KATIBU wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(BAWACHA) Kata ya Runazi, Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera, Oliva
Evodius, ameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.
Kifo hicho ambacho kimeacha maswali mengi, kinahusishwa na mambo ya siasa, lakini pia wapo wanaokihusisha na mambo binafsi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Diwani wa Kata ya Runazi,
Constantine N’kwenge, alisema kuwa katibu huyo ameuawa usiku wa kuamkia
Jumamosi Aprili 6, majira ya saa nne usiku baada ya kuvamiwa na watu
wasiojulikana na kumshambulia kwa mapanga akiwa nyumbani kwake.
Mume wa marehemu, Evodius Malembeka, aliliambia gazeti hili kuwa marehemu alikutwa na tukio hilo akiwa naye.
Alisema Oliva alivamiwa wakati akiingia chumbani mwake akitokea bafuni kuoga.
Msemaji wa familia hiyo, Raphael Sostenes Zitta, ameitaka serikali
kupitia vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi na kuongeza umakini katika
uchunguzi wa matukio ya mauaji yanayofanyika na kuhatarisha usalama wa
wananchi.
Jeshi la Polisi mkoani Kagera, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo
na kwamba linawashikililia watu wawili wakati likiendelea kufanya
uchunguzi zaidi kubaini wahusika wa mauaji hayo.
Wakati huo huo, watu wawili wamelazwa katika hospitali teule wilayani
hapa baada ya kujeruhiwa katika matukio tofauti yaliyotokea mwishoni
mwa wiki iliyopita.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali hiyo, Haula Balikaho, amewataja
waliojeruhiwa kuwa ni Frank Wera Mussa, mkazi wa Runazi na Chola
Rufungulo, mkazi wa Kisenga, Kata ya Nemba, wilayani humo.
Alisema Frank amejeruhiwa kichwani baada ya kupigwa na wananchi wenye
hasira wakati Chola amejeruhiwa jicho la kulia baada ya kupigwa risasi
na majambazi akitokea kwenye mnada wa ng’ombe.
Haula alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na wanaendelea
kupata matibabu katika hospitali hiyo na mmoja wa majeruhi hao, Frank
Mussa, anatibiwa chini ya uangalizi wa polisi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment