Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja
Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu (wa tatu kulia), akikata utepe kuashiria
uzinduzi rasmi wa mashamba darasa ya kilimo bora cha mihogo na migomba iliyozalishwa kwa njia ya chupa (tissue
culture), kwa ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia (OFAB) katika
vijiji vya Bunazi na Kashaba wilayani Missenyi mkoani humo leo. Shamba
hilo litasimamiwa na Kikundi cha Ushirika cha Batekaka. Kutoka kulia ni
Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali, Denis Mwila, Mwenyekiti wa Kikundi
hicho, Belington Kyokwete, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya
Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa
Utawala na Fedha, Shaban Hussein na Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya
ya Missenyi, Projestus Tegamaisho.
Ofisa Ugani wa Kata ya Kasambya, Hakika Ibrahim, akizungumza kataika uzinduzi huo.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi
wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein, akizungumza katika uzinduzi huo.
Mtafiti kutoka OFAB, Dk. Beatrice Lyimo akizungumza katika uzinduzi huo.
Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku akielezea mbegu hiyo mpya ya migomba.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu (wa tatu kulia), Mwakilishi
wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein na
Mkuu wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali, Denis Mwila (kulia), pamoja na Mwenyekiti wa Kikundi cha Ushirika cha Batekaka, Belington Kyokwete, wakiwa wameshika mmoja wa mche wa mgomba katika uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akipanda mche wa mgomba kwenye shamba darasa katika Kijiji cha Bunazi.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi
wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein, akipanda mgomba kwenye shamba
darasa hilo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akiwahutubia
wananchi wa Kijiji cha Kashaba kabla ya kuzindua shamba darasa la zao la
mhogo.
Usikivu katika uzinduzi huo. Kutoka kulia ni Mtafiti kutoka OFAB, Dk. Beatrice Lyimo, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Adam Swai na Mwakilishi
wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein,
akipanda mgomba kwenye shamba darasa hilo.
Wananchi wa Kijiji cha Kashaba wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja
Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akimpongeza kijana, Shafii Idrisa wa
Kijiji cha Kashaba ambaye ameamua kujishughulisha na kilimo kijijini
hapo badala ya kukimbilia mjini na kuendesha bodaboda kama walivyofanya
wenzake.
Mtafiti wa mazao ya jamii ya mizizi
kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku, Jasmeck Kilangi, akimueleza
Mkuu wa Mkoa namna ya upandaji wa zao la mihogo.
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu, akipanda mbegu ya
mhogo katika shamba darasa katika Kijiji cha Kashaba.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Missenyi, Projestus Tegamaisho, akitoa shukurani baada ya uzinduzi huo.
Na Dotto Mwaibale, Missenyi Kagera
WAKULIMA wilayani Missenyi Mkoani
Kagera wametakiwa kuyatumia matunda ya tafiti za kisayansi yanayoletwa
na wataalamu kuboresha kilimo chao na kuongeza tija kwenye mazao
mbalimbali ili kuweza kuchangia malengo ya nchi kufikia uchumi wa kati.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa
Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salumu Mustafa Kijuu wakati akizungumza
na wanakikundi cha Batekaka kwenye Kijiji cha Bunazi na kikundi cha
Obumo wa Kijiji cha Kashaba kwenye uzinduzi wa zoezi la utoaji wa
Mbegu bora za zao la migomba iliyozalishwa kwa njia ya chupa na Mihogo
yenye ukinzani na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia zoezi
lililofadhiliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)
kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo Tanzania (OFAB).
Alisema Kilimo pekee ndicho kinachoweza
kuwakwamua wananchi kutokana na wimbi la umasikini lakini akasisitiza
kuwa kilimo hicho lazima kizingatie mbinu zote za kilimo bora ambacho
kitamuwezesha mkulima kulima eneo dogo na kupata mavuno makubwa na
kuchana na kile cha zamani na mazoea cha kulima bila kutumia mbinu za
kisayansi.
“Tafiti nyingi zinafanyika hapa nchini
lakini zinaishia kwenye makabati na haziwafikii wakulima ambao ndio
walengwa wa tafiti hizo lakini nawashukuru COSTECH kwa kushirikiana na
watafiti wetu kwa kutuletea mbegu hizi bora mlizozitafiti na
kujihakikishia kuwa zinauwezo wa kutatua changamoto za wakulima wetu na
kuongeza tija”Alisema Mkuu huyo wa mkoa wa Kagera.
Mkuu huyo wa mkoa wa Kagera ameshukuru
COSTECH kwa kuamua kusaidia kuwafikishia wakulima mbegu bora za MIhogo
na Migomba na kuanzisha mashamba darasa kwenye wilaya zote za mkoa huo
ambayo yatawezesha wakulima wengi zaidi kujifunza kwa vitendo na hatimae
kuweza kuinga mbinu hizo za kisasa zilizotafitiwa na kwenda kuzitumia
kwenye mashamba yao baada ya kuona matunda yatokanayo na mshamba hayo.
Meja Jenerali Mstaafu Kijuu pia
alibainisha kuwa hivi sasa mkoa umejipanga kuhakikisha kila wilaya
inakuwa na kiwanda kimoja kikubwa cha kuchakata zao moja na kila wilaya
kuwa na zao moja la biashara hali ambayo itasaidia katika kuwahakikishia
masoko ya uhakika wa mazao ya wakulima na hivyo kuongeza ari ya
uzalishaji kwenye maeneo mengi.
Aliwataka maofisa ugani kuwasaidia
wakulima katika kutumia mbinu bora za kilimo ili kuweza kuzalisha kwa
tija na kuwataka kila mmoja kuwa na shamba lake ambalo wakulima wataweza
kuona na kujifunza kwao badala ya kuwa wazungumzaji tuu bila wao
kuonyesha mfano.
Awali akizungumza malengo ya mpango huo
wa ugawaji mbegu na malengo yake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa
COSTECH ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa COSTECH, Shabani
Hussein alisema kuwa mpango huo ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya
tume hiyo kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wake ya kuhakikisha
matokeo mazuri ya sayansi na teknolojia yanawanufaisha walengwa kwenye
maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kuwa ili kuweza kufikia adhima
ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa Tanzania ya viwanda ni lazima suala
la kilimo lipewe msisitizo wa kutosha ili kuweza kuzalisha malighafi za
kutosha kulisha vwanda vitakavyojengwa lakini bila kilimo mpango huo
unaweza kukwama.
Alisema pamoja na COSTECH kuwa mshauri
mkuu wa serikali katika masuala yote yanayohusu sayansi,teknolojia na
uvumbuzi lakini pia wanashirikiana na watafiti na vituo vya utafiti
katika kusaidia kufikisha matunda hayo ya tafiti kwa wakulima ili
kusaidia kuongeza tija na kuwakwamua wakulima katika wimbi la umasikini.
‘’Naamini mbegu hizi tulizozileta leo na
mashamba darasa haya yatakuwa chachu kwa wakulima wengine kuona na
kujifunza mbinu bora za kilimo kwenye maeneo yao na baadae mbinu hizo
kusambaa kwa wakulima wengine kwenye maeneo ya jirani" alisistiza
Hussein
Mwakilishi huyo wa Mkurugenzi mkuu wa
COSTECH alisema mbegu hizo bora za Migomba safi isiyo na magonjwa pamoja
na mbegu bora ya mihogo aina ya Kiroba yenye ukinzani na magonjwa ya
batobato kali na michirizi ya kahawia itagaiwa kwenye vikundi kwenye
wilaya zote za mkoa huo wa Kagera na kupewa mbinu bora za kilimo kutoka
kwa wataalamu.
Mkuu wa WIlaya ya Missenyi, Luteni
Kanali Denis Mwila amewapongeza COSTECH na OFAB kwa kutimiza ahadi yao
ya kuwaletea wakulima mbegu hizo na kuwaahidi kuwa watasimamia mashamba
darasa hayo vizuri hadi kuvuna ili wakulima waweze kuona umuhimu wa
sayansi na mbinu bora za kilimo kwenye uzalishaji.
“ Tumepata bahati kubwa sana wana
Missenyi uzinduzi huu kimkoa kufanyika kwenye wilaya yetu maana zipo
wilaya nyingi lakini bahati imetuangukia sisi hivyo tuyatunze mashamba
na mbegu hizi na tusiwaangushe COSTECH waliotuletea mbegu hizi bora”
alisema Mwila.
Pia ameiomba serikali kuangalia
uwezekano wa kutoa ruzuku za pembejeo mara mbili kwa mwaka kwenye mkoa
wa Kagera kutokana na kuwa na misimu miwili ya kilimo badala ya
kuwapatia pembejeo msimu mmoja pekee sawa na mikoa mingine yenye msimu
mmoja.
Ameahidi kushirikiana na COSTECH na
wataalamu katika kila aina ya teknolojia na mbinu bora inayowafaa
wakulima wa wilaya yake ili kuwawezesha kuzalisha chakula kingi na mazao
ya biashara ambayo wananchi watauza na kujipatia kipato.
Kwa upande wao wakulima kwenye vikundi
hivyo wameahidi kuyatunza na kuyalinda mashamba hayo na mbegu hizo ili
kuzizalisha kwa wingi na kuweza kuwasambazia wakulima wengine kwenye
maeneo yao ili kujihakikishia usalama wa chakula kwa kulima zao bora la
muhogo na kulima migombo bora iliyozalishwa kwa njia ya chupa baada a
migomba yao kushambuliwa sana na ugonjwa hatari wa mnyauko.
Pia wakapaza sauti zao kwa serikali
kuhakikisha wanawapelekea mbegu bora za mahindi na mazao mengine kwa
wakati kupitia mpango wa serikali wa kutoa ruzuku ya pembejeo maana
kilimo mbili za mbegu bora ya mahindi wananunua kwa wastani wa shilingi
15 bei ambayo ni kubwa kwa wakulima wengi.
0 comments:
Post a Comment