Wananchi wachoma nyumba ya mtendaji


na Ashura Jumapili, Kagera
WANANCHI wa Kijiji cha Nyakabango, Tarafa ya Kimwani, wilaya Muleba, mkoani Kagera wamechoma nyumba ya mtendaji na mwenyekiti wa kijiji hicho na kuharibu mali zenye thamani ya zaidi ya sh milioni baada ya viongozi hao kudaiwa ‘kuchakachua’ mahindi ya misaada yaliyotolewa kwa wananchi hao.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Philip Kalangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Juni 20 mwaka huu kati ya saa 2:00 hadi saa 6:00 usiku.
Alisema kabla ya mali hizo kuharibiwa kulikuwa na vurugu za wananchi dhidi ya viongozi wa Kijiji cha Nyakabango ambao ni Ofisa mtendaji wa Kata Nyakabango Ansbert Sabinian(52) na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakabango Ladislaus Manana (41).
Alieleza chanzo cha ugomvi huo ni msaada wa mahindi tani 61.5 uliopelekwa kwa viongozi hao wa kijiji Mei 28 mwaka huu uliotoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba lengo likiwa ni kugawa kwa wananchi na zoezi hilo lilifanyika.
Alieleza kwamba Juni 19 viongozi waligawa mahindi hayo katika Kitongoji vya Rwenkara na kesho yake waligawa vitongoji vya Nyamagojo na Nyakabango kisha kuwatangazia wananchi kuwa mahindi yamekwisha.
Alieleza kwamba ilipofika majira ya saa 1:00 usiku kulikuwa na minong'ono kuwa mahindi yamechakachulia na viongozi na kuwa ugawaji wa mahindi hayo haukufuata taratibu ndipo walipofanya msako na kukuta mahindi lukuki yakiwa kwa viongozi hao.
Miongoni mwa sehemu walizokuta mahindi hayo ni nyumbani kwa Sabinian (Ofisa Mtendaji wa Kata) ambako walikuta gunia moja na nusu na kwa Tilusubia (magunia mawili), ambapo waliyatoa nje na kuchoma nyumba moto.
Walikuta pia magunia 12 ya mahindi nyumbani kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Ladslaus Manana.
Kwa mujibu wa Kamanda Kalangi, uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea na wanawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni mtendaji na mwenyekiti.
Chanzo: Tanzania Daima

Bei ya kahawa yashuka Kagera


na Antidius Kalunde, Bukoba
CHAMA Kikuu cha ushirika mkoani Kagera (KCU 1990 LTD) kimeshusha bei ya kahawa kwa kile ilichodai kutokana na kushuka kwa bei hiyo katika soko la dunia.
Mwenyekiti wa chama hicho, John Binunshu, alisema kushuka kwa bei hiyo kunatokana pia na bei ya mnadani kuporomoka kwa siku za hivi karibuni hivyo kulazimu KCU kubadilisha bei ya manunuzi tofauti kama ilivyokuwa awali.
Kutokana na kushuka kwa bei hiyo Binunshu aliwataka wakulima wa kahawa mkoani hapa kutokuwa na wasiwasi kuhusu taarifa hizo kwani wataendelea kupatiwa taarifa za bei kadiri hali ya soko itakavyokuwa.
Katika taarifa ya Meneja mkuu wa KCU, Vedasto Ngaiza, iliyosambazwa kwa mameneja wote wa  vyama vya msingi vipatavyo 129 ambavyo vinaendelea na ununuzi wa kahawa kwa msimu huu ambao umefunguliwa rasmi mwezi Mei mwaka huu, bei ya kahawa imeteremka kutoka sh 1,350 hadi sh 1,100 kwa Kahawa aina ya Robusta maganda, huku robusta safi ikiuzwa kwa sh 2,200 kwa kilo.
Kahawa aina ya Arabica maganda imeshuka kutoka sh 1,550 hadi sh 1300 huku safi ikinunuliwa kwa sh 2,600.
Awali mabadiliko ya bei hizo yalionekana kuleta wasiwasi kwa wakulima huku baadhi yao wakihushutumu uongozi wa KCU kuamua kuteremsha bei mara baada ya kubaini kuwepo wingi za kahawa kwa wakulima.
Chanzo: Tanzania Daima

Madiwani wataka mgodi uongeze mrabaha


Na Ali Lityawi, Biharamulo
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera wamemtaka mwekezaji wa mgodi wa dhahabu wa Tulawaka aongeze malipo ya mrabaha kwa madai kuwa sh milioni 300 kwa mwaka zinazotolewa kaziendani na uzalishaji wanaoufanya.
Akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani, diwani wa Nyabusozi, Musure Bitanabona, alimtaka mwekezaji huyo kuongeza fedha za mrabaha zinazolipwa kwa mwaka kwa halmashauri kwa kuwa fedha hiyo hakiendani na faida kubwa anayoipata.
“Mheshimiwa mwenyekiti siungani mkono malipo ya mrabaha yanayolipwa na mgodi wa Tulawaka…hawa watu wamekuwa wakitupatia kiasi kidogo sana cha fedha ukilinganisha na uzalishaji wanaoufanya, ziara tuliyofanya mgodini imetufumbua mengi, tumeshuhudia kazi zinavyofanyika mgodini hapo.
‘Kwanza mazingira yetu wameyaharibu sana na tuliona mashimo marefu ambayo hata huwezi kufika kwa macho…hii inaonyesha wazi jinsi mwekezaji huyo anavyonufaika na rasilimali zetu huku sisi tukiendelea kutaabika,” alisema Bitanabona.
Hoja hiyo iliungwa mkono na madiwani wengie na kutaka mwekezaji huyo kuongeza fedha za mrabaha na kufuikia sh bilioni moja, ili iwe rahisi kwa halmashauri hiyo kupeleka maendeleo kwa wananchi wake.
Chanzo: Tanzania Daima

Wazee watakiwa kutojihusisha na siasa


na Antidius Kalunde, Bukoba
WAZEE wameshauriwa kutojihusisha na siasa na badala yake watafute mbinu za kukabiliana na hali ngumu ya maisha, ili kuepuka kuwa ombaomba katika maisha yao ya kila siku.
Ushauri huo ulitolewa na Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Bukoba, Mrisho Issa kwa niaba ya mkurugenzi wa manispaa hiyo wakati wa kufungua tawi la Saidia Jamii ya Wazee Kagera (SAJAWAKA) tawi la Kata ya Kahororo katika manispaa hiyo ambalo limeanzishwa kwa ajili ya kusaidia wazee.
Alisema wazee wanapofungua vikundi kama hicho wanapaswa wajue malengo yake na wala wasijihusishe na siasa, kwani wakati wa kushabikia masuala ya siasa yawe nje ya vikundi hivyo.
Aliongeza kuwa vipo vikundi vingi vinaanzishwa lakini malengo ambayo yamekuwa yamekusudiwa hayafanyiwi kazi na badala yake wanashabikia mambo ya kisiasa.
Katika hatua nyingine, alisema pamoja na kufungua tawi la wazee bado kuna changamoto kwa wazee kutopata huduma ya afya bure hasa wale waliotimiza miaka 60 na kuendelea kama sera ya wizara inavyosema.
Nae Mwenyekiti wa tawi la Saidia jamii ya wazee Kagera tawi la Kata ya Kahororo, Silivandi Muyoza alisema kikundi hicho hakikuanzishwa kwa lengo la siasa na badala yake ni kwa ajili ya kusaidia wazee kimaendeleo kwa kubuni miradi mbalimbali.
Chanzo: Tanzania Daima

Radi yaua sita Kagera


Na Mbeki Mbeki, Bukoba


WATU sita wamefariki dunia kwa kupigwa na radi, watatu wakiwa wa familia moja katika Kata ya Kibingo, Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Methodia Kaledunia (35), Bateganya Kamashana (miezi 10) na Kamugisha Kamashara (2).
Wengine waliokufa ni Kazungu Emmanuel (15), mwanafunzi wa darasa sita Shule ya Msingi Kihinda, Dawson Aaron (16) mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kihinda na Revelian Wilison (4).
Alisema tukio hilo lilitokea Juni 8, majira ya jioni katika Kijiji cha Kihinda, wilayani Kyerwa na kwamba watu hao walikuwa wamejikinga na mvua kwa jirani yao.
Aidha, alisema katika tukio hilo pia mbuzi watano walikufa kwa kupigwa na radi, nyumba moja na baadhi ya mashamba yaliharibiwa vibaya.
Mtendaji wa kijiji hicho, Jofrey Milambwe, alisema watu watatu wa familia moja wamezikwa katika kaburi moja kutokana na mwili yao kuharibika vibaya.

Chanzo: Tanzania Daima

Muleba haina viwanda vya samaki


Na Amana Nyembo, Muleba

LICHA ya Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, kuwa na eneo kubwa la uvuvi, uchunguzi umebaini kuwa haina kiwanda hata kimoja cha kusindika minofu ya samaki.
Uchunguzi uliofanywa na wilayani hapa umebaini kuwa Muleba yenye eneo la mita za mraba 7,225 za maji ya Ziwa Victoria, visiwa 25 pamoja na Ziwa Burigi, wakazi wake kwa kiasi kikubwa wamejikuta wanabakia maskini kutokana na mapato makubwa kwenda nje ya wilaya.
Ofisa Uvuvi wa Wilaya hiyo, Symphorian Ngaiza, aliliambia Tanzania Daima kuwa kutokana na hali hiyo wakazi hao wamekuwa wakikosa ajira kwa vile viwanda vingi viko mkoani Mwanza.
Alisema kikwazo kikubwa kilichozuia wawekezaji kutovutika kuwekeza kwa kujenga viwanda ni miundombinu mibovu ya barabara za kuelekea maeneo ya uvuvi, ukosefu wa umeme, kiwanja cha ndege.
“Mathalani eneo la mwalo wa Kyamkwikwi lilitengwa kama sehemu inayofaa kwa ujenzi wa viwanda vya samaki lakini hakuna umeme, barabara na miundombinu nyingine, hivyo wanunuzi wa samaki wananunua na kupeleka viwandani kwao Mwanza,” alisema Ngaiza.
Hata hivyo, wakati halmashauri ikifikiria zaidi katika upatikanaji wa viwanda vya samaki, kumekuwapo na mgongano wa mawazo baina yake na wananchi wengi wanaodhani ujio wa viwanda hivyo, unatowesha samaki na hivyo kufanya kitoweo hicho kipande bei.
Licha ya wananchi hao kulitazama suala la ajira kama faida moja wapo kwao lakini hatua ya samaki wengi kwenda viwandani hawaliafiki wakati wao wakiendelea kuhangaika kukosa kitoweo.
Aidha, kwa upande wa pili uchunguzi umebaini kuwa wafanyabiashara hao wadogo hawana imani na viwanda kwa sababu huwanyonya katika suala zima la mauzo.
Wakizungumzia suala la samaki kwenda viwandani walisema tangu kuingia biashara ya kimataifa ya samaki wao kama wazawa wilayani Muleba hawanufaiki na ziwa Victoria.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Al Haji Masoud Abeid alisema uvuvi ulipoingiliwa na serikali kwamba samaki waende viwandani na hatimaye kuuza nje ya nchi wao wanapata shida.
Alisema samaki wanapovuliwa na kwenda viwandani ndio chanzo cha wananchi kukosa kitoweo hicho, hali inayowasababishia kula mboga nyingine tofauti na samaki.
Naye Festol Brason alisema shida ya wenye viwanda ni kwamba samaki anapotoka kuvuliwa wao ndio hupanga bei ya kununua kitu ambacho hakiwanufaishi kwa chochote.
Alisema wao kama wavuvi ndio wanaopaswa kupanga bei kutokana na kukumbana na vikwazo mbalimbali ziwani, lakini hali ilivyo ni tofauti.
Habari hii ni sehemu ya uchunguzi wa chanzo cha hali ya umaskini na maisha duni ya wakazi wa visiwani, mialoni na maeneo karibu na Wilaya ya Muleba na Bukoba. Uchunguzi huu umefadhiliwa na Tanzania Media Fund (TMF).

Chanzo: Tanzania Daima

Jambazi auawa akutwa na silaha kali za kivita, mabomu 3, bunduki 3 AK 47na risasi 246



Na Theonestina Juma, Bukoba

JESHI la polisi Mkoani Kagera limefanikiwa kuua jambazi mmoja na kukutwa na silaha kali za kivita zikiwemo bunduki tatu, risasi 246 mabomu matatu ya kurushwa kwa mkono wakiwa katika harakati za kutaka kuvamia mgodi wa Tulawaka wilani Biharamulo.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa polisi Mkoani Kagera, Philip Kalangi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mapema leo asubuhi na kwamba tukio hilo lilitokea Juni 9,m mwaka huu saa 10.30 alafajiri Mavota Tulawaka wilayani humo.

Kamanda Kalangi alisema jambazi huyo aliuawa baada ya polisi kupambana na kundi la majambazi wasiojulikana idadi kwa dakika kadhaa,  ambao walizidiwa nguvu na mmoja kuuawa na wengine kukimbilia kusikojulikana.

Alisema baada ya jambazi huyo kuuawa alipopekuliwa alikutwa na silaha hizo, zikiwemo bunduki tatu aina ya AK 47 mbili zikiwa na namba UC 55231990,
UC 16081998 na pamoja  na bunduki aina ya Short gun mashine  (SMG) yenye namba 56128033262 ambapo mbili zikikuwemo kwenye mfuko wa kiroba ambayo alikuwa akiitumia katika kujihami katika tukio hilo.

Alisema mbali na kukutwa na silaha hizo pia alikutwa na sare pea mbili ambazo zinafanana na za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) buti jozi moja koti ya mvua ambazo zilikuwwa zimefungiwa bunduki mbili na magazine saba zilizokuwa na risasi.

Alisema mwili wa jambo huyo umehifadhiwa katika hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo  ambapo msako unaendelea wa kuwatafuta majambazi wengine waliokimbia kusikojulikana.

Chanzo-Rorya Kwetu Blog

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa