Na Amana Nyembo, Muleba
LICHA ya Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, kuwa na eneo kubwa la uvuvi, uchunguzi umebaini kuwa haina kiwanda hata kimoja cha kusindika minofu ya samaki.
Uchunguzi uliofanywa na wilayani hapa umebaini kuwa Muleba yenye eneo la mita za mraba 7,225 za maji ya Ziwa Victoria, visiwa 25 pamoja na Ziwa Burigi, wakazi wake kwa kiasi kikubwa wamejikuta wanabakia maskini kutokana na mapato makubwa kwenda nje ya wilaya.
Ofisa Uvuvi wa Wilaya hiyo, Symphorian Ngaiza, aliliambia Tanzania Daima kuwa kutokana na hali hiyo wakazi hao wamekuwa wakikosa ajira kwa vile viwanda vingi viko mkoani Mwanza.
Alisema kikwazo kikubwa kilichozuia wawekezaji kutovutika kuwekeza kwa kujenga viwanda ni miundombinu mibovu ya barabara za kuelekea maeneo ya uvuvi, ukosefu wa umeme, kiwanja cha ndege.
“Mathalani eneo la mwalo wa Kyamkwikwi lilitengwa kama sehemu inayofaa kwa ujenzi wa viwanda vya samaki lakini hakuna umeme, barabara na miundombinu nyingine, hivyo wanunuzi wa samaki wananunua na kupeleka viwandani kwao Mwanza,” alisema Ngaiza.
Hata hivyo, wakati halmashauri ikifikiria zaidi katika upatikanaji wa viwanda vya samaki, kumekuwapo na mgongano wa mawazo baina yake na wananchi wengi wanaodhani ujio wa viwanda hivyo, unatowesha samaki na hivyo kufanya kitoweo hicho kipande bei.
Licha ya wananchi hao kulitazama suala la ajira kama faida moja wapo kwao lakini hatua ya samaki wengi kwenda viwandani hawaliafiki wakati wao wakiendelea kuhangaika kukosa kitoweo.
Aidha, kwa upande wa pili uchunguzi umebaini kuwa wafanyabiashara hao wadogo hawana imani na viwanda kwa sababu huwanyonya katika suala zima la mauzo.
Wakizungumzia suala la samaki kwenda viwandani walisema tangu kuingia biashara ya kimataifa ya samaki wao kama wazawa wilayani Muleba hawanufaiki na ziwa Victoria.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Al Haji Masoud Abeid alisema uvuvi ulipoingiliwa na serikali kwamba samaki waende viwandani na hatimaye kuuza nje ya nchi wao wanapata shida.
Alisema samaki wanapovuliwa na kwenda viwandani ndio chanzo cha wananchi kukosa kitoweo hicho, hali inayowasababishia kula mboga nyingine tofauti na samaki.
Naye Festol Brason alisema shida ya wenye viwanda ni kwamba samaki anapotoka kuvuliwa wao ndio hupanga bei ya kununua kitu ambacho hakiwanufaishi kwa chochote.
Alisema wao kama wavuvi ndio wanaopaswa kupanga bei kutokana na kukumbana na vikwazo mbalimbali ziwani, lakini hali ilivyo ni tofauti.
Habari hii ni sehemu ya uchunguzi wa chanzo cha hali ya umaskini na maisha duni ya wakazi wa visiwani, mialoni na maeneo karibu na Wilaya ya Muleba na Bukoba. Uchunguzi huu umefadhiliwa na Tanzania Media Fund (TMF).
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment