jonestha Kanyiginya, alisema  vijana wanaoishi kwenye vyoo hivyo  wamekuwa kero katika utendaji wa kazi, kwani usiku vyoo hivyo hugeuzwa kuwa makazi, hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji.
Alitaja changamoto nyingine  anazokabiliana nazo kuwa ni baadhi  ya vijana katika mji huo kujihusisha  na vitendo vya uporaji na  uvutaji bangi.
Aliuomba uongozi wa kata kutoa ulinzi ili wanaotumia vyoo hivyo kama makazi, wachukuliwe hatua.
Chanzo:Tanzania Daima

Wakazi Missenyi wawahofia askari wa Uganda

WATANZANIA waishio mpakani mwa nchi za Tanzania na Uganda  eneo la Mtukula lililopo wilayani Missenyi, Kagera, wamesema  wamechoshwa na vitendo vinavyofanywa na askari wa Uganda kuingia upande wa Tanzania  kukamata wahalifu wakiwa na silaha bila kufuata  sheria.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa majina, wananchi hao walisema juzi, saa 11 jioni askari wanne waliotokea Mbalala, Uganda walivuka mpaka kuwafuatilia wezi wa pikipiki waliokuwa upande wa Tanzania.
Walisema katika kurupushani za kuwakamata watuhumiwa  hao walikimbia  na kuingia ndani ya Kituo cha Polisi Mtukula kilichopo Tanzania.
Walisema wakati mtuhumiwa huyo akikimbilia katika kituo hicho, askari hao walianza kumfyatulia risasi ambazo hazikumpata mlengwa na badala yake kuwajeruhi  watu  wawili.
Walisema baada ya askari huyo kuingia katika kituo hicho cha polisi, alikamatwa na kunyang’anywa bunduki huku wenzake watatu walipoona mwenzao amekamatwa waliondoka na vijana wawili ambao ni Watanzania kuelekea nao Uganda.
Wananchi hao walisema imekuwa ni kawaida kwa askari wa Uganda kuingia  upande wa Tanzania na kuwakamata watu wanaowatuhumu na kuwapeleka Uganda  bila kufuata utaratibu wa mipaka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo alisema hayuko tayari kulizungumzia suala hilo linalogusa nchi mbili.
Alisema tukio hilo linashughulikiwa na vyombo vya ulinzi na usalama, ili taarifa zitumwe Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.
Chanzo ;Tanzania Daima

Kamanda CHADEMA auawa

KATIBU wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA) Kata ya Runazi, Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera, Oliva Evodius, ameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.
Kifo hicho ambacho kimeacha maswali mengi, kinahusishwa na mambo ya siasa, lakini pia wapo wanaokihusisha na mambo binafsi.
Akizungumza na gazeti hili jana,  Diwani wa Kata ya Runazi, Constantine N’kwenge, alisema kuwa katibu huyo ameuawa usiku wa kuamkia Jumamosi Aprili 6, majira ya saa nne usiku baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana na kumshambulia kwa mapanga  akiwa nyumbani kwake.
Mume wa marehemu, Evodius Malembeka, aliliambia gazeti hili kuwa marehemu alikutwa na tukio hilo akiwa naye.
Alisema Oliva alivamiwa wakati akiingia chumbani mwake akitokea bafuni kuoga.
Msemaji wa familia hiyo, Raphael Sostenes Zitta, ameitaka serikali kupitia vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi na kuongeza umakini katika uchunguzi wa matukio ya mauaji yanayofanyika na kuhatarisha usalama wa wananchi.
Jeshi la Polisi mkoani Kagera, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba linawashikililia watu wawili wakati likiendelea kufanya uchunguzi zaidi kubaini wahusika wa mauaji hayo.
Wakati huo huo, watu wawili wamelazwa katika hospitali teule wilayani hapa baada ya kujeruhiwa katika matukio tofauti yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali hiyo, Haula Balikaho, amewataja waliojeruhiwa kuwa ni Frank Wera Mussa,  mkazi wa Runazi na Chola Rufungulo, mkazi wa Kisenga, Kata ya Nemba, wilayani humo.
Alisema Frank amejeruhiwa kichwani baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira wakati Chola amejeruhiwa jicho la kulia baada ya kupigwa risasi na majambazi akitokea kwenye mnada wa ng’ombe.
Haula alisema hali za majeruhi  zinaendelea vizuri na wanaendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo na mmoja wa majeruhi hao, Frank Mussa, anatibiwa chini ya uangalizi wa polisi.
Chanzo;Tanzania Daima 

Umaskini chanzo cha vifo vya wajawazito

IMEELEZWA kuwa wajawazito wengi wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na umaskini wa kipato.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera, Revocatus Dominick, alipozungumza na Tanzania Daima Jumapili lilipomtembelea ofisini kwake.
Alisema, umbali wa vituo vya afya ni sababu inayochangia kwa kuwa wengi wao wanakosa fedha za usafiri wa kwenda kwenye vituo hivyo au hospitali.
“Umaskini unasababisha wanawake wengi kufariki dunia wakati wa kujifungua… watoto hufia tumboni mwa mama zao kwa vile wanachelewa kufika hospitalini,” alisema Dominick.
Awali aliwataka wanaume kuwasindikiza wake zao kliniki wakati wa ujauzito ili kwenda kupata ushauri na maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya wakiwa pamoja.
“Sababu nyingine ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu elimu sahihi ya afya ya uzazi, ukarimu wa wahudumu, jambo linalochangia wajawazito wengi kutofika kwenye vituo vya afya,” alisema.
Chanzo:Tanzania Daima 

GARI LATUMBUKIA KWENYE MTO KANONI MANISPAA YA BUKOBA‏

 Ajali hii imeyotokea usiku wa kuamkia  leo jumamosi  katika daraja la mto Kanoni barabara iendayo Bandarini kwenye manispaa ya Bukoba, Gari hilo ndogo ainaya  Toyota yenye namba za usajili T 910 CTC, ambalo mmiliki wake hajajulikana.
Japo katika eneo la tukio mwananchi mmoja alisikika akisema ni mal;i ya Askari Polisi ambae hakumtaja jina, Mtandao huu ulifika kwenye kituo cha Polisi kujilidhisha na tulikutana na Bw Magayane ambae ni msaidizi katika kitengo cha Usalama Barabarani alikiri kuwa na Tarifa za ajali hiyo na kusibitisha kuwa hakuna aliyeumia, na nilipotaka kujua mmiliki wa Gari hili alisema hawamjui wapo katika jitihada za kumtambua.
 Wananchi wakiangalia ajali ya gari  Daraja la mto Kanoni barabara iendayo Kastam bandarini
 Kama kweli ni ulevi ni nomaaaa
 Jamani umakini Barabarani ni muhimu

Mwendo kasi, ulevi, kuongea na simu ni hatari unapoendesha gari kuwa makini. 

PICHA NA JAMCO BLOG
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa