KITIMUTIMU cha kumtafuta bingwa wa Kombe la Rweikiza kinatarajiwa
kuanza kutimua vumbi Machi 25, mwaka huu na kushirikisha vijiji 92 vya
Jimbo la Bukoba Vijijini, mkoani Kagera.
Kombe hilo litaanza kwa mchujo kuanzia ngazi za vijiji na hatimaye
kata na kumpata mshindi wa kwanza, ambako zawadi kwa washindi
zinatarajiwa kutajwa hivi karibuni na waandaaji wa mashindano hayo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Kishogo juzi,
Katibu wa Michezo wa Jimbo hilo, Cajethanus Charles, alisema tayari
mchakato umekamilika na kwamba, Machi 25 michuano itaanza katika vijiji
mbalimbali na hatimaye kumpata mshindi wa kombe hilo maarufu kwa jina
la Rweikiza Cup.
Hata hivyo, aliwataka viongozi walioteuliwa katika maandalizi hayo
kuanza kuwaandaa vijana vema ili michuano iwe na mvuto zaidi kwa kupata
pia mashabiki wengi wa kuiangalia.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo ambaye ndiye muandaaji wa mashindano hayo,
Jasson Rweikiza, alisema tayari amenunua mipira zaidi ya 1,000 na jezi
za kugawa kwa timu zote katika vijiji husika, sambamba na mabasi mawili
ambayo yatatumika kubeba wachezaji pamoja na dawa mbalimbali, hivyo
wachezaji wanatakiwa kukaa mkao wa kula tayari kwa mashindano hayo.
Alibainisha kuwa amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara lengo likiwa ni
kujenga umoja baina ya vijana waliopo kijijini humo na hata kuwafanya
wawe katika hali ya kuwaza michezo na si kuwaza kujiingiza katika mambo
mabaya ambayo katika jamii hayana nafasi.
Pia alisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa sasa lipo katika
mchakato wa kusaka vipaji katika wilaya mbalimbali, hivyo ingekuwa vema
wakafika katika ligi hiyo ambayo anaamini vijana wake wana vipaji ili
waweze kutangazika.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment