Home » » Tuhuma za ufisadi: CAG aiokoa CCM Bukoba

Tuhuma za ufisadi: CAG aiokoa CCM Bukoba

  Meya Amani akwepa kura ya kutokuwa na imani, ajiuzulu
  Kama ilivyokuwa kwa Balozi Kagasheki bungeni, Pinda ahusika
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoah
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoah, amekiokoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka kwenye mgawanyiko uliodumu miongoni mwa madiwani wake kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Taarifa ya CAG kuhusu utata uliodaiwa kuwapo kwenye mikataba iliyosainiwa kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo, imebaini ‘madudu’ yaliyosababisha kujiuzulu kwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk Anatory Amani.
Hoja ya kuwapo kwa mikataba yenye utata ikihusishwa na ufisadi, ikidaiwa kukiukwa taratibu na sheria ya manunuzi ya umma, iliwagawa madiwani wa CCM katika manispaa hiyo na kuathiri utendaji wa baraza la madiwani, lenye wawakilishi kupitia vyama vya upinzani.
Pamoja na asili ya mgogoro huo kuwa katika mikataba yenye utata, mpasuko kwa madiwani wa CCM, ulihusishwa na ‘mbio za ubunge’ wa Bukoba Mjini kwa Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Pande mbili za madiwani hao zikagawanyika katika kuwaunga  Dk Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Kagasheki.
Wawili hao walishawahi kukutanishwa katika vikao mbalimbali vya CCM kuanzia ngazi ya wilaya hadi Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyowahoji mjini Dodoma, Agosti mwaka jana.
Kufuatia kuhitimishwa kwa ukaguzi wa CAG na kugundulika kwa kasoro kadhaa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alimshauri Dk Amani kutumia busara ya kujiuzulu wadhifa huo kwa manufaa ya wananchi.  
Akitangaza hatua hiyo jana, Dk Amani ambaye pia ni diwani wa kata Kagondo, alikubaliana na ushauri wa Pinda, kuwa ajiuzulu kwa hiari yake, kabla ya madiwani kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Kujiuzulu kwa Dk Amani, kumekuja siku 27 baada ya hatua kama hiyo kuchukuliwa na Mbunge wa Bukoba Mjini aliyekuwa pia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Wakati Dk Amani aliepuka kura ya kutokuwa na imani kutoka kwa madiwani jana, Balozi Kagasheki, alijiuzulu Desemba 21, mwaka jana, muda mfupi kabla ya tamko la Rais Jakaya Kikwete, kuwawajibisha yeye na wenzake watatu. 
Mawaziri wengine waliokuwa kwenye ‘kapu moja’ na Balozi Kagasheki, ambao Rais Kikwete alisitisha uteuzi wao kutokana na kashfa zilizoibuka wakati wa Operesheni Tokomeza Majangili ni pamoja na Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi).
Wengine walikuwa na wizara walizokuwa kwenye mabano ni David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa). 
Taarifa ya Pinda kumshauri Dk Amani ajiuzulu, ilisomwa na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Agrey Mwanri.
Mwanri alisoma taarifa hiyo katika mkutano ulioitishwa na ofisi ya Waziri Mkuu, ikiwa ni hitimisho la taarifa ya ukaguzi wa CAG katika manispaa hiyo na ushauri wake kwa serikali.
Pinda, kupitia kwa Mwanri, alisema kufuatia tuhuma zinazomkabili Dk Amani, kusaini mikataba yenye utata ni bora ajiuzulu kwa manufaa ya umma.
Mbali na Dk Amani,  taarifa ya Pinda iliagiza aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo, aliyehamishiwa wilaya mpya ya Momba mkoani Mbeya, Khamis Kaputa, avuliwe madaraka hayo.
Pia, Pinda aliagiza kuvuliwa madaraka kwa wakuu wa idara za uhandisi, Mhandisi Steven Nzihirwa, kitengo cha manunuzi, Baraka Marwa na Mweka Hazina Amduni Uromi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Pinda, aliagiza uongozi wa manispaa hiyo kupitia upya taarifa ya CAG na kutoa maelezo yake kwa Katibu Mkuu (Tamisemi) ndani ya siku saba, baada ya kukabidhiwa taarifa ya CAG.
Kabla ya tamko la Pinda, Utouh aliwasilisha ripoti ya uchunguzi iliyobaini kuwapo mikataba iliyosainiwa na manispaa hiyo, chini ya uongozi wa Dk Amani.
Mikataba hiyo ilibainika kukiuka taratibu za matumizi ya fedha za umma, ikiwamo kutojadiliwa na kikao cha baraza la madiwani.
Utouh, alisema kuwa mikataba hiyo ilisababishia kuzuka kwa mgogoro na hasara kubwa kwa manispaa hiyo, ikiwamo kukosa mapato ya zaidi ya Shilingi milioni 256.2 katika kipindi cha mwaka 2012/2013 na 2013/2014.
Fedha hizo ni ambazo zingetokana na ushuru wa soko kuu la Bukoba, uliosimamishwa kutokana na mgogoro huo.
Baadhi ya mikataba  iliyothibitishwa na CAG kusainiwa kinyume cha utaratibu ni wa ujezi wa soko kuu jipya na la kisasa na ujenzi wa jengo la kitega uchumi lililopo eneo la kituo kikuu cha mabasi.
Miradi mingine ni ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi eneo la Kyakailabwa, zabuni ya kukusanya ushuru katika kituo kikuu cha mabasi  na mradi wa upimaji viwanja.
Utouh, alisema Pinda, aliiomba ofisi ya CAG kufanya ukaguzi maalum katika manispaa ya Bukoba, kutokana na kuwapo kutoelewana kulikosababisha makundi na vikao vya kisheria vya madiwani kutofanyika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, aliwataka madiwani wa halmashauri hiyo na watendaji kuipokea taarifa hiyo na maelekezo ya serikali kwa manufaa ya wananchi wa Bukoba.
Kanali Massawe, alisema kuwa mgogoro huo ambao umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, umesababisha kukwamisha miradi ya maendeleo ya wananchi.
Kwa mujibu wa Kanali mstaafu Massawe, miongoni mwa miradi hiyo ilipaswa kufadhiliwa na Benki ya Dunia ikiwa na thamani ya Shilingi bilioni 18.5. 
Pia, alisema madiwani wa manispaa hiyo walishindwa kufanya vikao vya kisheria, kikiwamo cha kupitisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2014/2015.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa