Home » » Polisi, TRA watuhumiana kuwalinda wauza viroba

Polisi, TRA watuhumiana kuwalinda wauza viroba

Jeshi la Polisi Tanzania
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga amesema watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani hapa wanashirikiana na wafanyabiashara wa pombe kali aina ya viroba wanaokwepa kodi.
Kauli ya Kamanda Mayunga imekuja siku chache baada ya Kaimu Meneja wa TRA Kagera kuwatuhumu polisi kuwalinda wafanyabiashara hao wanaotokea Uganda kupitia njia ya maji katika Ziwa Victoria.

Akizungumza mjini hapa jana, Kamanda Mayunga alisema wafanyabiashara hao wanapita kwenye geti la Mtukula ambapo watumishi wa mamlaka hiyo wapo kwa ajili ya kukagua na kutoza kodi mizigo inayoingizwa nchini.

Kamanda huyo alikiri kuwapo kwa askari wasio waaminifu ambao wanalichafua jeshi la polisi, hivyo aliahidi kupambana nao huku akisisitiza kwamba siyo kweli kuwa jeshi hilo linakwamisha utendaji wa TRA kama ilivyotuhumiwa awali.

“Suala la pombe kali aina ya viroba nimefanya uchunguzi nimegundua vinaingia kupitia Mtukula eneo ambalo TRA wapo ‘responsible’ (wanawajibika) kukusanya kodi baada ya hapo kuna beria ya polisi na Tanroads Misenyi” alisema na kuongeza:

“Cha kushangaza TRA wanawakimbiza wafanyabiashara waliovusha viroba huku Karagwe… hapo lazima kutilia shaka kwamba wanapitishaje mizigo yao kama hawashirikiani na maofisa wa mamlaka hiyo?” alihoji Kamanda Mayunga.

Kamanda huyo alisema wafanyabiashara wanaoingiza viroba kwa wingi hawapiti njia za panya, badala yake ina aminika kwamba wanavusha kwa njia halali kwa kuwahonga maofisa wanaokua kwenye vizuizi.

“Hii ni vita nyepesi tukishirikiana vizuri na TRA ninaahidi tutalimaliza tatizo hili tutawakamata wanaokwepa kodi, wanaotoa na kupokea rushwa.”

 “Tabu tunayoiona hapa hatujashirikishwa ipasavyo, ninaahidi kuwapa msaada maofisa wa mamlaka hiyo wakati na mahali popote nasisitiza kwamba hatujashindwa iwapo tutashirikishwa kwenye operesheni za kuwakamata wafanyabiashara hao,” aliongeza kusema Kamanda Mayunga.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kagera Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa