Muleba. Watu watatu akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Chochea Moto,
Elmes Fabian, wanashikiliwa na polisi mkoani Kagera kwa tuhuma za
kufanya uhalifu, kufyeka mashamba ya migomba na kuvunja nyumba tatu za
wakazi wa Kijiji cha Kishulo wilayani Muleba wakiwatuhumu kwa uchawi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga
alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kudai kuwa mchungaji wa kanisa
hilo, wakiwamo watu watatu wanashikiliwa kwa kosa la kuchochea vurugu,
kuidhuru miili na kuharibu mali kinyume cha sheria.
Kamanda Mayunga aliwataja walionusurika kuuawa
kuwa ni Fabian Albert na mkewe Gaudensia Fabian, Methodia Leonard na
Georgina Kayonga wote wakazi wa Kijiji cha Kashulo wilayani humo mkoani
Kagera.
Alisema uchunguzi wa jeshi hilo umebaini baadhi ya
wananchi wakiwamo watoto wa watuhumiwa wa ushirikina walifanya ukatili
huo wakishirikiana na baadhi ya wananchi waliokuwa na lengo la kuwaua
wazee wa familia hizo.
Tukio hilo limesababisha wananchi zaidi ya 12
wakiwamo watoto na wanafunzi wa shule za msingi kukosa makazi, huku
wazazi wao wakilazimika kukimbilia kwenye Taasisi ya Kusaidia Wazee na
Yatima ya “Kwa Wazee” iliyopo Kata ya Nshamba wilayani Muleba ili kupata
hifadhi ya muda.
Aidha, alisema mchungaji wa kanisa hilo anadaiwa
kuwahubiri waumini wake kuwa ana uwezo mkubwa wa kuwabaini wachawi ambao
wamekuwa wakisumbua kijijini humo kabla ya kuanza kuwataja kwa majina.
Hatua hiyo, ilionekana kupokewa kwa hisia kali na
waumini wake wakiwamo watoto wa watuhumiwa, hivyo kuungana na wananchi
wengine kwenda kuharibu mali na kuwadhuru wazee hao kwa mapanga.
Kwa upande wake, Mratibu wa “Kwa Wazee”, Lydiah
Lugazia alisema kutokana na ukatili huo kwa wazee hao wamelazimika
kuwachukua na kuwahifadhi kwa muda, ili kunusuru maisha yao kutokana na
wananchi kutaka kuwaua kwa imani potofu za kishirikina.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Lambris Kipuyo akiongea
na gazeti hili alitoa onyo kwa wananchi wote wenye tabia ya kujichukulia
sheria mkononi na kwamba wanapaswa kutoa taarifa kwenye vyombo vya
usalama iwapo kuna mtu mwenye tuhuma mbaya katika jamii husika.
Alisema vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ni
kuvunja sheria za nchi na kuondoa uhai wa mtu ni kuvunja sheria za
mungu, hivyo wazingatie maadili ya kiimani na kufuata sheria.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment