Kabla ya Uhuru na hadi kufikia mwaka
1961, eneo la sasa la Mkoa wa Kagera, lilikuwa ni moja ya maeneo
yaliounda jimbo lililoitwa “Lake Province”. Jimbo hili lilijumuisha
Wilaya za Bukoba, Musoma, Shinyanga na Tabora. Baada ya uhuru mwaka 1962
mkoa ulibadilishwa jina na kuitwa ‘West Lake Region’ (Ziwa Magharibi)
na kujumuisha Wilaya 4 za Ngara, Biharamuro, Karagwe na Bukoba.
Uchumi wa wenyeji wa mkoa wa Kagera
ulijikita katika mashamba ya migomba na kahawa. Chakula chao kikuu ni
ndizi katika aina zake mbalimbali. Katika mashamba yao hulima mazao
mengine kufuatana na msimu. Mazao hayo ni pamoja na maharage, mihogo,
mahindi na mboga.
Baada ya kuja kwa wazungu waliongeza
ulimaji wa kahawa kama zao la biashara lililowasaidia kujiongezea
kipato. Wakazi wa asili ya Kagera ni wabantu na wengi wao wanaasili ya
Bunyoro. Wanaongea lugha sawa na ile ya Wanyoro, Wanyankole, Watoro na
Wakiga. Busubi na Bugufi wana lugha na desturi sawa na Watusi, Wahutu na
Waha. Lakini makabila hayo ni ya Wabantu wa Ziwa (Interlacustrine
Bantu) na yanafanana mila na desturi.
Makundi hayo yaligawanyika katiya
wachungaji (Bahima) ambao walitawala na wakulima (Bairu) ambao
walitawaliwa na mara nyingi kudharauliwa. Bahima (Balangira) walikuwa na
koo chache zipatazo 20 na walitawaliwa na Wahinda, Wabito na Wankango
Bairu walikuwa na koo kama 130 zenye mashina 24 ambayo kiasili walikuwa
Bairu lakini kwa kuoa katika Bahima au kufanya kazi kwa Watemi
walipandishwa hadhi na kuwa Bahima (Batware). Kila ukoo uliitwa jina la
Baba mwanzilishi wake na kina ukoo ulikuwa na kitu walichokatazwa kula
(Omuziro) na mnyama walioshirikishwa nae (Ekyerumono).
Kabla na baada ya kuja kwa wakoloni mkoa
wa Kagera ulikuwa na utawala wa Kimila (Chiefdoms) uliogawanyika katika
himaya 8. Himaya hizo ni pamoja na Kyamutwara, Kihanja (Kanazi),
Kiziba, Ihangiro, Bugabo, Karagwe, Biharamulo (Rusubi) na Maruku
(Bukara).
Baadhi ya Watemi waliotawala himaya hizo
ni pamoja na Emmanuel Rukamba (Kyamtwara), Rumanyika (Karagwe),
Kasusura (Biharamulo), Lugomola (Bukara), Rutinwa (Kiziba), Kayo za
(Bugabo), Kahigi (Kihanja) na Nyarubamba (Ihangiro). Kila mtemi alikuwa
na walinzi wake walioitwa Warugaruga.
Makabila yanayopatikana hivi sasa katika
mkoa wa Kagera ni pamoja na Wahaya ambao wanapatikana zaidi katika
wilaya za Bukoba, Muleba na Missenyi. Makabila mengine ni Wanyambo,
wanaopatikana katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa, Wasubi katika wilaya
ya Biharamulo, Wahangaza wanaopatikana katika Wilaya ya Ngara. Pia kuna
Waha, Wazinza and Warongo.
Chanzo Tovuti ya Mkoa wa Kagera
0 comments:
Post a Comment