BAADHI ya wakazi wa Kijiji cha Bulembo ambao walikumbwa na maafa ya
nyumba zao kuanguka na nyingine kuezuliwa na mazao yao kuharibiwa na
mvua, wamedai kutelekezwa na serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema walipatwa na
maafa hayo Machi 20, mwaka huu, lakini hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu,
Kitengo cha Maafa kimekaa kimya wakati hawana chakula wala mahala
salama pa kuishi na kwamba baadhi yao wanalala katika magofu.
Pia wameulalamikia uongozi wa kijiji hicho kwa kugawa misaada kwa upendeleo.
Walisema misaada inayotolewa wanagawiwa hata ambao hawakuathiriwa na mvua hizo huku walioathiriwa wakiachwa.
Mmoja wa wananchi hao, Elipidius Christopher, mkazi wa kitongoji cha
Bulembo, alisema nyumba yake ilianguka, mazao yake yote ikiwamo
migomba, mibuni, magimbi na mihogo yameharibika, lakini amekuwa
akibaguliwa wakati wenzake wanapopatiwa misaada.
“Sikupewa hema, nalala kwenye gofu nikiwa na watoto wangu, viongozi
wangu wana taarifa kuwa nami ni mmoja wa watu walioathirika, lakini
sifahamu kwa nini nabaguliwa,” alisema Christopher.
Pia walilalamikia uongozi wa kijiji hicho kupokea misaada ya vyakula na kuifungia stoo wakati wao hana chakula.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bulembo, Longinus Clement, alikiri baadhi
ya wananchi wake kutopatiwa misaada inayopelekwa kijijini hapo
kutokana na kutoorodheshwa katika orodha ya awali ambayo inatumika
kugawa misaada hiyo.
“Wakati wanapita kuorodhesha wananchi walioathirika katika kitongoji
changu, mimi nilipewa kazi ya kuhesabu miti iliyoangushwa na upepo,
niliporejea nilikuta viongozi wenzangu wamekwishaorodhesha waathirika,
nikagundua kuwa kuna ambao walibaki bila kuorodheshwa,” alisema.
Clement alisema baada ya kugundua hilo aliwasiliana na viongozi
wenzake lakini cha kushangaza walikataa kuwapatia misaada wakidai
wanagawa kwa kutumia orodha ya awali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulembo, Trazias Kyabona, alisema
wanaolalamika kuwa misaada inayotolewa imefungiwa stoo ni majungu,
kwani kinachofanyika wanakusanya misaada midogomidogo na kuiweka
pamoja na baadaye kuigawa kwa wananchi.
Kyabona pia alikana misaada hiyo kuwagawia watu ambao hawajaathirika
na kuwa misaada hiyo wanapewa kulingana na walivyoorodheshwa na kamati
ya maafa ya kijiji kwa kushirikiana na kamati ya maafa ya wilaya.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment