Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara Atembelea Shamba la Kahawa na Migomba ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana kutoka SACCOS ya Ibwera Bukoba


 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Dk. Fenella Mukangara (kushoto) akiangalia kahawa katika shamba darasa
inayolimwa na Ibrahim Mulokozi (kulia) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ibwera
wilayani Bukoba aliyenufaika na mkopo wa shilingi laki nne kutoka mfuko wa
maendeleo ya vijana. Waziri Dk. Mukangara alilitembelea shamba hilo la kahawa
na migomba jana ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana kutoka SACCOS ya
Ibwera zimewanufaishaje kimaisha.
 Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kushoto)
akimuangalia samaki mwenye umri wa miezi mitatu anayefugwa katika bwawa la
Kikundi cha Msifuni kilichopo kijiji cha Kemondo wilayani Bukoba ambacho
kilipata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana. Waziri Dk. Mukangara
alilitembelea bwawa hilo jana ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana
kupitia mfuko wa Halmashauri nimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kushoto) akipokea
taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo wilayani Bukoba kutoka kwa Benedicta Peter
ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo ilipata mkopo wa shilingi milioni tano
kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na kuvikopesha vikundi mbalimbali vya
maendeleo vya vijana.

----

Na Anna Nkinda –Maelezo, Kagera

Serikali
imeombwa kuongeza kiasi cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko
wa maendeleo wa vijana na Halmashauri za wilaya kwani kiwango
kinachotolewa kwa sasa cha shilingi milioni tano kwa vyama vya Kuweka
Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo ukilinganisha na mahitaji ya mkopo
huo.



Ombi hilo limetolewa jana na baadhi ya vijana
waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na halmashauri ya wilaya
ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.



Vijana
hao walisema kuwa fedha za mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua
kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya
biashara zao, kulipa karo za shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha
tofauti na ilvyokuwa awali kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za
ujasiriamali. 



Kwa
upande wake mkazi wa kijiji cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata
mkopo wa shilingi laki nne kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa
ameweza kununua matandazo na kulipa wasaidizi wanaohudumia shamba lake la migimba na kahawa ambalo ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni na Nyakibimbili na kwenda kujifunza na kuchukua miche ya migomba.



Alisema
kuwa anakabiliwa na changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza
shughuli za kilimo, kutoka na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba,
bei ya miche ya kahawa kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche
mmoja, kuendelea kutumia jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika
hasa soko la ndizi na magonjwa ya migomba.



Naye katibu wa kikundi cha Msifuni Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na laki tano kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba alisema kuwa kikundi chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa samaki na walianza na bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha kuwa kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.



“Changamoto
zinazotukabili ni kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na
elimu ya kuendesha na kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma
kwa mradi wetu wa samaki ikiwa ni pamoja na kuibiwa na kuharibiwa kwa mabwawa hasa nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za maendeleo”, allisema Joel. 



Kwa
upande wake waziri Dk. Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho
kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga katika vikundi vya maendeleo jambo
ambalo litawafanya waweze kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana na halmashauri ya wilaya na hivyo kuweza kujishughulisha na kazi za upandaji wa miti, kilimo cha samaki na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki.



Dk. Mukangara alisema, “Vijana ni lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya uvivu, kufanya
kazi si lazima uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa
Ibwera kunahali ya hewa nzuri na milima mingi haina miti mnaweza kuwa na
mradi wa kupanda miti na kufuga nyuki ambao watawapatia asali na
mkiiuza mtapata fedha nahivyo kujikwamua kiuchumi”. 



Kwa
upande wa mafunzo ya ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa
wizara yake inavituo vya kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika
ambao ni vijana watakuwa tayari kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi, stadi za maisha watayapata na yatawasaidia katika maisha yao.



Waziri Dk. Mukangara alikuwa mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na vikundi vya vijana vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha hizo zimewasaidiaje vijana
kujikwamua kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba alilitembelea shamba la
mfano la kahawa na migomba, kikundi cha burudani cha Rugazi na shamba la samaki la kikundi cha Msifuni.

WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO DK MUKANGARA AMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA KAGERA




Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara (kushoto) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu Fabian Massawe mara baada ya kumtembelea ofisini kwake jana mjini Bukoba. Waziri Dk. Mukangara yupo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe alipomtembelea ofisini kwake jana mjini Bukoba. Waziri Dk. Mukangara yupo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kushoto ) akiongea na viongozi wa mkoa wa Kagera (hawapo pichani) jana mjini Bukoba jinsi Serikali inavyoangalia uwezekano wa kuongeza mkopo kwa SACCOS zinazolenga shughuli za maendeleo ya vijana kutoka shilingi milioni tano hadi kumi kutokana na mahitaji ya fedha hizo kuwa makubwa. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana James Kajugusi.(Picha na Anna Nkinda – Maelezo)

TAMASHA LA SHANGWE LAFANA MJINI BUKOBA




 Mwimbaji wa
Nyimbo za Injili,Rose Muhando akitumbuiza kwenye Tamasha la shangwe
Kagera katika uwanja wa Kaibata mjini Bukoba mwishoni mwa wiki,tamasha
hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Beula Communication kwa ajili ya
kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika mkoa wa kagera.




 Mwimbaji wa
Nyimbo za Injili,Enock Jonas(Zunguka) akitumbuiza kwenye Tamasha la
shangwe Kagera katika uwanja wa Kaibata mjini Bukoba mwishoni mwa
wiki,tamasha hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Beula Communication kwa
ajili ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika mkoa
wa kagera.




 Masista wa
Kituo cha Tumaini Children’s Centre, Sr.Adventina Kyamanywa (kushoto) na
Sr.Esther  wakijadiliana jambo  wakati wa tamasha la shangwe Kagera
katika viwanja vya Kaitaba mjini Bukoba.






Mkurugenzi wa
Beula Communication, Melkzedek  Mutayabarwa akizungumza kwenye Tamasha
laShangwe Kagera,ambapo kampuni hiyo ndio iliyoandaa tamasha hilo.  




Mkuu wa
Wilaya  Bukoba,Zippora Pangani akihutubia kwenye  Tamasha la shangwe
Kagera katika uwanja wa Kaibata mjini Bukoba mwishoni mwa wiki,tamasha
hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Beula Communication kwa ajili ya
kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika mkoa wa kagera.




 Waimbaji wa kwaya ya Vijana ya KKKT Usharika wa kanisa Kuu la Mjini Bukoba wakitumbuiza kwenya tamasha la Shangwe Kagera.




Rose Muhando akiwaburudisha viongozi walioudhuria Tamasha la Shangwe Kagera katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa