SHULE ya Msingi Mugeza Mseto inakabiliwa na ukosefu wa vyoo na bafu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Philemon Coelestine, alibainisha hayo
juzi alipokuwa akitoa taarifa ya shule kwa Balozi wa China nchini
aliyetembelea shule hiyo na kutoa vitabu vyenye thamani ya sh milioni
tano.
Coelestine alisema mabweni yanayotumiwa na wanafunzi ambao ni walemavu hayakidhi mahitaji ya wahitaji.
Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa nyumba za watumishi, usafiri
kwa wanafunzi na uchakavu wa miundombinu ya majengo, umeme na viwanja
vya michezo.
Alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 650 kati yao walemavu
wasioona 40, walemavu wa ngozi ni 40 na walemavu wa viungo ni 52.
Hata hivyo alisema pamoja na changamoto hizo shule hiyo imekuwa
ikiendelea kufanya vizuri katika matokeo ya kumaliza elimu ya msingi
kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2010/13.
Alisema mwaka 2013 wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya
msingi walikuwa 66, kati yao wanafunzi 40 ambayo ni asilimia 61
walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Balozi wa China Tanzania, Dk. Lu Youging, alisema wanafunzi wenye
ulemavu wanao uwezo wa kujitegemea na kutoa mchango wao kwa maendeleo
ya taifa.
Aliwashauri wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Ado Mapunda, alisema
atasimamia msaada huo uliotolewa na Ubalozi wa China ili utumike kwa
malengo yaliyokusudiwa.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment