na Antidius Kalunde, Bukoba
CHAMA Kikuu cha ushirika mkoani Kagera (KCU 1990 LTD) kimeshusha bei ya kahawa kwa kile ilichodai kutokana na kushuka kwa bei hiyo katika soko la dunia.
Mwenyekiti wa chama hicho, John Binunshu, alisema kushuka kwa bei hiyo kunatokana pia na bei ya mnadani kuporomoka kwa siku za hivi karibuni hivyo kulazimu KCU kubadilisha bei ya manunuzi tofauti kama ilivyokuwa awali.
Kutokana na kushuka kwa bei hiyo Binunshu aliwataka wakulima wa kahawa mkoani hapa kutokuwa na wasiwasi kuhusu taarifa hizo kwani wataendelea kupatiwa taarifa za bei kadiri hali ya soko itakavyokuwa.
Katika taarifa ya Meneja mkuu wa KCU, Vedasto Ngaiza, iliyosambazwa kwa mameneja wote wa vyama vya msingi vipatavyo 129 ambavyo vinaendelea na ununuzi wa kahawa kwa msimu huu ambao umefunguliwa rasmi mwezi Mei mwaka huu, bei ya kahawa imeteremka kutoka sh 1,350 hadi sh 1,100 kwa Kahawa aina ya Robusta maganda, huku robusta safi ikiuzwa kwa sh 2,200 kwa kilo.
Kahawa aina ya Arabica maganda imeshuka kutoka sh 1,550 hadi sh 1300 huku safi ikinunuliwa kwa sh 2,600.
Awali mabadiliko ya bei hizo yalionekana kuleta wasiwasi kwa wakulima huku baadhi yao wakihushutumu uongozi wa KCU kuamua kuteremsha bei mara baada ya kubaini kuwepo wingi za kahawa kwa wakulima.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment