SHILINGI milioni 8.8 zimekusanywa katika harambee ya kuchangia
ujenzi wa Kituo cha Afya cha Buganguzi, wilayani Muleba iliyoratibiwa
na Umoja wa Maendeleo ya Buganguzi (Bugadea).
Akizungumza katika harambee hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki,
Mwenyekiti wa umoja huo ulioasisiwa na wakazi wa Kata ya Buganguzi
waishio Dar es Salaam, Rodrick Lutembeka, alisema kiasi hicho
kilitokana na michango ya wananchi, pia ofisi ya mkuu wa mkoa
imechangia sh milioni 1.8 na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Muleba imeahidi kuchangia sh milioni 30.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe, aliyekuwa mgeni rasmi
kwenye harambee hiyo iliyofanyika kwenye makao makuu ya kata hiyo,
amehimiza wakazi mkoani humo kuepuka tabia ya kusubiri misaada na
badala yake wachangie miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Alisema juhudi za wananchi lazima zionekane kwanza katika miradi yao kabla ya kuomba misaada.
Alisema ni aibu kuomba misaada kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali hata kwa vitu ambavyo viko ndani ya uwezo wa wananchi.
Massawe alisema miradi mingi ya maendeleo katika Wilaya ya Muleba
ukiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, haikutekelezwa kwa kasi ya
kuridhisha kwa kile alichodai ni wananchi kurubuniwa na kushindwa
kuchangia nguvu zao.
Katika kuhamasisha ujenzi wa Kituo cha Afya Buganguzi
kinachokadiriwa kugharimu zaidi ya sh milioni 600, Mkuu wa Mkoa
ameshauri kila kaya kuchangia sh 20,000 au vitu vyenye thamani hiyo,
ili kufikia lengo la kata hiyo kuwa na huduma hiyo.
Alipongeza wakazi wa Buganguzi walioko nje ya mkoa chini ya
mwavuli wa Bugadea kwa kuwa na wazo la kukumbuka nyumbani na kushiriki
kuchangia maendeleo. Kata ya Buganguzi iliyo katika Tarafa ya Nshamba,
ina vijiji vya Buhanga, Bushemba, Katare na Kashozi.
Mwenyekiti wa Bugadea, Lutembeka, alihimiza wakazi wa kata hiyo
kuunganisha nguvu katika ujenzi wa kituo hicho na miradi mingine ya
maendeleo.
Alisema hakuna sababu ya kushindwa kufanya hivyo kwa kuwa fursa
zilizopo, ikiwemo ardhi na rasilimali vinatosheleza kutekeleza
ujenzi huo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Rembris Kipuyo, alisema serikali
itaendelea kushirikiana na wananchi wa kata hiyo hadi kukamilika kwa
kituo hicho.
Diwani wa Buganguzi, Onesmo Yegira alipongeza uamuzi wa Bugadea
kuandaa tamasha hilo la maendeleo lililopambwa na burudani pamoja na
michezo mbalimbali ikiwa ni njia ya kukutanisha wakazi kuchangia
maendeleo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment