WATANZANIA waishio mpakani mwa nchi za Tanzania na Uganda eneo la
Mtukula lililopo wilayani Missenyi, Kagera, wamesema wamechoshwa na
vitendo vinavyofanywa na askari wa Uganda kuingia upande wa Tanzania
kukamata wahalifu wakiwa na silaha bila kufuata sheria.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotajwa majina,
wananchi hao walisema juzi, saa 11 jioni askari wanne waliotokea
Mbalala, Uganda walivuka mpaka kuwafuatilia wezi wa pikipiki waliokuwa
upande wa Tanzania.
Walisema katika kurupushani za kuwakamata watuhumiwa hao walikimbia
na kuingia ndani ya Kituo cha Polisi Mtukula kilichopo Tanzania.
Walisema wakati mtuhumiwa huyo akikimbilia katika kituo hicho, askari
hao walianza kumfyatulia risasi ambazo hazikumpata mlengwa na badala
yake kuwajeruhi watu wawili.
Walisema baada ya askari huyo kuingia katika kituo hicho cha polisi,
alikamatwa na kunyang’anywa bunduki huku wenzake watatu walipoona
mwenzao amekamatwa waliondoka na vijana wawili ambao ni Watanzania
kuelekea nao Uganda.
Wananchi hao walisema imekuwa ni kawaida kwa askari wa Uganda
kuingia upande wa Tanzania na kuwakamata watu wanaowatuhumu na
kuwapeleka Uganda bila kufuata utaratibu wa mipaka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alipohojiwa
kuhusiana na tukio hilo alisema hayuko tayari kulizungumzia suala hilo
linalogusa nchi mbili.
Alisema tukio hilo linashughulikiwa na vyombo vya ulinzi na usalama, ili taarifa zitumwe Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.
Chanzo ;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment