Ndege wa ajabu wakiwa juu ya miti katika Kisiwa cha Musira kilichopo
Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. Ndege hao wamezua hofu kwa wakazi
kutokana na kinyesii chao kudhuru mifugo na ndege.
Ndege wa ajabu wanaosadikiwa kutoa kinyesi chenye sumu kali,
wamevamia Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba na kusababisha
vifo vya mifugo na ndege wafugwao, huku ukali wa sumu hiyo ukisababisha
kutoboka mabati ya nyumba zilizopo kisiwani humo.
Ndege hao wanaoaminika kuvamia kisiwa hicho mwezi
mmoja uliopita tayari wameshasababisha vifo vya kuku 516 na mbuzi 12
wanaodaiwa kugusa au kula kinyesi chao. Hata hivyo, bado haijafahamika
ndege hao wanatokea nchi gani.
Akithibitisha habari hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera,
Kanali Mstaafu, Fabian Massawe alisema Serikali ilipata taarifa hizo
kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na baadaye kuundwa timu ya
kutafuta taarifa za awali za tatizo hilo.
Massawe alisema ndege hao, pamoja na kusababisha
vifo vya mifugo na ndege wafugwao pia baadhi ya miti katika kisiwa hicho
imekauka na mabati kutoboka inapotokea kinyesi chao kitaangukia kwenye
paa za nyumba zao.
Pia Massawe alisema kuwa, taarifa ya kuwapo kwa
ndege hao katika Kisiwa cha Musira, ilifikishwa kwa Naibu Waziri wa
Afya, Dk. Kebwe Stephene Kebwe aliyekuwa mkoani humo wiki iliyopita na
kuwa suala la kuwapo kwa ndege hao siyo la ghafla kwa kuwa walikuwapo
hapo awali.
Dk. Kebwe alisema wizara imetuma wataalamu
kuchunguza tatizo hilo na kuwa wizara hiyo itaangalia ukubwa wa tatizo
hilo linavyoweza kuwaathiri wananchi.
Hata hivyo, alisema suala hilo pia linahitaji
ufuatiliaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Dk. Munda Elias
alikwishawasili kwa ajili ya uchunguzi na kuthibitisha kuwa tayari
kinyesi cha ndege hao kimepelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi na Mkoa
unasubiri matokeo ya utafiti huo.
Naye Ofisa Tarafa wa Rwamishenye, Abdon Kahwa
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Ziporah Pangani alisema
tayari Serikali imechukua hatua za kupiga marufuku kupeleka au
kusafirisha mifugo kutoka kisiwani humo kwenda maeneo mengine kwa hofu
ya kusambaa kwa sumu hiyo.
Pia alisema ndege hao wameleta hofu kwa wakazi wa
kisiwa hicho, kwani kinyesi chao kinapodondoka kwenye bati hupata kutu
na kutoboka, huku kukiwa na hofu nyingine kwamba huenda mifugo nayo
imeathiriwa.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment