Home » » DHURUBA YALAZA NJE KAYA 122 KAMACHUMU

DHURUBA YALAZA NJE KAYA 122 KAMACHUMU

KAYA 122 katika Kijiji cha Bulembo, Kata ya Ibuga, Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera zimekumbwa na maafa kutokana na mvua na upepo mkali ulioezua nyumba zao na kuangusha migomba na mazao mengine kwenye mashamba yao.
Maafa hayo yameathiri wakazi zaidi ya 600 ambao hadi jana hawakuwa na makazi wala uhakika wa chakula.
Baadhi yao walisema kuwa hadi jana serikali ngazi ya wilaya na mkoa ilikuwa haijatoa msaada wowote kwao, ingawa Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, alisambaza taarifa kwenye mtandao wa Friends of Bukoba (FoB) kuwa alikuwa ametoa taarifa kwa uongozi wa wilaya na mkoa.
Hata hivyo, taarifa zinasema wataalamu kutoka wilayani walikuwa kijijini hapo wakiendelea na ‘upimaji’ katika maeneo ya nyumba zilizoezuliwa wakiambatana na Mwenyekiti wa Kijiji, Trasias Kyabona.
Haikujulikana baada ya upimaji huo serikali itatoa msaada gani kwa wananchi hao.
Diwani wa Kata ya Ibuga, Joseph Rweyongeza Rwazo (75), anasema hajawahi kuona upepo mkali wa namna hiyo.
Dhoruba hiyo imeezua pia madarasa yote katika Shule ya Msingi Rugongo iliyo kijijini hapo.
Kijiji hicho kina vitongoji vinne – Bulembo, Bungezi, Butorogo na Katoma. Vyote vimeathirika kwa dhoruba hiyo.
Viongozi wa vitongoji na kijiji walizungumza na Tanzania Daima kwa simu kutoka Bulembo jana na kuthibitisha kuwa juzi na jana waliendelea kukutana na wanakijiji  ili kutafuta ufumbuzi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bungezi, Jason Mutema, alisema kwamba kwenye kitongoji chake pekee nyumba 82 zimeezuliwa na upepo.
Nyumba nyingine zilizoezuliwa katika vitongoji vingine ni kama ifuatavyo: Bulembo (27), Katoma (7) na Butorogo (5).
Kutokana na maafa hayo, viongozi hao na wanakijiji wengine wanaendelea na jitihada za kusaidia familia hizo, ambazo hadi jana zilikuwa zinaishi kwa taabu.
Wengine wamelazimika kuishi kwa majirani, wakati wakitafuta ufumbuzi wa tatizo hili.
Mvua za masika bado zinaendelea kunyesha na kuleta hofu kwa wananchi. Kuanguka na kung’oka kwa migomba kumeongeza misukosuko kwa wananchi hao, kwani migomba hiyo ambayo ndilo zao kuu la chakula mkoani Kagera, imeshambuliwa na ugonjwa wa ‘mnyauko’ ambao kwa muda sasa umekuwa unatishia usalama wa chakula mkoani humo.
Viongozi wa kijiji wanaendelea kuwasiliana na ndugu, wadau na serikali ili kunusuru familia zilizoathiriwa na maafa hayo.
Maeneo mengine yaliyoathirika na mvua za masika ni kata za Ngenge na Rutoro, ambako mafuriko yanahatarisha ustawi wa wananchi wa maeneo hayo.
Juzi Ijumaa, Mto Kasharunga ulifurika na kuzuia wananchi kwa siku nzima. Mafuriko hayo yalivuruga pia soko la wazi la kila wiki (Omujajaro) katika eneo la Omumpike, ambalo hutumika kuuza na kununua bidhaa kwa wakazi wa Rutoro, Ngenge na maeneo jirani.
Baadhi ya wananchi walinusurika kusombwa na maji. Kwa mujibu wa mwananchi mmoja, Robert Rwegasira, ambaye alikuwa anasafiri kutoka Kamachumu kwenda Rutoro na wenzake watatu, wananchi kadhaa, akiwamo mwenzake, Justin Kingi, waliokuwa wamepanda pikipiki, walikuwa wamesombwa na mkondo wa maji, lakini wananchi walifanikiwa kuwanusuru.
Tofauti na kata nyingine za Jimbo la Muleba Kaskazini, Kata ya Rutoro ni moja ya maeneo yasiyo na miundombinu ya kutosha.
Hakuna barabara. Hakuna mito ya kudumu. Hakuna visima vya maji.
Gazeti hili linahamasisha wananchi wa Muleba waishio popote ndani na nje ya nchi watakaopata ujumbe huu, wanaopenda kutoa mchango wa kusaidia wananchi hawa wawasiliane moja kwa moja na mratibu kwa simu namba 0758000225.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa