Wananchi katika Kisiwa cha Musira mkoani Kagera wameanza
kuteketeza ndege waliodaiwa kutoa kinyesi chenye sumu, huku Wizara ya
Afya na Ustawi wa jamii ikiendelea kukalia majibu ya utafiti kuhusu
ukweli wa madai hayo.
Wizara iliahidi ingetoa majibu ya utafiti huo mapema.
Gazeti hili lilishuhudia idadi kubwa ya viota
vilivyokuwa na vifaranga na mayai ya ndege hao waliodaiwa kuwa wa ajabu
vikiwa vimeharibiwa.
Awali ilielezwa kinyesi chao kilidaiwa kuwa na sumu kali iliyohusishwa na vifo vya mifugo.
Mmoja wa wananchi katika kisiwa hicho Jackson
Robert ambaye alikutwa akikata matawi yenye viota ili kuharibu mazalia
ya ndege hao alisema wananchi walikubaliana kuwaangamiza ndege hao ili
kuepuka madhara yaliyojitokeza.
“Hawa ni viumbe wa ajabu sana, kinyesi chao kina
sumu kali kwani kikianguka kwenye bati zinatoboka baada ya muda mfupi,
lakini pia wanyama wakila kinyesi hicho hufa,” alisema mkazi huyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Fabian
Massawe alithibitisha ndege hao kuvamia kisiwa hicho na baadaye Wizara
ya Afya kutuma watafiti kuchunguza ukweli wa madai ya ndege hao kutoa
kinyesi chenye sumu.
Ilidaiwa ndege hao pamoja na kinyesi chao kutoboa
mabati pia kuku 516 na mbuzi 12 walikufa katika mazingira yaliyohusishwa
na ukali wa kinyesi chenye sumu kilichosababishwa na ndege hao.
Hata hivyo gazeti hili lilipomtafuta Dk. Munda
Elias ambaye aliongoza utafiti huo kutoka Wizara ya Afya kutaka kupata
majibu ya utafiti huo, mtaalamu huyo alikata simu na kuendelea kufanya
hivyo kila alipotafutwa.
Hata baada ya kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi
kwa njia ya simu kuhusu nia ya kufahamu matokeo ya utafiti huo, hakuna
jibu lolote lililotolewa pamoja na kuwa ndiye aliyefika katika kisiwa
hicho na kuchukua sampuli za ndege hao kwa ajili ya chunguzi zaidi wa
kimaabara.
Pia mtafiti huyo wa wanyama na ndege baada ya
kufika katika kisiwa hicho wiki chache zilizopita aliwaeleza wananchi
kuwa wamefika kuangalia ukubwa wa tatizo na kuwataka watoe ushirikiano
ili kupata ufumbuzi wa madai yao.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment